Mada kuu ya tatu
Dakika 2 za kusoma ·
Yaliyomo
Fasihi Kwa Ujumla
Maana ya fasihi
Fasihi ni nini? Ni kazi ya sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe wa msanii kwa hadhira.
Hadhira ni wapokeaji wa kazi ya fasihi.
Sanaa Na Matawi Ya Fasihi
Fasihi ni moja ya sanaa katika jamii.
Sanaa ni ufundi na upekee wa kuwasilisha mawazo na ujumbe ulio katika fikra za binadamu.
Ufundi wa sanaa hujitokeza kupitia uzuri unaovutia macho na hisia za watu.
Mifano ya sanaa ni
- uimbaji
- michoro
- uchongaji
- maandishi
- ususi
- n.k.
Kila umbo la sanaa lina nyenzo zake. Mfano, uchongaji unahitaji ubao, msumeno, rangi n.k.
Matawi Ya Sanaa
Fasihi ni tawi la sanaa linalotumia nyenzo ya maneno.
Fasihi hutumia maneno ya kawaida kuwasilisha ujumbe kwa ustadi mkubwa.
Tawi hili hujitokeza katika maandishi na masimulizi yanayowasilishwa kwa ustadi mkubwa.
Dhima Au Kazi Za Fasihi Katika Jamii
Fasihi ina kazi au faida gani katika jamii?
- Kuelimisha jamii.
- Kuendeleza utamaduni.
- Kusisimua hadhira.
- Kukuza lugha.
- Kusaidia kuikomboa jamii.
- Kuhifadhi historia.
- Kuburudisha jamii.
Aina Za Fasihi
Fasihi simulizi
Ni aina ya fasihi inayowasilishwa kwa njia ya mazungumzo na utendaji.
Fasihi simulizi ni kongwe zaidi kuliko fasihi andishi.
Fasihi andishi
Ni aina ya fasihi inayowasilishwa kwa maandishi.
Kazi nyingi za fasihi andishi zimetokana na fasihi simulizi. Mfano ni mashairi, riwaya na tamthiliya.
Fasihi andishi ilianza pale tu maandishi yalipogundulika.
Tofauti Kati Ya Fasihi Simulizi Na Fasihi Andishi
Umbo la asili
- Fasihi simulizi: umbo lake la asili ni masimulizi.
- Fasihi andishi: umbo lake la asili ni maandishi.
Njia ya uwasilishaji
- Fasihi simulizi: huwasilishwa kwa njia ya mdomo.
- Fasihi andishi: huwasilishwa kwa maandishi.
Ubunifu na mabadiliko
- Fasihi simulizi: hubuniwa na hupokea mabadiliko ya papo kwa hapo.
- Fasihi andishi: huchukua muda kuandikwa na haipokei mabadiliko ya papo kwa hapo.
Umiliki
- Fasihi simulizi: ni mali ya jamii nzima.
- Fasihi andishi: ni mali ya mwandishi.
Hadhira
- Fasihi simulizi: hushirikisha hadhira moja kwa moja katika utendaji.
- Fasihi andishi: haishirikishi hadhira, na aghalabu haimjui mtunzi.
Uhifadhi
- Fasihi simulizi: huhifadhiwa kichwani.
- Fasihi andishi: huhifadhiwa katika maandishi.
Muundo
- Fasihi simulizi: muundo wake ni sahili, yaani moja kwa moja.
- Fasihi andishi: muundo wake aghalabu ni changamano.
Kubagua
- Fasihi simulizi: haibagui wanaojua kusoma na wasiojua kusoma.
- Fasihi andishi: hubagua wanaojua kusoma na wasiojua kusoma.
Maswali
- Fasihi ni zao la jamii. Nini maana ya kauli hii?
- Fasihi yenye manufaa kwa jamii ni ile inayoelimisha jamii. Thibitisha kauli hii kwa kutumia methali zifuatazo:
- Nenda na uchwao usiende na uchao.
- Siyo kila king'aacho ni dhahabu.
- Eleza umuhimu wa vipengele vifuatavyo vya fasihi:
- Mandhari
- Wahusika
- Dhamira
- Toa maelezo mafupi kuhusu vipengele vifuatavyo vya fasihi:
- Falsafa
- Mtazamo wa mwandishi
- Fasihi ya Mtanzania ni miongoni mwa mambo yaliyopitwa na wakati, hasa wakati huu wa utandawazi. Jadili kauli hii.
