Kiswahili · Kidato 1

Mada kuu ya kwanza 1…

Dakika 5 za kusoma ·

Yaliyomo

Mada Kuu Ya Kwanza 1: Mawasiliano

Mawasiliano

Mawasiliano ni nini?

Mawasiliano ni kitendo cha kubadilishana habari au taarifa baina ya watu wawili au zaidi.

Mawasiliano hujumuisha lugha ya mazungumzo, maandishi au ishara mbalimbali.

Dhana Ya Lugha

Nini maana ya lugha?

Lugha ni sauti za nasibu zenye kuleta maana. Sauti hizi zimekubaliwa na watu wa jamii fulani kutumika kwa mawasiliano miongoni mwao.

Mfumo wa lugha ni namna lugha ilivyo kimuundo.

Muundo Wa Lugha

Lugha huundwa na vitu vikuu vinne (4)

  • SAUTI: Ni sehemu ndogo kabisa ya neno isiyoweza kugawanyika zaidi. Mfano: b, a, b, a katika neno baba.
  • SILABI: Ni sehemu ya neno inayoundwa na sauti moja au zaidi. Mfano: si, ta, ki katika neno sitaki.
  • NENO: Ni muunganiko wa silabi kuanzia mbili na kuendelea. Mfano: anakula. Neno hili limeundwa na silabi nne, ambazo ni a, na, ku, la.
  • SENTENSI: Ni kifungu cha maneno kinachotoa maana kamili. AU ni neno kuanzia moja na kuendelea yanayotoa maana kamili.

Dhima / Kazi Ya Lugha Katika Mawasiliano Na Jamii Kwa Ujumla

  • Hutumika kupashana habari.
  • Lugha ni utambulisho wa jamii.
  • Lugha hutumika kama nyenzo ya kudhihirisha hisia. Mfano: chuki, hasira, upendo n.k.
  • Lugha ni sehemu ya utamaduni wa watu.
  • Lugha hutumika kuelimisha jamii.
  • Lugha hutumika kutunza amali za jamii.

Lugha Fasaha Na Umuhimu Wake

Ufasaha wa lugha ni utamkaji wa maneno ya lugha kwa usahihi. Pia ni kuyapa maneno hayo maana kamili kwa usahihi.

Umuhimu / faida za kutumia lugha fasaha

  • Hudumisha taratibu za kisarufi za lugha.
  • Huhakikisha kukamilika kwa mawasiliano baina ya watu. Mfano: kuepuka matumizi ya misimu.
  • Hudumisha kaida za lugha kutegemeana na mila na desturi.
  • Huhakikisha uwiano. Mfano: "Mgonjwa wa UKIMWI amekonda", badala ya "Migonjwa ya UKIMWI amekonda".
  • Huifanya lugha iwe ya mvuto na yenye kupendeza.
  • Hukuza hadhi ya lugha.

Madhara ya kutumia lugha isiyo fasaha

  • Kuvunjwa kwa kanuni za sarufi ya lugha.
  • Kukwamisha mawasiliano.
  • Kutozingatiwa kwa maadili.
  • Kudunishwa kwa lugha.

Matamshi Na Lafudhi Ya Kiswahili

Matamshi sahihi ni namna ya kutamka maneno katika hali inayozingatia kanuni zote za kisarufi za maneno hayo.

Neno likitamkwa katika hali isiyo sahihi, husababisha yafuatayo

  • Kutokea kwa maana inayotofautiana na ile iliyokusudiwa. Mfano: "Tafadhali niletee huo mlago", badala ya "Tafadhali niletee huo mlango".
  • Kutokea kwa maneno yasiyoeleweka. Mfano: "Mzee Ali ameshida hapa leo", badala ya "Mzee Ali ameshinda hapa leo".

Mambo Ya Kuzingatia Katika Utoaji Wa Sauti

  • KIIMBO: Ni utaratibu maalumu wa kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti wakati wa utamkaji.

Mfano

  • Mjomba anakuja. (maelezo)
  • Mjomba anakuja? (swali)
  • Mjomba anakuja! (mshangao)
  • MKAZO: Ni nguvu ya ziada inayotumika kutamka silabi mojawapo ya neno kuliko silabi zingine. Matumizi mabaya ya mkazo huweza kubadili maana.

