Mada kuu ya nne
Dakika 6 za kusoma ·
Yaliyomo
Fasihi Simulizi
Maana ya fasihi simulizi
Fasihi simulizi ni nini?
Ni sanaa au aina ya fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya mdomo.
Mfano: hadithi, nyimbo na kadhalika.
Dhima, kazi au umuhimu wa fasihi simulizi
- Kuelimisha jamii.
- Kuburudisha jamii.
- Kufunza utamaduni wa historia.
- Kukuza lugha.
- Kukomboa jamii.
- Kuhamasisha utendaji.
- Kunoa akili.
- Kuipa jamii muelekeo.
- Ina mchango katika fasihi andishi.
Tanzu Za Fasihi Simulizi
Fasihi simulizi ina tanzu au matawi makuu manne. Matawi hayo ni
- Hadithi: Ni masimulizi marefu yanayohusisha visa mbalimbali vinavyofanywa na wahusika.
- Ushairi: Ni kazi ya kifasihi inayojumuisha mapigo ya ala ya kimuziki.
- Maigizo: Ni kazi za kifasihi simulizi zinazoambatana na utendaji wa vitendo mbele ya hadhira.
- Semi: Ni vifungu vifupi vifupi vya maneno vinavyotumia lugha ya picha au tamathali za semi. Mfano: mafumbo, nahau, methali na kadhalika.
Sifa Za Fasihi Simulizi
- Kuzaliwa: Hiki ni chanzo cha fasihi simulizi. Mfano: mambo yanayotendeka katika jamii.
- Kukua: Hii ni namna ya kupokea mabadiliko katika jamii, kama vile ya kisiasa na kiuchumi.
- Kufa: Huu ni utelekezwaji wa kazi za fasihi simulizi. Mfano: majigambo, utambaji wa hadithi na kadhalika.
Vipera Vya Tanzu Za Fasihi Simulizi
Vipera ni vikundi vidogo vidogo vya tanzu au matawi ya fasihi simulizi. Tanzu hizo ni hadithi, ushairi, maigizo na semi.
Vipera vya hadithi
- Tarihi: Ni hadithi zinazosimulia kuhusu matukio ya kihistoria. Matukio hayo yanaweza kuwa ya kweli au ya kubuni.
- Soga: Ni hadithi fupi fupi zenye ucheshi. Husimuliwa kwa nia ya kejeli.
- Ngano: Ni hadithi zinazosimuliwa ili kuwaasa watu, hata vijana, kuhusu maisha na maadili ya jamii fulani.
- Visasili: Ni hadithi zinazotumika kuelezea asili ya kitu, vitu au mambo mbalimbali. Mfano: asili ya mlima Kilimanjaro, na kwa nini sungura ana mkia mfupi.
- Vigano: Ni hadithi fupi zinazoelezea uovu wa watu kwa lengo la kuwaadilisha. Mara nyingi hutumia nahau, misemo na methali katika usimulizi wake.
Vipera vya ushairi
- Mashairi: Ni tungo zenye mpangilio maalumu wa silabi, uteuzi mahususi wa maneno, na lugha ya mkato.
Kuna mashairi ya kimapokeo. Haya hufuata na kuzingatia kanuni ya urari wa vina na mizani.
Kuna pia mashairi huru. Haya hayafuati urari wa vina na mizani.
- Nyimbo: Ni tungo za ushairi zenye mpangilio maalumu wa maneno. Hutumia mahadhi, yaani kupanda na kushuka kwa sauti, melodia, mapigo na muwala.
- Tenzi: Ni tungo zenye mpangilio wa silabi zinazolingana kila mstari.
- Maghani: Ni ushairi unaoghaniwa. Yaani, hutolewa kwa kutamkwa badala ya kuimbwa.
- Ngonjera: Ni tungo zenye muundo wa mashairi ya kimapokeo. Huwa na muundo wa mazungumzo baina ya watu au makundi mawili kwa majibizano.
Vipera vya semi
- Methali: Ni semi fupi zenye mpangilio maalumu wa maneno. Hueleza kwa muhtasari na kwa mafumbo mawazo mazito yanayotokana na (sentensi ya chanzo imeishia hapa).
- Vitendawili: Ni aina ya maswali yanayotumia sana lugha ya picha ili kuyafanya yawe mafupi. Vitendawili hufikirisha. Huwafanya watu wahusishe hali halisi ya maisha na vitu au matukio mbalimbali katika mazingira yao ya duniani kwa ujumla. Hutumia tashihisi, sitiari, taswira na kadhalika.
- Mafumbo: Ni semi au kauli za maonyo zenye maana iliyofichika. Hutolewa kwa kuficha ili kuwafikirisha walengwa.
- Misemo: Ni mafungu ya maneno yanayotumiwa na jamii kwa namna maalumu ili kutoa maana inayoafiki ukweli fulani. Hueleza maana ya kauli moja kwa moja. Hutumia maneno ya kawaida lakini yenye hoja au maana maalumu.
