Uandishi
Dakika 4 za kusoma ·
Yaliyomo
Insha Za Hoja
Insha za hoja ni insha zinazoeleza jambo fulani kwa kujenga hoja. Hoja hizo hutetea msimamo fulani kuhusu jambo linaloelezwa.
Muundo wa insha
- Kichwa cha insha. Huandikwa kwa herufi kubwa.
- Utangulizi. Ni maelezo mafupi yanayodokeza mada.
- Kiini cha insha. Ni sehemu kuu ya insha.
- Mwisho. Ni maelezo ya msisitizo juu ya jambo lililojadiliwa.
Barua Rasmi
Barua rasmi ni barua zinazohusu mambo rasmi ya kiofisi. Mifano ni kutoa taarifa, kuomba kazi, kuagiza vitu na kadhalika.
Muundo au sehemu kuu za barua rasmi
- Anwani ya mwandishi. Huandikwa juu upande wa kulia wa barua au karatasi.
- Tarehe. Huandikwa chini kidogo ya anwani ya mwandishi.
- Namba ya kumbukumbu ya barua. Huandikwa kwa ufupi. Husaidia kurejea barua za zamani zilizohifadhiwa katika majalada.
- Anwani ya mwandikiwa barua. Hukaa upande wa kushoto wa barua, chini kidogo ya namba ya kumbukumbu.
- Mwanzo wa barua. Hukaa upande wa kushoto wa barua, chini kidogo ya anwani ya mwandikiwa.
- Kichwa cha habari au barua. Huandikwa kwa herufi kubwa na kuwekewa mstari chini yake. Hukaa katikati ya barua.
- Utangulizi wa barua. Hukaa chini kidogo ya kichwa cha habari.
- Kiini cha barua. Huonesha madhumuni ya barua.
- Mwisho wa barua. Ni hitimisho la barua. Hutoa maelezo mafupi ya msisitizo juu ya jambo lililowasilishwa.
- Saini ya mwandishi. Huandikwa chini kidogo ya maelezo ya mwisho.
- Jina kamili la mwandishi. Huandikwa chini kidogo ya saini.
- Wadhifa wa mwandishi, kama unahitajika.
Mfano wa barua rasmi
CHAMA CHA WAKULIMA MALINYI,
S.L.P. 9219,
MALINYI, MOROGORO,
12.01.2019.
KIWANDA KIKUU CHA MBOLEA,
S.L.P 354,
DAR ES SALAAM.
Ndugu;
YAH: MAHITAJI YA MZIGO WA MBOLEA.
Husika na kichwa cha barua hapo juu, napenda kukuagiza mzigo wa mbolea kwa mahitaji ya wilaya ya Malinyi kama ifuatavyo;
- Mbolea ya chumvi chumvi mifuko 200.
- Mbolea ya CAN mifuko 150.
- Mbolea ya DAP mifuko 100.
Nitafurahi iwapo nitapokea mzigo huo ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya maombi.
Saini…………………
Lwanda Magere
Mwenyekiti.
Simu Za Maandishi Au Telegramu
Simu za maandishi au telegramu ni aina ya barua fupi. Husafirishwa kwa haraka sana kuliko barua za kawaida.
Simu hizi huandikwa kwenye fomu maalumu zinazotolewa kwenye shirika la posta.
Simu hizi huandikwa kwa maneno yasiyozidi 10-15.
Mfano
MUSA KINGAMBE SLP 5679 DSM NJOO HARAKA DADA MGONJWA LINGINDO.
Simu Za Mdomo
- Hufikisha ujumbe kwa njia ya mazungumzo.
- Hazitumii muda mrefu kufikisha ujumbe.
- Huduma za simu za mkononi hutolewa mahali popote.
- Ujumbe wa simu za mdomo haupotei, kwa sababu ni mawasiliano ya moja kwa moja na mlengwa.
Tofauti kati ya simu za maandishi na simu za mdomo
- Simu za maandishi hufikisha ujumbe kwa njia ya maandishi. Simu za mdomo hufikisha ujumbe kwa njia ya mdomo.
- Katika simu za maandishi, ujumbe huchukua muda mrefu kufika ulikokusudiwa. Simu za mdomo huchukua muda mfupi kufikisha ujumbe.
- Simu za maandishi huwalenga wanaojua kusoma. Simu za mdomo hazitegemei mtu kujua kusoma.
- Simu za maandishi hutolewa posta tu. Simu za mdomo hazichagui mahali.
Dayalojia
Dayalojia ni mazungumzo na majibizano baina ya watu wawili au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana.
Mambo ya kuzingatia katika utungaji wa dayalojia
- Kutoa maelezo ya ufafanuzi katika mabano ili kumfahamisha msomaji na msikilizaji mambo yanayotendeka.
- Kuwa na mazungumzo ya mkato na yasiyozidiana sana kati ya wahusika.
- Kutumia vihisishi kama loh!, ala!, kweli! na kadhalika, ili kuifanya dayalojia iwe ya kuvutia.
- Pawepo mwingiliano wa mazungumzo ya wahusika na kudakia maneno ili dayalojia iwe na uhalisia.
- Lugha inayotumiwa izingatie sarufi.
Kadi Za Mialiko
Kadi za mialiko ni aina ya karatasi ngumu zinazopeleka taarifa fupi za kumwomba mtu ahudhurie sherehe fulani. Mifano ya sherehe hizo ni harusi, maulidi, ubatizo, mahafali na kadhalika.
Mambo muhimu yanayozingatiwa katika uandishi wa kadi ya mwaliko
- Jina la mwandishi au mualikaji.
- Jina la mwandikiwa au mwalikwa. Ni muhimu kuandika vyeo pia. Mfano: sheikh, prof, mchungaji, dkt na kadhalika.
- Lengo la mwalikaji. Huandikwa kwa ufupi na uwazi.
- Mahali pa kufanyia shughuli.
- Tarehe ya mwaliko.
- Wakati au muda wa shughuli.
- Jina la anwani ya mtu atakayepelekewa majibu.
Mfano wa kadi ya mwaliko
Familia ya Bwana SAIDI MAGANZA
Inapenda kukualika / kuwaalika Prof, Sheikh, Mchungaji, Mwl, Dkt OCHINCHO SANCHO
Kwenye harusi ya mtoto wao FLORA itakayofanyika tarehe 06-12-2018 katika ukumbi wa KIBO kuanzia saa 2 usiku.
Tafadhali fika ukumbini na kadi hii.
Kwa wasiofika watoe taarifa kupitia namba zifuatazo au .
Nyote mnakaribishwa.
Watoto tunawapenda lakini hawaruhusiwi.
Barua Za Mialiko
Barua za mialiko huwa fupi sana, ingawa zinazidi kidogo kadi za mialiko.
Mambo yote yanayoonyeshwa katika kadi za mialiko ndiyo huonyeshwa pia katika barua za mialiko.
Maswali
- Eleza maana ya uandishi.
- Toa maana ya insha za hoja.
- Onesha hatua muhimu za kufuatwa katika uandishi wa insha. (Sifa za insha)
- Barua ni nini?
- Tunapata faida gani tunapotumia barua kama njia ya mawasiliano?
- Nini maana ya barua rasmi?
- Orodhesha sehemu muhimu za barua rasmi.
- Nini tofauti kati ya simu ya mdomo na simu za maandishi?
- Eleza maana ya barua za mialiko.
