Kiswahili · Kidato 1

Mada kuu ya pili ( 2 )

Dakika 10 za kusoma ·

Yaliyomo

Aina Za Maneno

Maana ya neno

Neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazobeba maana.

Kuna aina mbalimbali za maneno katika lugha ya Kiswahili. Aina hizo ni hizi

Nomino Au Majina (N)

Nomino ni majina yanayotaja watu, vitu, hali na mahali.

Katika sentensi, nomino huwekwa penye nafasi ya mtendaji, mtendwa au mtendewa.

Nomino huwa katika hali ya umoja au wingi.

Mifano

  • Mtoto amerudi. (Mtoto ni N)
  • Magari yameanguka. (Magari ni N)

Viwakilishi (W)

Viwakilishi ni maneno yanayotumiwa badala ya nomino. Au ni maneno yanayotumiwa kuwakilisha nomino.

Viwakilishi hujitokeza pale ambapo nomino haipo.

Viwakilishi huru ni viwakilishi vinavyoweza kusimama peke yake. Mfano: mimi, wao, huyu na yule.

Viwakilishi tegemezi hujitokeza kama sehemu ya vitenzi. Mfano: wanaenda, chema, nk.

Vivumishi (V)

Vivumishi ni maneno yanayoeleza sifa au kutoa taarifa zaidi kuhusu nomino.

Mfano: wetu, yangu, watatu, mweupe, nk.

Vitenzi (T)

Vitenzi ni maneno yanayotoa taarifa zaidi kuhusu tukio au tendo linalotendwa na mtu au kitu.

Mifano

  • Wakulima hawataki kulima. (hawataki ni T)
  • Sote tutaandika vizuri. (tutaandika ni T)

Vielezi (E)

Vielezi ni maneno au vikundi vya maneno vinavyotoa taarifa zaidi kuhusu vitenzi.

Mifano

  • Alisimama nyuma ya mlango. (nyuma ya mlango ni E)
  • Ukitembea polepole tutakuacha. (polepole ni E)

Viunganishi (U)

Viunganishi ni maneno au kikundi cha maneno kinachounganisha maneno au vifungu vya maneno viwili au zaidi.

Viunganishi huunganisha

  • Neno na neno. Mfano: Utakula wali au ugali? (au ni U)
  • Kikundi kimoja cha maneno na kingine. Mfano: Wazee kwa vijana wamefika. (kwa ni U)
  • Sentensi na sentensi. Mfano: Baba analima na mama anapika. (na ni U)

Aina za viunganishi

  • Viunganishi huru: Hivi ni viunganishi vinavyoweza kusimama peke yake. Mfano: lakini, yaani, ila, ingawa, hatimaye, nk.
  • Viunganishi ambatano au tegemezi: Hivi ni viunganishi vinavyojumuisha maneno mawili au zaidi. Mfano: mbali na, badala ya, licha ya, nk.

Vihisishi (H)

Vihisishi ni maneno yanayoashiria hisia mbalimbali za msemaji au mwandishi.

Vihisishi hubainisha hisia kama vile mshangao, mshtuko, furaha, huzuni, wasiwasi, nk.

Mifano: alaa!, salale!, huree!, loh!, nk.

Vihisishi vinapoandikwa hufuatwa na alama ya mshangao (!).

Vihusishi (I)

Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano baina ya watu au vitu viwili, au zaidi.

Mifano

  • Tulipumzika chini ya mti.
  • Amesimama mbele ya ofisi.

Maneno yaliyokolezwa wino ndiyo vihusishi. (Hapa ni "chini ya" na "mbele ya".)

Aina Za Nomino

  • Nomino za pekee: Haya ni majina maalumu yanayotaja vitu au watu wenye maumbile au sifa za pekee. Majina haya huandikwa kwa herufi kubwa. Mifano: majina ya watu kama Asha, Joni, Halima; majina ya siku kama Ijumaa, Alhamisi; majina ya mahali kama Dodoma, Tanga, Arusha, nk.
  • Nomino za kawaida: Haya ni majina ya jumla ya vitu vya kawaida vyenye umbile moja. Mifano: wanyama, watu, mimea na wadudu. Mifano mingine: mvulana, twiga, mchicha na matunda. Kwa kawaida maneno haya huandikwa kwa herufi ndogo, isipokuwa yanapokuwa mwanzoni mwa sentensi.
  • Nomino za jamii: Ni majina yanayojumuisha kutaja vitu au watu katika makundi. Mifano: jeshi, baraza, genge, matunda na kikosi.
  • Nomino dhahania: Ni maneno yanayotaja vitu, tabia au matendo ya kufikirika tu. Yaani ni majina ya hali, dhana au mambo ambayo hujenga picha akilini mwa watu, lakini haiwezekani kuyaona wala kuyagusa. Mifano: njaa, upepo, jinni, uvivu, nk.

