Utungaji wa kazi za fasihi andishi
Dakika 5 za kusoma ·
Yaliyomo
Utungaji Wa Kazi Za Fasihi Andishi
Maana Ya Kazi Za Fasihi Andishi
Kazi za fasihi andishi ni kazi za sanaa ambazo huwasilishwa kwenye jamii kwa njia ya maandishi. Zinaweza kuwa katika vitabu au vijarida.
Msanii wa fasihi andishi ni mtu anayeandika mambo ya kawaida, lakini kwa lugha isiyo ya kawaida.
Kazi za fasihi andishi ndizo zinazodumu kwa muda mrefu. Hii ni kwa sababu huhifadhiwa kwa maandishi kwenye vitabu. Hivyo ni rahisi kuvipata kwenye maktaba mbalimbali.
Hatua Za Kutunga Kazi Ya Sanaa
Ili msanii aweze kutengeneza kazi ya sanaa, ni lazima azingatie mambo yafuatayo
- Kubaini jambo linalogusa jamii
Jamii zetu zimezungukwa na mambo mengi ambayo ni kero. Msanii anaweza kutumia mambo hayo kuiweka jamii sawa. Pia anaweza kutumia mambo yanayotokea kila siku.
Msanii anaweza kuandika kuhusu rushwa, mapenzi, magonjwa, umasikini, uongozi mbaya, unyanyasaji, mmomonyoko wa maadili na kadhalika.
Anaweza kuandika mambo hayo yote katika riwaya, tamthiliya na ushairi.
- Kuchagua umbo la kazi
Mwandishi akishapata wazo la kuandika, anatakiwa kuchagua namna kazi yake itaonekana. Yaani aamue kama kazi yake itakuwa hadithi, tamthiliya, riwaya, shairi au utenzi.
- Kupanga ploti au msuko wa visa
Ni vema msanii apange kazi yake katika hatua kuu kutokana na vipengele vya ploti. Vipengele hivyo ni utangulizi, mgogoro, mgogoro mkuu (kilele) na suluhisho.
- Kubaini hadhira
Mwandishi lazima ajue anaandikia nani. Hilo litamfanya achague lugha mwafaka. Pia litafanya kazi yake iwavutie lika alilolilenga, kwa sababu inaendana nao.
- Kubuni wahusika na mandhari
Mwandishi anatakiwa kubuni wahusika wa kazi yake.
Angalizo: mwandishi asitumie majina ya viongozi walio madarakani. Pia asitumie jina la mhusika wa kweli aliye kwenye jamii. Hii inaweza kumwingiza kwenye matatizo makubwa.
Mwandishi awe mbunifu. Anaweza kubuni wahusika kama wanyama na mazimwi. Pia anaweza kubuni majina ya utani.
- Kuanza kuandika
Hapa mwandishi anaanza kuweka mawazo yake kwenye maandishi. Hii ni kwa sababu si rahisi kwa mtunzi kuhifadhi kichwani kazi yote aliyoibuni.
Utungaji Wa Hadithi
Maana ya hadithi
Hadithi ni masimulizi marefu na ya kubuni yaliyoandikwa kinathari. Ina wahusika, matukio na mandhari.
Kuna aina mbili za hadithi
- Hadithi ndefu (riwaya)
- Hadithi fupi (riwaya fupi)
Pia kuna aina mbili za riwaya
- Riwaya pendwa
- Riwaya dhati
Riwaya dhati
Riwaya dhati ni riwaya zinazozungumzia masuala mazito ya maisha ya kijamii. Masuala hayo yanagusa tabaka tawala. Mifano ni rushwa, wizi, uhujumu uchumi na ukombozi wa mwanamke.
Mifano ya riwaya dhati ni Rosa Mistika (E. Kezilahabi) na Nyota ya Rehema (M.S. Mohamed).
Riwaya pendwa
Riwaya pendwa ni hadithi au riwaya zenye mafunzo mengi. Lengo lake kuu ni kuburudisha.
Usimuliaji wake husisimua akili. Umejaa taharuki na matumizi mengi ya mubalagha. Mazungumzo yake pia yamejazwa sana chumvi.
Riwaya pendwa huzungumzia mambo kama mapenzi, mauaji, ujasusi na upelelezi.
Mifano ni Kikosi cha Kisasi, Hofu, Miwani Meusi, Asali Chungu na Njama.
Mikondo Ya Hadithi
Mkondo wa hadithi ni mwelekeo ambao mtunzi huufuata katika kutunga hadithi yake.