Mfano

  • Songa mbele: maana yake ni elekea mbele.
  • Songambele: maana yake ni jina la mtu au mahali.
  • Barabara: maana yake ni sawasawa.
  • Barabara: maana yake ni njia pana.
  • LAFUDHI: Ni namna ya mtu ya kutamka maneno ambayo humtambulisha mahali anapotokea.

Mfano

  • Wababa banasikia vizuri (Mkongo)
  • Ntoto kankula nkate wote (Mpemba)
  • Walikulaga viazi (Msukuma)
  • UMBO: Umbo la neno hufuata tabia ya lugha husika. Maneno ya Kiswahili yana muundo maalumu na hujengwa kwa silabi. Muundo wa maneno ya Kiswahili huwa wa silabi zenye irabu moja, konsonanti moja na irabu moja.
  • MPANGILIO: Ni kuyapanga maneno kwa utaratibu maalumu ili kuunda sentensi zinazotoa maana.

Mfano

  • Daktari nzuri dawa amenipa. (sentensi hii haitoi maana)
  • Daktari amenipa dawa nzuri. (sentensi hii inatoa maana)
  • MAANA: Ni dhana inayobebwa katika neno au sentensi. Kila sentensi huwa na maana. Maana hufanya mawasiliano yakamilike baina ya msemaji na msikilizaji.

Msikilizaji asipoelewa kilichosemwa, au msomaji asipoelewa kilichoandikwa, mawasiliano hayakamiliki.

Tanzu Za Lugha (Matawi Ya Lugha)

Lugha ina tanzu zifuatazo

  • SARUFI

Utanzu huu wa lugha hujishughulisha na maeneo manne katika lugha. Maeneo hayo ni maumbo, sauti, mpangilio wa maneno katika tungo, na maana ya maneno.

Kutokana na maeneo hayo manne, tunapata pia aina nne za sarufi. Aina hizo ni

  • Sarufi matamshi: Ni aina ya sarufi inayoshughulikia matamshi ya vitamkwa vya lugha. Kanuni za lugha huelekeza namna ya kuvitamka. Vikitamkwa vibaya, huleta maana tofauti au kupoteza maana kabisa. Mabadiliko katika herufi moja huleta mabadiliko kabisa katika neno.

Mfano: toza na tosa; piga na pita.

  • Sarufi maumbo: Ni aina ya sarufi inayojihusisha na jinsi maneno yanavyoundwa na kazi yake katika sentensi. Vitamkwa vikipangwa katika mpangilio usio wa lugha husika, maana hubadilika au hupotea kabisa.

Mfano: chai ikibadilishwa na kuwa chia, maana hupotea.

  • Sarufi muundo: Ni aina ya sarufi inayozingatia mpangilio na mfuatano wa maneno katika sentensi.

Mfano: "Uchumi wetu umeanza kuimarika", na siyo "kuimarika uchumi wetu umeanza".

  • Sarufi maana: Ni aina ya sarufi inayotawala maana katika sentensi au matini. Sehemu hii isipozingatiwa, inaweza kuzuia mawasiliano au pengine kuibua utata katika mazungumzo.

Mfano: "Mtoto amelalia uji." Tungo hii ina maana zifuatazo

  • Mtoto amelala juu ya uji, au
  • Mtoto amekunywa uji kisha akalala.

Kazi Au Dhima Za Sarufi

  • Huweka utaratibu ambao wanaoitumia lugha wanaufuata.
  • Huwaongoza wanaotumia lugha ili waweze kuelewana.
  • Huipa lugha mfumo maalumu unaoitambulisha na kuitofautisha na lugha nyingine.
  • Hudumisha mfumo wa lugha.

Maswali

  1. Lugha yako ina umuhimu gani kwa jamii yako?
  1. Taja njia za mawasiliano unazozifahamu.
  1. Unafikiri ni kwa nini lugha ni kitambulisho cha jamii?
  1. Unadhani ni jambo gani linaloweza kudunisha lugha yako?
  1. Ufasaha wa lugha hutegemea nini? Taja mambo muhimu matatu.
  1. Eleza kwa kutumia sentensi mbili tu umuhimu wa tanzu za fasihi katika ukuzaji wa lugha.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 45