Aina Za Viwakilishi

Viwakilishi nafsi huru

Hivi hutumika katika ngeli ya kwanza (Yu – a – wa). Hupatikana katika umoja na wingi kutegemea nafsi inayohusika.

Jedwali la nafsi

  • Nafsi ya kwanza: umoja mimi, wingi sisi
  • Nafsi ya pili: umoja wewe, wingi nyinyi
  • Nafsi ya tatu: umoja yeye, wingi wao

Mifano katika sentensi

  • Mimi nitakuja. – Sisi tutakuja.
  • Wewe utaanza. – Nyinyi mtaanza.
  • Yeye anaenda. – Wao wanaenda.

Viwakilishi nafsi tegemezi

Hivi pia hutumika katika ngeli (Yu – a – wa) na huambatishwa katika kitenzi. Huonyesha nafsi mbalimbali katika umoja na wingi.

Jedwali la nafsi

  • Nafsi ya kwanza: umoja ni-, wingi tu-
  • Nafsi ya pili: umoja u-, wingi m-
  • Nafsi ya tatu: umoja a-, wingi wa-

Mifano katika sentensi

  • Nitacheza. – Tutacheza.
  • Uelezee. – Muelezee.
  • Alicheka. – Walicheka.

Viwakilishi vya kuonyesha

Ni aina ya viwakilishi vinavyosimamia nomino kwa njia ya kuashiria.

Mifano: yule, hicho, hayo, huyo, kule, nk.

Viwakilishi viambata vya ngeli

Ni viwakilishi vinavyowakilisha ngeli mbalimbali za nomino. Pia hutambulisha ngeli ya nomino husika.

Vilevile huambatishwa katika shina la kitenzi kuonyesha umoja au wingi wa nomino inayohusika.

Mifano

  • Ngeli a – wa: mkulima – wakulima. Katika sentensi: analima – wanalima.
  • Ngeli u – i: mti – miti. Katika sentensi: umezaa – imezaa.

Aina Za Vivumishi

  • Vivumishi vimilikishi: Ni maneno yanayoonyesha kuwa kitu ni mali ya nani. Mifano: yangu, change, wenu, yao, yetu, nk.
  • Vivumishi vya sifa: Ni maneno yanayoeleza sifa fulani za kitu au mtu. Mifano: mvivu, mweupe, mrefu, kichafu, nk.
  • Vivumishi vya idadi: Ni maneno yanayoonyesha idadi ya vitu au watu. Mifano: mmoja, wengi, maelfu, nk.
  • Vivumishi vionyeshi: Huonyesha ujirani au umbali wa kitu au mtu. Mifano: yule, kule, kile, pale, nk.
  • Vivumishi viulizi: Ni maneno yanayouliza maswali ili kujua idadi na uhakika wa kitu au mtu. Mifano: ipi?, zipi?, wapi?, ngapi?, upi?, nk.
  • Vivumishi vya jina kwa jina: Hizi ni nomino zinazotoa taarifa zaidi kuhusu nomino nyingine. Mifano:
  • Mtu mlemavu amekuja.
  • Bata mzinga anatembea.
  • Bata maji amekufa.
  • Vivumishi vya pekee: Ni maneno yanayoonyesha ziada ya jambo linalotajwa. Mifano:
  • Mtoto mwenyewe ameanguka.
  • Sisi sote tulifuzu.
  • Panda gari lolote.
  • Vivumishi vya a – unganifu: Ni maneno yanayotumika kutofautisha kitu, jambo au mtu na mtu mwingine. Mifano:
  • Kigoda cha mwalimu.
  • Ana kwa ana.
  • Kombe la dunia.

Aina Za Vitenzi

  • Kitenzi kikuu (T): Hiki ni kitenzi kinachoelezea tendo lililofanywa, linalofanywa au litakalofanywa. Mifano: anaimba, atakula, alikimbia, nk.
  • Vitenzi visaidizi (Ts): Vitenzi hivi hutumika pamoja na vitenzi vikuu katika kuelezea taarifa kikamilifu. Mfano:
  • Mtoto alikuwa analia.
  • Vitenzi vishirikishi (ts): Haya ni maneno yanayoonyesha kuwapo kwa hali au tabia kwa mtu au kitu. Mifano:
  • Mwanawe ni mgonjwa.
  • Basi wewe u mchawi.
  • Kuku huyu ni mzuri.
  • Yule si mwaminifu.