Mikondo ya hadithi ni ifuatayo
- Mkondo wa kipelelezi
Mkondo huu unahusu hadithi zinazozungumzia upelelezi wa mambo kama mauaji, rushwa na wizi.
Mifano ni Simu ya Kifo (F. Katalambula) na Dimbwi la Damu (B. Mtobwa).
- Mkondo wa kihistoria
Mkondo huu unahusu hadithi zilizotokana na matukio fulani ya kihistoria ya jamii, kama vita na njaa.
Mfano ni riwaya ya Zawadi ya Ushindi (B. Mtobwa).
- Mkondo wa kijasusi
Mkondo huu unahusu upelelezi wa ngazi ya kimataifa, au ujasusi unaotishia masilahi ya taifa fulani.
Mifano ni Kufa na Kupona na Kikosi cha Kisasi.
- Mkondo wa historia binafsi
Mkondo huu unajikita katika hadithi zinazohusu maisha ya mtu binafsi.
Mifano ni Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (Shaaban Robert).
Kutunga Riwaya Fupi
Ili kutunga riwaya au hadithi fupi na kuhakikisha ujumbe unamfikia hadhira, ni lazima kuzingatia mambo yote yanayohusu hadithi kwa ujumla, kama tulivyoona kwenye maelezo yaliyopita.
Hata hivyo, hii ni misingi ya kuzingatia kuhusu uandishi wa riwaya fupi
- Riwaya ya namna hii lazima iwe fupi.
- Huwa na mhusika mmoja anayejitokeza kuliko wahusika wengine.
- Idadi ya wahusika ni ndogo ukilinganisha na ile ya riwaya ndefu.
- Mandhari yake si pana kama ya riwaya ndefu.
- Huzungumzia dhamira moja.
- Hutumia lugha ya kisanaa.
Kutunga Tamthiliya
Maana ya tamthiliya
Tamthiliya ni kazi ya fasihi andishi iliyoandikwa kwa lengo la kuonyeshwa kama igizo jukwaani. Wahusika huzungumza na kutenda vitendo mbalimbali.
Sanaa hii huigiza maisha ya kila siku ya jamii.
Tamthiliya pia huitwa drama, maigizo au michezo ya kuigiza.
Aina za tamthiliya
- Tanzia
Tanzia ni tamthiliya inayoibua hisia za huzuni, woga au hofu kwa hadhira. Mwisho wa mhusika mkuu huwa wa kuhuzunisha, kwa mfano kufa.
- Ramsa
Ramsa ni tamthiliya ambayo mhusika mkuu hupambana na vikwazo vingi vizito, lakini mwisho wake huwa mzuri na wa kufurahisha. Kwa mfano, kuwashinda maadui.
Ramsa ni kinyume cha tanzia.
- Vichekesho
Vichekesho ni tamthiliya ambayo lengo lake kuu ni kuchekesha na kufurahisha. Pia hufundisha mambo mengi katika jamii, ingawa huwasilishwa kwa njia ya vichekesho.
Dhamira za tamthiliya
Tamthiliya ina dhamira zifuatazo
- Huburudisha jamii.
- Huelimisha jamii.
- Hukosoa jamii.
- Ni chanzo cha ajira kwa vijana.
- Ni chachu ya mabadiliko kwa jamii.
Mbinu za utungaji wa tamthiliya
- Chagua dhamira au jambo la kuandika.
- Panga ploti au msuko wa matukio.
- Buni wahusika watakaoendana na kile unachokiandika.
- Chagua mandhari yanayofaa kwa wahusika na jambo unaloliandika.
- Tumia mtindo wa mazungumzo na majibizano kati ya wahusika.
- Gawa tamthiliya katika maonyesho, yaani onyesho la kwanza, onyesho la pili na kadhalika.
- Weka maelekezo ya jukwaa.
- Tumia lugha ya kisanii, kwa mfano tamathali za semi.
- Jumuisha mbinu nyingine kama ucheshi, taharuki na kadhalika.
Maswali
- Eleza maana ya (a) fasihi simulizi (b) fasihi andishi.
- Kuna aina ngapi za riwaya? Zitaje.
- Orodhesha hatua za kufuata ili kuweza kutunga kazi ya fasihi andishi.
- Tamthiliya ina umuhimu gani katika jamii yako?
- Eleza maana ya wahusika wajenzi.
- Nini tofauti kati ya riwaya pendwa na riwaya dhati?
