Mjengo wa tungo
Dakika 9 za kusoma ·
Yaliyomo
Mjengo Wa Tungo
Tungo:
Tungo ni kipashio katika lugha ambacho mtu anakisema au anakiandika.
Tungo inaweza kuwa neno moja au zaidi.
Pia tungo inaweza kutoa taarifa kamili au isiyo kamili.
Mfano
- Taarifa kamili: Tulionana na Musa.
- Taarifa isiyo kamili: Baada ya kumtafuta sana.
Katika mfano huo hapo juu, mfano wa kwanza unatoa taarifa kamili kwamba walikutana na Musa.
Mfano wa pili si kamili. Hautoi taarifa inayoeleweka. Haujasema baada ya kumtafuta sana kulifuata nini, au nini kilitokea na kusababisha kumtafuta sana. Kwa hiyo sentensi ya pili siyo kamili.
Tungo zimegawanyika katika makundi makuu matatu. Aina hizo ni zifuatazo
- TUNGO KIRAI
- TUNGO KISHAZI
- TUNGO SENTENSI
Tungo Kirai
Kirai ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi.
Kirai ni tungo ambayo haigawanyiki katika sehemu ya kiima au kiarifu. Badala yake, kirai huwa ni sehemu tu ya ndani ya sentensi.
Kuna aina tano za virai
- Kirai Nomino au kikundi nomino (KN)
- Kirai Kitenzi (KT)
- Kirai Kielezi (KE)
- Kirai Kivumishi (KV)
- Kirai Kiunganishi (KU)
Chunguza jedwali hapa chini. Kiima ni KN. Kiarifu ni KT na KE.
- Mama (KN) | Anapika (KT) | Vizuri (KE)
- Baba (KN) | Alikua anatembea (KT) | Kuelekea sokoni (KE)
Mifano inaonyesha kuwa kirai kinaweza kuundwa kwa neno moja au zaidi.
Kirai nomino au kikundi nomino (KN)
Kirai nomino ni neno moja au zaidi yanayofanya kazi ya nomino. Yaani, hutaja mtu, kitu, mahali au hali.
Neno kuu katika aina hii ya kirai ni nomino.
Kirai nomino kinaweza kuundwa kwa
- Nomino tu (N)
Mfano: Juma ni rafiki yangu.
Mfano: Ng'ombe wanakula majani.
- Nomino mbili au zaidi
Mfano: Baba na Mama wanakula.
Mfano: Nimenunua shati na suruali.
- Nomino na kivumishi (N+V)
Mfano: Tumekunywa maji baridi.
Mfano: Koti jeusi limepotea.
Mfano: Safari ndefu inachosha.
- Kiwakilishi tu (W)
Mfano: Yeye ni rafiki yangu.
Mfano: Ametukabidhi sisi.
- Nomino na kishazi tegemezi (N+Ktg)
Mfano: Watoto waliofika mapema wameondoka.
Mfano: Gari lililoibiwa limepatikana.
Kirai kitenzi (KT)
Kirai kitenzi ni kipashio cha lugha kinachofanya kazi ya kitenzi. Yaani, huelezea kitendo ndani ya tungo.
Kirai kitenzi huundwa kwa neno moja au zaidi.
Neno kuu ndani ya kirai kitenzi ni kitenzi.
- Kitenzi kikuu (T)
Mfano: Mwalimu anafundisha.
Mfano: Mama anapika.
Mfano: Joni ataimba.
- Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu (Ts + T)
Mfano: Wanafunzi walikuwa wanaongea.
Mfano: Shamimu anajua kuimba.
Mfano: Frola anapenda kusoma.
- Kitenzi kishirikishi (t)
Mfano: Wewe utakuwa Mwenyekiti.
Mfano: Huyu si Mwalimu.
Mfano: Juma ni mchapakazi.
Kirai kielezi (KE)
Kirai kielezi ni neno moja au zaidi yanayofanya kazi ya kielezi. Yaani, hutoa taarifa zaidi kuhusu kitenzi au tendo.