Aina Za Vielezi

Vielezi vya namna au jinsi

Haya ni maneno yanayofafanua namna au jinsi tendo lilivyofanyika. Aina hii ya kielezi imegawanyika katika sehemu kuu sita (6).

Vielezi vya namna mfanano

Huonyesha mfanano au mlingano. Mfano

  • Amevaa kijambazi.
  • Anatembea kifahari.

Vielezi vya namna au hali

Huonyesha jinsi au katika hali gani kitendo kilifanywa. Mfano

  • Walikula haraka.
  • Walifika salama.

Vielezi vya namna vikariri

Hivi huonyesha kujirudiarudia kwa neno kama lilivyo.

Vielezi hivi huleta dhana ya tendo kutofanyika kwa nguvu. Pia huleta dhana ya kufanya kwa kadiri tu na kurudiwarudiwa baada ya muda kidogo. Mfano:

  • Mtoto anapenda kulialia usiku.
  • Mpishi anapenda kuonjaonja chakula.

Vielezi vya namna halisi

Huonyesha hali, hasa ya utendaji. Mfano

  • Tunawapenda sana.
  • Hanipendi kabisa.

Vielezi vya namna viingizi

Hivi hujibu swali kama vile "vipi?". Kwa kifupi, hueleza namna au jinsi tendo linavyotendeka kwa kuiga sauti ya tendo husika. Mfano:

  • Saa ukutani ilisonga ta,ta,ta.
  • Alianguka chini tii.

Vielezi vya namna vya ala

Hivi husaidia kujibu maswali haya: Kitendo kilitendwa kwa kutumia nini? Ni kitu gani kilichotumiwa kutendea jambo? Mfano:

  • Nilisafiri kwa basi.
  • Nilikula kwa kijiko.

Vielezi vya wakati

Hivi hujibu swali: kitendo kitatendeka lini, kilitendwa lini, au kitatendwa lini? Mfano

  • Tutaenda kwao kesho asubuhi.
  • Alimaliza mwaka jana.

Vielezi vya idadi

Vielezi hivi huonyesha kuwa kitendo kilichotajwa kilifanywa au kitafanywa mara ngapi. Mfano:

  • Tunaanza awamu ya pili.
  • Wameniibia tena.

Vielezi vya mahali

Huonyesha mahali tendo lilipofanyika au litakapofanyika. Mfano

  • Alikuja kwetu leo.
  • Ameenda kazini.

Aina Za Viunganishi

Viunganishi huru

Ni maneno au viunganishi vinavyoweza kusimama peke yake. Mfano: iwapo, lakini, ila, labda, ingawa, kwamba, isipokuwa, n.k.

Viunganishi tegemezi

Ni viunganishi ambavyo haviwezi kusimama peke yake. Hutokea kama viambishi katika vitenzi. Mfano:

  • Alivyojishaua nikamuacha.
  • Nilioupiga umesikika.

Aina Za Vihisishi

Vihisishi vya huzuni

Huonyesha huzuni. Mfano: looh!, masikini!, la haula!

Vihisishi vya furaha

Mfano: oyee!, huree!, wee wee!, alo alo!, n.k.

Vihisishi vya mshtuko

Mfano: ka!, hee!, aah!, n.k.

Aina Za Vihusishi

Vihusishi vya mahali

Hivi ni vihusishi vinavyoonyesha mahali. Mfano: kando ya, karibu na, juu ya, chini ya, n.k.

Vihusishi vya wakati

Huonyesha muda. Mfano: baada ya, hadi, mpaka, tangu, n.k.

Vihusishi vya sababu

Hutumika kuonyesha usababishi. Mfano: kwa sababu, kwa ajili ya, kwa minajili ya, n.k.

Vihusishi vya a

Hutumika kulinganisha ngeli za nomino. Mfano: la, ya, cha, wa, n.k.

Matumizi Ya Aina Za Maneno Katika Tungo

Aina zote za maneno hutumika katika tungo kutegemea lengo la msemaji.

Kwa mfano, msemaji akitaka kutoa taarifa kuhusu namna nomino ilivyo, atalazimika kutumia kivumishi.

Akieleza namna nomino hiyohiyo inavyotenda, inavyotendwa au inavyotendewa, atatumia kitenzi.

Vilevile, akitaka kuonyesha namna fulani ya hisia, atatumia vihisishi. Mfano

  • Maji ni uhai. (nomino)
  • Maji meupe. (kivumishi)
  • Maji yanamwagika. (kitenzi)

Matumizi Ya Kamusi

Maana ya kamusi (kamusi ni nini?)

