Kiswahili · Kidato 2

Utunzi wa kazi za fasihi simulizi

Dakika 3 za kusoma ·

Yaliyomo

Utunzi Wa Kazi Za Fasihi Simulizi

Kwa kawaida, utunzi wa kazi za fasihi hutegemea nguzo kuu mbili. Nguzo hizo ni fani na maudhui.

Utunzi Wa Mashairi

Kanuni za utunzi wa mashairi ya kimapokeo

  1. Kutafuta maudhui na kuweka dhamira.

Hatua hii inajumuisha mambo yafuatayo

  • a) Mtunzi awe na jambo muhimu linalohusu jamii.
  • b) Mtunzi anatakiwa afahamu msimamo wa wanaotungiwa au hadhira, ili asiibue hisia kali.
  • c) Kuweka lengo kuu la shairi. Mfano: kupinga ubaguzi.
  • d) Kuteua wazo kuu la shairi.
  • e) Kufanya utafiti na kufahamu kwa kina mambo ya kutungia shairi.
  • f) Kupanga mawazo yanayojenga maudhui kwa mantiki, kutegemea uzito, upya, ugumu na kadhalika.
  1. Kufanya uamuzi kuhusu fani.

Mambo ya kuzingatia katika fani ni haya

  • a) Kuteua mtindo wa shairi (huru au arudhi).
  • b) Kuamua muundo wa shairi (tarbia, tathilisa, takhmisa na kadhalika).
  • c) Idadi ya mizani. Mfano: mizani 12 kila mstari.
  • d) Aina ya vina. Mfano: vina vya kati au vya mwisho.
  • e) Vipande. Mistari ya ushairi inaweza kuwa na vipande katika kila mstari.
  • f) Kibwagizo. Ni mstari wa mwisho katika kila ubeti.
  1. Matumizi ya lugha.

Ushairi una lugha tofauti na kazi nyingine za kifasihi. Mtunzi hana budi kutumia lugha yenye sifa zifuatazo:

  • a) Maneno ya mkato. Mfano:

Lilala ni nililala.

Siombe ni usiombe.

  • b) Mpangilio wa maneno usio wa kawaida. Mfano: "Hufika navyo viroba, wachinjaji" ni "Hao wachinjaji hufika na viroba."
  • c) Uteuzi wa maneno kama ni ya kikale au ya kisasa. Mfano: gesi na kuka.
  • d) Matumizi ya lugha ya picha au taswira.
  1. Aina na idadi ya wahusika. Mfano: binadamu, wanyama, miti na kadhalika.
  1. Maana ya shairi. Ni vizuri kuficha maana ya shairi ili isiwe wazi kwa kila mtu kubaini.
  1. Anwani. Kila shairi liwe na kichwa muafaka.
  1. Vituo. Ni muhimu mtunzi azingatie utaratibu wa kuandika kwa kutumia alama mbalimbali ipasavyo.

Utunzi Wa Maigizo

Kanuni za utunzi wa maigizo

  • Kuchagua tukio la kuigiza. Mfano: madhara ya UKIMWI.
  • Kuchagua muktadha au mahali pa kutendeka kwa jambo. Mfano: shuleni.
  • Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa. Mfano: mtindo wa fumbo au vichekesho.
  • Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo. Mfano: migogoro na suluhisho.
  • Kuweka mpangilio wa maonyesho.
  • Kubuni wahusika na kuweka aina na idadi yao kwa kutegemea matukio.
  • Kuumba wahusika na kuamua mavazi yatakayotumika na vifaa vingine.
  • Kuamua urefu wa igizo.
  • Kutunga maelezo kuhusu mandhari.
  • Kuandika maigizo na kuhariri.

Utunzi Wa Ngonjera

Kanuni za kutunga ngonjera

  • Kuteua mada. Mfano: kilimo.
  • Kuweka dhamira.
  • Kuteua maudhui.
  • Kutumia mtindo wa mashairi ya kimapokeo.
  • Kutumia muundo wa mashairi wenye mizani, vina, vipande na mishororo.
  • Kuteua mandhari kutokana na mada.
  • Kuwa na wahusika wawili au zaidi, au vikundi viwili au zaidi.

Maswali

  1. Kwa kawaida utunzi katika fasihi hutegemea nguzo kuu mbili. Zitaje.
  1. Eleza kwa muhtasari kanuni za kutunga mashairi.
  1. Ngonjera ni nini?
  1. Eleza maana ya methali huku ukitoa mifano mitatu ya methali.
  1. Tunga vitendawili vitatu na maana zake.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 39