Uhakiki wa kazi za fasihi simulizi
Dakika 3 za kusoma ·
Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi Simulizi
- UHAKIKI WA MASHAIRI
Mashairi huhakikiwa kwa kuzingatia vigezo vya maumbo yake mawili. Maumbo hayo ni fani na maudhui.
Fani huchunguza mbinu za kifani alizotumia mtunzi katika ushairi.
Katika maudhui, mhakiki huchunguza mawazo muhimu yanayojitokeza katika shairi linalohusika.
Vipengele vya fani
Uhakiki wa fani za ushairi ni uchambuzi wa kina unaoweka wazi mbinu za kisanaa zilizotumika katika shairi husika.
Vipengele vya fani katika ushairi ni hivi
- Mtindo: Huonesha kama shairi ni la kimapokeo au la kisasa.
- Muundo: Hubainisha mambo yafuatayo:
- Idadi ya beti.
- Idadi ya mistari na aina ya vibwagizo.
- Idadi ya vipande.
- Idadi ya mizani.
- Aina ya mpangilio wa vina.
- Wahusika: Wahusika wanaweza kuwa watu, wanyama, vitu na kadhalika.
- Matumizi ya lugha: Katika kipengele hiki mhakiki huchunguza yafuatayo:
- Mpangilio wa maneno. Mfano: "wengi wari" badala ya "wari wengi".
- Matumizi ya mazida, inkisari na tabdila:
- Mazida: Kurefusha maneno. Mfano: "kiwembe" badala ya "wembe".
- Inkisari: Kufupisha maneno. Mfano: "siombe" badala ya "usiombe".
- Tabdila: Kubadilisha mwendelezo wa neno. Mfano: "kujitanuwa" badala ya "kujitanua".
- Matumizi ya nahau, methali na misemo.
- Matumizi ya lugha ya picha.
- Matumizi ya tamathali za semi. Mfano: takriri, tashihisi, sitiari na kadhalika.
- Mbinu nyingine za kisanaa. Mfano: alama ya mshangao.
Vipengele vya fani husaidia kuwasilisha maudhui.
Vipengele vya maudhui
Uhakiki wa maudhui ya ushairi ni kuchambua na kuweka wazi mawazo makuu na mafunzo yanayopatikana katika shairi.
Ili kuhakiki na kupata maudhui ya shairi, huna budi kulisoma shairi mara mbili au tatu.
Vipengele vya maudhui ni kama ifuatavyo
- Dhamira: Ni wazo kuu au mawazo makuu yanayojitokeza katika shairi.
- Mtazamo: Ni hali ya kuyaona mambo katika maisha kwa kuzingatia matukio fulani katika maisha.
- Msimamo: Ni hatua ya mtunzi kusimamia jambo fulani.
- Falsafa: Ni imani ya mwandishi au msanii.
- Ujumbe na maadili: Ni ujumbe na maadili yanayotolewa na msanii.
- Migogoro: Ni mivutano na misuguano inayojitokeza katika ushairi. Mfano: migogoro ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika.
Maswali yanayoongoza kufanyika kwa uhakiki
- Shairi liliungwa wakati gani?
- Mshairi anatueleza nini?
- Mshairi anamtungia nani?
- Mshairi anatukuza au kubeza nini? Au nani?
- Mshairi anashauri tuchukue hatua gani katika utatuzi wa jambo alilozungumzia?
- UHAKIKI WA MAIGIZO
Vipengele vya fani
- MTINDO: Ni sura ya maigizo inayojitokeza kupitia mpangilio wa maneno na vitendo. Vitu vya kuchunguza katika mtindo ni hivi:
- Mchezo wa jukwaani: Una mpangilio wa maneno na vitendo baina ya watu.
- Majigambo: Yanaonyesha kujisifu kwingi kwa watu.
- Vichekesho: Ni mpangilio mzuri wa maneno unaowasilisha ujumbe kwa kuchekesha.
- Mazungumzo: Ni maongezi ya kujibizana baina ya watu.
- Ngonjera: Ni mpangilio wa tungo za kishairi ambapo watu wawili au makundi mawili hukinzana juu ya jambo fulani.
- Miviga: Ni sherehe za kitamaduni kama vile matambiko.
- MUUNDO: Muundo katika maigizo huhusu vitendo vingi vinavyotokea sehemu tatu:
- Mwanzo: Hubainisha jambo la kuigizwa.
- Mwendelezo: Hujenga kisa au visa vinavyoonesha mgogoro.
- Misho: Mgogoro husuluhishwa.
- MANDHARI: Ni sehemu au mazingira ya kutendea maigizo.
- WAHUSIKA: Je, wamejitokeza kikamilifu? Je, wanaaminika?
- MATUMIZI YA LUGHA: Mfano: semi, picha, methali, nahau na kadhalika.
- MALEBA NA VIFAA: Huakisi muktadha na vifaa vinavyotumika katika maigizo.
- MATUMIZI YA ALA: Mfano: ngoma, baragumu na sauti nyingine.
- MBINU NYINGINE: Mfano: nyimbo, uchezaji ngoma, usimulizi na kadhalika.
Vipengele vya maudhui
Mhakiki huchunguza yafuatayo
- DHAMIRA.
- UJUMBE.
- FALSAFA.
- MAFUNZO NA MAADILI.
- MIGOGORO.
- UHAKIKI WA HADITHI
Hadithi pia huhakikiwa kwa kutumia vipengele vya fani na maudhui. Vipengele hivyo tumekwishaviona katika uhakiki wa maigizo na ushairi.
Maswali
- Taja vipengele vya fani na maudhui katika uhakiki wa hadithi.
- Eleza maana ya wahusika.
- Nini tofauti kati ya fanani na hadhira?
- Eleza faida ya kuhakiki ushairi.
- Nini maana ya dhamira?