Ni kitabu chenye orodha ya maneno yaliyotafsiriwa maana zake. Maneno hayo yameonyeshwa aina zake, yanavyotamkwa na asili ya kila neno.

Vilevile picha hutumika katika kamusi kama kielelezo cha kubainisha maana ya neno husika.

Dhima au kazi ya picha na michoro katika kamusi

  • Huvuta umakini wa mtumiaji na kumfanya azingatie anachotazama.
  • Huwawezesha watumiaji wa kamusi kuunda dhana ya jambo, hasa kama ni geni.
  • Huwasaidia watumiaji wa kamusi kutofautisha vitu vinavyokaribiana kimaana au kimaumbile.
  • Huwawezesha watumiaji wa kamusi kuona mfanano baina ya vitu.
  • Maumbo au picha hunata katika kumbukumbu za watumiaji kwa haraka.
  • Uhitilifiano huifanya kamusi ivutie, hasa zinapotumia rangi.

Mpangilio wa maneno katika kamusi

Maneno katika kamusi huweza kuorodheshwa kwa namna nyingi. Utaratibu unaotumiwa sana ni ule unaozingatia mpango wa alfabeti.

Maneno yenye kategoria zaidi ya moja yanaweza kuingizwa katika makundi mawili au zaidi. Huweza kutumiwa kama nomino au kitenzi.

Mfano ni neno chupa. Katika kamusi, neno kama hili huorodheshwa kwanza kama nomino, halafu pili kama kitenzi.

Neno lenye kategoria moja linapokuwa na maana kuu mbili au zaidi, litaingizwa kila moja kama kidahizo kamili mara mbili au zaidi.

Mpangilio wa maneno hayo utaanza na maana kuu, halafu maana ndogondogo.

Maneno yenye kategoria tofauti au maana zaidi ya moja hutofautishwa kwa namba za kipeo. Mfano: Chupa1, Chupa2, Chupa3.

Faida ya maneno kupangwa kwa alfabeti

  • Humrahisishia mtumiaji wa kamusi kupata neno analolitafuta kwa urahisi zaidi.
  • Humwezesha mtumiaji kubaini kwa haraka maana anayotafuta.

Dhima au kazi ya fasihi katika jamii

  • Kuhifadhi na kueleza maana ya misamiati.
  • Kuwa chanzo cha tahajia.

Vidahizo Na Vitomeo

Vidahizo

Ni maneno yaliyoorodheshwa katika kamusi na kuandikwa kwa chapa iliyokoza (bold). Hupangwa kialfabeti kuanzia herufi A hadi Z.

Vitomeo

Ni neno au maneno au kidahizo pamoja na taarifa zake zote anazozihitaji mtumiaji wa kamusi.

Taarifa hizo ni kama vile

  • aina ya maneno
  • wingi wa neno
  • fasili ya kidahizo
  • mfanano wa matumizi
  • muktadha wa matumizi
  • matumizi katika methali, misemo na nahau
  • mnyumbuliko, hasa wa vitenzi

Mbinu za kusoma kamusi

  1. Angalia neno limeanza na herufi gani katika umoja.
  2. Kwa maneno yenye viambishi, kwanza livunje neno hilo katika sehemu zake mbili, yaani kiambishi na shina. Kisha angalia shina la neno linaanzia na herufi gani.
  3. Pekua kamusi huku ukiangalia kwa makini ni katika ukurasa gani yalipo maneno yanayoanzia na alfabeti hiyo.

Maswali

  1. Ainisha maneno yafuatayo:

(a) jeshi

(b) salama

(c) karibu na

(d) vyangu

(e) eh!

  1. Tunga sentensi mbili kwa kutumia miundo hii:

(a) wingi

(b) lakini

  1. Nomino na vielezi vinatofautianaje?
  1. Taja mifano miwili ya aina za vihusishi ambazo unazifahamu.
  1. Kamusi ni nini? Kamusi zina umuhimu gani katika ukuzaji wa lugha?
  1. Ipo tofauti gani kati ya nomino na viwakilishi?
  1. Tofautisha vitenzi na vivumishi.
  1. Katika sentensi hii "watoto wote wamekimbia", likiondolewa neno "watoto", neno "wote" litakuwa aina gani ya neno?
  1. Taja aina za vivumishi zinazojitokeza katika sentensi hizi.

(a) Mtoto wao amekuja.

(b) Kitabu hiki nimekipenda.

(c) Umefika lini?

Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 45