Matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali
Dakika 5 za kusoma ·
Yaliyomo
Matumizi Ya Lugha Katika Miktadha Mbalimbali
Maana Ya Utumizi Wa Lugha
Utumizi wa lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha fulani huitumia lugha. Wanazingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika.
Dhima Au Kazi Ya Utumizi Wa Lugha
- Hutumika kupashana habari, ujuzi na maarifa.
- Kujenga mahusiano mazuri baina ya watu.
- Kuepusha migongano baina ya watu.
Misingi Ya Utumizi Wa Lugha
Kuna misingi mbalimbali ya kusimamia katika utumizi wa lugha. Ni hii
- Mada inayozungumzwa. Mfano: mada inayohusu mambo ya elimu, umasikini, ajali, vifo, mpira na kadhalika.
- Muktadha au mahali ambapo mazungumzo yanafanyika. Mfano: shuleni, msikitini, vijijini, barabarani, sokoni, uwanjani na kadhalika.
- Malengo ya mazungumzo. Mfano: kuelimisha, kutoa taarifa, kutia moyo, kukejeli, kufurahisha na kadhalika.
- Uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji. Mfano: baina ya wanafunzi kwa wanafunzi, wazee, walimu, madaktari, wasichana, wavulana na kadhalika.
Rejesta, Misimu Na Utata
Rejesta:
Rejesta ni mtindo wa lugha ambao maneno na miundo yake ni kwa ajili ya kukidhi haja ya mawasiliano katika muktadha fulani. Mfano: hospitalini, shuleni, kijiweni, hotelini na kadhalika.
Aina za rejesta
Kuna aina nyingi za rejesta. Kwa mfano
- Rejesta za shuleni
- Rejesta za hospitalini
- Rejesta za kijiweni
- Rejesta za msikitini
- Rejesta za kanisani
- Rejesta za dukani
- Rejesta za mpirani
- Rejesta za siasa
- na nyinginezo.
Dhima au kazi za rejesta
- Kukidhi mawasiliano ya uwanja fulani maalumu.
- Kutambulisha wazungumzaji kuwa wao ni wa kundi fulani. Mfano: vijana.
- Kuficha ujumbe kwa watu wasiohusika.
- Kuokoa muda. Mfano: 2×3 (hospitalini), chai moja (hotelini) na kadhalika.
- Hukuza lugha.
Misimu:
Misimu ni maneno ya lugha ya kawaida ambayo si sanifu. Huzushwa na wazungumzaji wa lugha fulani kwa ajili ya kukidhi haja ya mawasiliano.
Sifa kuu ya misimu ni kuzuka na kupotea katika jamii.
Mfano wa misimu katika lugha ya Kiswahili: amefulia, noma, soo, wowowo, chakachua, denti, wakusoma, chabo na kadhalika.
Misimu ikitumika sana na kuzoeleka husanifishwa na kuwa msamiati rasmi. Mfano: neno Mshikaji.
Chanzo cha misimu
Misimu inatokana na mabadiliko na matukio ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yanayotokea katika jamii.
Miktadha ya misimu
Mara nyingi misimu hutumika katika mazingira yasiyo rasmi. Mfano: mitaani.
Misimu inaweza kutumika eneo finyu au pana zaidi. Mfano: darasani, shuleni, kijijini, kata, tarafa, wilaya, mkoa, taifa na hata katika kanda nzima.
Misimu huenezwa na wasafiri, redio, wafanyabiashara, televisheni na magazeti.
Utata:
Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Mfano: mbuzi, paa, ndege na kadhalika.
Sababu za utata wa maneno
- Neno kuwa na maana zaidi ya moja. Mfano:
Mbuzi: mnyama.
Mbuzi: kifaa cha kukunia nazi.
- Kutozingatia taratibu za uandishi. Mfano:
"Tulimkuta Juma na rafiki yake, Meshaki."
"Tulimkuta Juma na rafiki yake Meshaki."
- Kutumia maneno bila kuzingatia mazingira au muktadha unaohusika wa matumizi ya maneno.
- Utamkaji wa maneno. Mfano:
Ana uma
Mimina wewe
- Mjengo wa maneno. Mfano:
Anampigia mgeni (kwa ajili ya ..)
Anampigia ngoma (kifaa au chombo)
Anampigia chumbani (mahali)
Lugha Ya Mazungumzo Na Lugha Ya Kimaandishi
Lugha ya kimazungumzo
Lugha ya kimazungumzo hutolewa kwa njia ya mdomo. Mazungumzo yanapotolewa kunakuwa na mzungumzaji na msikilizaji.