- Nahau: Ni kauli fupi fupi zinazotumia sana lugha ya picha. Nahau hutumia maneno ya kawaida yenye maana tofauti. Mfano: kavaa miwani (mlevi).
- Mizungu: Ni kauli zinazotumia lugha ya picha na mafumbo ili kuelezea vipengele mbalimbali vya mila na desturi ya jamii fulani. Hutumika kufunza miiko mbalimbali kwa watoto ambao sasa wanaingia katika kundi la watu wazima.
- Utani: Ni kipera cha fasihi simulizi kinachohusisha kufanyiana mzaha au masihara baina ya watu na makundi mbalimbali katika jamii.
Mfano
Babu: "Njoo mke wangu" (kwa mjukuu).
Mjukuu: "Sitaki! Mke wako ni yule bibi."
Vipera vya maigizo
- Michezo ya kuigiza: Huigiza matukio mbalimbali ya maisha ya jamii fulani. Matukio hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Huambatana na ucheshi au huzuni ili kugusa hisia za hadhira.
- Vichekesho: Vinafanana na maigizo, lakini hivi huwa vifupi. Mara nyingi hakuna visa vingi katika kichekesho kimoja. Lengo ni kuburudisha na kufundisha jamii.
- Majigambo: Ni maigizo yanayohusu mambo ya kishujaa ambayo mtu au watu fulani walifanya. Mfano: matukio ya kivita.
- Ngonjera: Ni aina ya maigizo ambayo wahusika wake hutumia lugha ya ushairi. Mara nyingi katika ngonjera pande mbili hujibizana kuhusu jambo fulani. Hatimaye hukubaliana na kuchukua msimamo wa pamoja.
- Miviga: Ni sherehe zinazofanywa na jamii katika vipindi na mazingira mbalimbali. Mfano: unyago, jando, harusi na kadhalika.
- Ngoma: Ni uchezeshaji wa viungo vya mwili kwa mitindo na miondoko maalumu. Huambatana na muziki wa kuimba tu au wa ala katika sherehe fulani.
Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi Simulizi
Uhakiki ni kitendo cha kuichunguza kazi ya fasihi. Lengo ni kubaini namna ilivyo katika maumbo yake yote mawili, yaani fani na maudhui.
Fani
Fani ni nini? Au nini maana ya fani?
Fani ni upekee wa msanii katika kazi ya fasihi. Katika fani, vipengele vinavyochunguzwa ni kama vifuatavyo:
- Muundo: Ni mjengo au umbo la kazi ya fasihi. Au ni mtiririko wa visa na matukio wa kazi ya fasihi.
- Mtindo: Ni mbinu au njia pekee anayotumia msanii fulani kuwasilisha ujumbe.
- Matumizi ya lugha: Hapa kinachoangaliwa ni vipengele vya lugha vilivyotumika pamoja na mpangilio wa maneno.
- Wahusika: Ni washiriki wakuu katika kazi ya fasihi. Wahusika wanaweza kuwa watu, wanyama, vitu na viumbe vingine.
- Muktadha au mandhari: Ni mahali maalumu ambapo matukio ya kazi ya kifasihi hufanyika.
Maudhui
Maudhui ni maana ya kazi ya fasihi. Ni yale mawazo anayoyazungumzia mtunzi katika kazi ya fasihi.
Katika kigezo hiki mhakiki hutathmini kama mambo yafuatayo yamejitokeza katika kazi ya fasihi:
- Dhamira.
- Ujumbe uliomo, na kama unaambatana na hali halisi.
- Migogoro: Ni muhimu kuchunguza aina ya migongano au mivutano, uzito wake, wanaohusika, na kama mivutano hiyo inaakisi maisha halisi.
- Mafunzo: Huchunguza ubora na mafundisho anayoyatoa mtunzi kwa hadhira.
- Falsafa ya mtunzi: Huchunguza msimamo au hekima ya mtunzi kuhusu maisha.
Tathmini ya uhakiki wa kazi za fasihi
Katika kutathmini kazi za fasihi, huchunguzwa mambo yafuatayo
- Ukweli wa mambo yanayoelezwa. Je, jambo lililoelezwa linafanyika katika jamii?
- Uhalisia wa watu, mazingira na matukio katika jamii.
- Umuhimu wa kazi ya fasihi kwa jamii inayohusika.
Maswali
- Kazi ya fasihi simulizi hupimwa kutokana na ubora wake. Eleza ukweli wa kauli hiyo.
- Eleza namna hadhira inavyonufaika na uhakiki wa mhakiki.
- Ngonjera ni maigizo, pia ni mashairi. Unafikiri ni kwa nini?
- Eleza maana ya kauli hii: "Mhakiki ni mwalimu".
- Taja faida mbili za ngoma.
