Kiswahili · Kidato 1

Mada kuu ya saba

Dakika 2 za kusoma ·

Yaliyomo

Uandishi Wa Barua

Maana Ya Barua:

Barua ni karatasi yenye ujumbe ulio katika maandishi.

Uandishi wa barua ni kitendo cha kuandika barua.

Barua Za Kirafiki Au Kindugu

Hizi ni barua ambazo watu huandikiana kwa lengo la kufikishiana ujumbe usio rasmi.

Mifano ya ujumbe huo ni

  • kujuliana hali
  • kupashana habari
  • kuomba
  • kushukuru
  • na mengineyo

Taratibu Au Muundo Wa Barua Za Kirafiki

  • Anwani ya mwandishi: Huandikwa juu upande wa kulia. Huwa katika umbo la mshazari.
  • Tarehe ya kuandikwa barua.
  • Mwanzo wa barua (maamkizi): Huwa upande wa kushoto wa barua, chini kidogo ya tarehe. Mfano: Mpendwa baba, Ndugu mpendwa, nk.
  • Kiini cha barua: Huanza kwa aya fupi ya utangulizi ambapo hutolewa salamu. Mfano: Habari za siku nyingi. Kisha hufuatwa na kiini au maelezo, ambayo hupangwa katika aya.
  • Mwisho wa barua: Ni sehemu ya maagano. Katika maagano maneno ya kiungwana hutumika. Mfano: Wasalaam, Wako akupendaye, Kwa heri, Wako wa moyoni, nk.
  • Jina la mwandishi: Huandikwa mwisho wa barua, baada ya maagano.

Mambo Mengine Muhimu Ya Kuzingatia

  • Matumizi ya lugha inayoeleweka.
  • Kutoa maelezo katika mtiririko mzuri.
  • Kuzingatia alama za uandishi.

Mfano Wa Barua

SHULE YA MSINGI AJE,

S.L.P 65,

KIGOMA,

12-01-1992.

Kwako dada,

Habari ya huko, natumai unaendelea vizuri wewe pamoja na watoto wako. Mimi ni mzima wa afya njema kabisa.

Lengo la kuandika barua hii ni kutaka kukutaarifu kuwa nimechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Twende pamoja. Nategemea kuanza masomo yangu mapema mwezi ujao. Nitakuja kukusalimia nikipata likizo.

Wako mdogo wako mpenzi,

Pondamali Kufa kwaja.

Uandishi Wa Anwani Juu Ya Bahasha

Uandishi wa anwani juu ya bahasha ndiyo unaowezesha barua kumfikia anayehusika.

  • Bahasha kwa mbele: Iandikwe anwani ya anayetumiwa. Mfano:

Kwa,

Safari Masoud,

Shule ya msingi Aje,

S.L.P 65,

Kigoma, Tanzania.

  • Bahasha kwa nyuma: Iandikwe anwani ya aliyetuma. Mfano:

Kutoka kwa,

Leila Ali,

Shule ya msingi Mtakuja,

S.L.P 98,

Mwanza.

Kutuma Barua

Zipo njia mbalimbali za kutuma barua. Baadhi ya njia hizo ni kwa mkono au kwa posta.

Hatua Za Kutuma Barua Kwa Njia Ya Posta:

  1. Baada ya kuandika barua yako, ikunje vizuri. Iweke katika bahasha, kisha ifunge bahasha hiyo vizuri.
  1. Nenda nayo hadi ofisi ya posta. Kisha nunua stempu inayoendana na gharama kamili ya usafirishaji wa barua hiyo.
  1. Bandika stempu vizuri juu ya bahasha, upande wa juu kulia. Kisha tumbukiza barua katika kisanduku cha kupokelea barua zinazosafirishwa kwa njia ya posta.

Maswali

  1. Kimuundo barua za kirafiki zina sehemu kuu ngapi? Zitaje.
  1. Nini maana ya barua?
  1. Uandishi wa tarehe katika barua husaidia nini?
  1. Taja umuhimu wa mambo haya katika uandishi wa barua:

(a) Anwani ya mwandishi

(b) Bahasha

(c) Shirika la posta

(d) Stempu

Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 45