Mazungumzo yanaweza kutolewa kwa njia ya ana kwa ana au vinginevyo.
Faida ya lugha ya mazungumzo
- Kuimarisha uhusiano.
- Kutumika kwa ishara za mwili katika kusisitiza jambo.
- Huruhusu kuuliza au kuulizwa swali.
- Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake. Mfano: kulia, kupaza sauti, kusikitika na kadhalika.
- Mzungumzaji anaweza kufuta makosa yake, kuongeza jambo au kufafanua zaidi.
Matatizo au hasara za lugha ya mazungumzo
- Kupotea kwa baadhi ya taarifa. Mfano: mzungumzaji akisahau.
- Mzungumzaji huweza kuichosha hadhira kwa kurudia rudia baadhi ya vipengele.
- Ujumbe unaweza kutoeleweka kama utatolewa mahali penye kelele.
Lugha ya kimaandishi
Lugha ya kimaandishi ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Maandishi hayo yanaweza kuandikwa kwa mkono au kompyuta.
Lugha ya maandishi huambatana na taratibu za uandishi. Mfano: vituo, aya, herufi kubwa na kadhalika.
Faida au ubora wa lugha ya maandishi
- Huwezesha watu walio mbali kuwasiliana.
- Hustawisha sarufi ya lugha na misingi yake.
- Hufuata taratibu zote za lugha.
Matatizo au hasara za lugha ya maandishi
- Hutumiwa tu na wanaojua kusoma na kuandika.
- Haina msisimko wa lugha kama ule uletwao na lugha ya mazungumzo.
- Hukosa vidokezo vingi ambavyo hutolewa na lugha ya mazungumzo.
- Inamnyima mwandishi nafasi ya kupima uelewa wa msomaji kwa kuwa hamuoni.
Dhima ya lugha ya kimazungumzo na lugha ya kimaandishi
- Huwezesha watu kuwasiliana.
- Kuhifadhi kumbukumbu kwa muda mrefu.
Tofauti baina ya lugha ya maandishi na lugha ya mazungumzo
- Lugha ya mazungumzo huwezesha mawasiliano ya ana kwa ana, lakini lugha ya maandishi haiwezeshi mawasiliano ya ana kwa ana.
- Lugha ya mazungumzo haihitaji maandalizi, lakini lugha ya maandishi huhitaji maandalizi.
- Lugha ya mazungumzo hailazimiki kufuata kanuni za kisarufi, lakini lugha ya maandishi hutakiwa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Matumizi Ya Lugha Ya Kimazungumzo Na Kimaandishi Katika Miktadha Mbalimbali
Utumiaji wa lugha zote mbili huongozwa na mambo yafuatayo
- Mada inayozungumzwa.
- Muktadha au mahali pa mazungumzo.
- Malengo ya mazungumzo hayo.
- Uhusiano uliopo kati ya wazungumzaji.
Kutumia Lafudhi Na Matamshi Sahihi Katika Mawasiliano
Ni jambo la msingi kutumia lafudhi sahihi. Pia ni muhimu kutamka kila neno kwa usahihi unapozungumza na mtu.
Makosa ya matamshi na lafudhi husababishwa na mambo mawili
- Athari za lugha mama.
- Dosari katika viungo vya utamkaji.
Athari za lugha mama
Mfano
- "Fiatu fyangu": Mnyakyusa.
- "Rara bira kura": Mkurya.
Dosari za ala za utamkaji
Ala za utamkaji ni mdomo, ulimi, kaakaa gumu na laini, pua, koo na meno.
Ala mojawapo kati ya hizi ikiwa na kasoro, huathiri utamkaji wa maneno. Mfano: sisi inakuwa thithi (tatizo la meno).
Maswali
- Taja mambo makuu manne yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa mazungumzo.
- Kuna utofauti gani kati ya lugha ya baba na mtoto na ile lugha inayotumiwa na watu wa rika moja?
- Eleza maana, aina na dhima tatu za rejesta.
- Kwa kutumia lugha mwafaka, fanya maigizo kama vile uko:
(a) Gulioni
(b) Darasani
(c) Kijiweni
(d) Mahakamani
- Kuna utofauti gani baina ya lugha ya mazungumzo na lugha ya kimaandishi?
- Taja misimu mitano unayoifahamu.
- Eleza maana ya lafudhi huku ukitoa mifano kadhaa ya lafudhi unayoielewa.
- Tungo zifuatazo ni tata. Eleza maana mbili kwa kila tungo:
(a) Mtoto amelalia uji
(b) Kaka amepata jiko
(c) Amenunua mbuzi.
