Mada kuu ya sita
Dakika 2 za kusoma ·
Yaliyomo
Uandishi Wa Insha
Maana Ya Insha:
Insha ni mfuatano wa tungo wenye mtiririko. Tungo hizi zinaeleza kuhusu mada fulani.
Mawazo katika insha hupangwa katika aya.
Muundo Wa Insha
Insha ina sehemu hizi
- Kichwa cha insha: Huandikwa kwa herufi kubwa na kupigiwa mstari. Huandikwa kwa maneno yasiyozidi matano. Huzingatia wazo kuu la insha.
- Utangulizi: Huu ndio mwanzo wa insha. Hueleza kwa ufupi juu ya jambo lililoandikwa kwenye kichwa cha insha.
- Kiini cha insha: Hii ndiyo sehemu kuu kabisa ya insha. Sehemu hii hueleza kwa undani na kwa urefu juu ya mada au jambo lililotambulishwa. Maelezo hayo hutolewa katika aya mbalimbali.
- Mwisho wa insha: Hutoa msisitizo na majumuisho. Pengine hutoa pia ushauri kwa ufupi juu ya yote yaliyoandikwa. Hapa ndipo panapoonekana msimamo, maoni na falsafa ya mwandishi.
Aina Za Insha
Insha za kisanaa
Hizi ni insha zinazoandikwa kwa lugha ya kifasihi na yenye mvuto.
Hutumia misemo, nahau, methali na tamathali za semi. Mfano wa tamathali za semi ni lakabu, takriri, chuku na kadhalika.
Sifa Za Insha Za Kisanaa
- Kuwa na uteuzi wa maneno.
- Kuwa na lugha ya kisanaa.
Hatua Za Uandishi Wa Insha
- Kubaini la kuandika.
- Insha ibebe ujumbe fulani.
- Insha lazima iwe na dhamira au wazo kuu.
- Insha lazima ihusishe visa na mikasa.
- Insha iwe na uzuri wa kisanaa.
- Insha izingatie uteuzi wa maneno.
- Insha lazima izingatie kanuni za uandishi.
Insha zisizo za kisanaa (insha za hoja)
Hizi ni insha zinazotumia lugha ya kawaida. Huelezea mtiririko wa mawazo juu ya kitu fulani.
Mfano ni insha za wasifu. Hizi ni insha zinazoeleza kuhusu sifa binafsi za mtu au kitu fulani.
Kimuundo, insha za wasifu huwa na sehemu kuu tatu. Sehemu hizo ni utangulizi, kiini na hitimisho.
Maswali
- (a) Insha ni nini?
(b) Eleza sehemu kuu za insha.
- Fafanua mambo muhimu yanayohitajika katika uandishi wa insha.
- Taja sifa kuu moja ya insha ya wasifu.
- Uandishi wa insha hukuzaje lugha?
- Eleza maana ya maneno yafuatayo:
(a) Aya
(b) Nukta
(c) Mkato
- Kwa kutumia maneno yasiyozidi 200, andika insha ya wasifu kuhusu mlima Kilimanjaro.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 45