Kirai kielezi hutoa taarifa zinazojibu maswali kama lini, wapi, kwa vipi na mara ngapi.
Mfano
- Lini? Alikuja asubuhi sana.
- Wapi? Amekaa sakafuni.
- Kwa vipi? Musa alishuka kiaskari.
- Mara ngapi? Tunakutana mara kwa mara.
Maneno yaliyoandikwa kwa mcharazo ndiyo kirai kielezi.
Kirai kivumishi (KV)
Kirai kivumishi ni maneno yanayofanya kazi ya kuvumisha. Yaani, yanatoa taarifa zaidi kuhusu nomino au kiwakilishi.
Neno kuu ndani ya kirai ni kivumishi.
Mara nyingi virai vivumishi huwa sehemu ya kirai nomino.
Mfano
- (Mwanafunzi mkimya zaidi) amekuwa wa kwanza.
- (Mtu mkatili kama huyo) atatupwa gerezani.
- (Punda mzito kupita kiasi) ameninunuliwa.
Maneno yaliyoandikwa kwa mcharazo ndiyo virai vivumishi.
Kirai kiunganishi (KU)
Hiki ni kirai ambacho neno linalotawala ndani yake ni kiunganishi.
Kwa kawaida, kiunganishi hiki hufuatiwa na kirai nomino.
Tazama mifano ifuatayo
Amesafiri kwa ndege.
Utanikuta kwenye ukumbi.
Vishazi
Kishazi ni tungo ambayo inaweza kutoa taarifa kamili au isiyo kamili.
Kishazi ni tungo ambayo ndani yake kuna kitenzi, kiima na kiarifu.
Mfano: Wale waliofika mchana walishangiliwa na kila mtu.
Aina za vishazi
- Kishazi tegemezi
- Kishazi huru
- Kishazi tegemezi:
Kishazi tegemezi ni kishazi ambacho kikisimama peke yake hakitoi taarifa kamili.
Mfano
- Iliyoungua moto
- Tunayoikaribia
- Atakayejibu swali hili
Kishazi tegemezi kina sifa zifuatazo
- Hakijitoshelezi kimaana
Mfano
- Tuliwaona kule mjini
- Yaliyomwagika pale
Ili vishazi hivi vilete maana iliyokamilika, vinahitaji kuongezewa kishazi huru.
Mfano: Watu tuliowaona kule mjini washaondoka.
- Huweza kufanya kazi kama kiima kwenye sentensi
Mfano: Tuliowaona wanatafuta kazi.
Hapa "Tuliowaona" ni kiima (K) na "wanatafuta kazi" ni kiarifu (A).
- Huweza kufanya kazi kama shamirisho kwenye sentensi
Mfano: Nilimwona aliyetupigia simu.
Hapa "Nilimwona" ni kitenzi (T) na "aliyetupigia simu" ni shamirisho (Sh), yaani kishazi tegemezi (KTg).
Mfano: Anahitajika atakayekubali masharti haya.
Hapa "Anahitajika" ni kitenzi (T) na "atakayekubali masharti haya" ni shamirisho (Sh), yaani kishazi tegemezi (KTg).
- Kishazi huru:
Hiki ni kishazi chenye kitenzi ambacho kinatoa taarifa kamili.
Mfano
- Kipindi kimeanza
- Nazi zimeanguka
- Nitamueleza kila kitu
- Juma alikua anapika ugali
Kishazi huru kina sifa zifuatazo
- Kinajitosheleza kimaana
Mfano
- Jamila anapenda kuimba
- Maji haya ni safi
- Kitenzi chake ni sehemu ya kiarifu cha sentensi
Mfano
- Helena anapenda kuimba. (T ni sehemu ya A)
- Maji haya ni safi. (t ni sehemu ya A)
- Kitenzi chake huweza kuwa kitenzi kikuu, kitenzi kishirikishi, au kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu
Mfano
- Rajabu atakuja kesho. (T)
- Huyu si mwalimu. (t)
- Asma anataka kula chakula chake. (Ts + T)
Sentensi
Sentensi ni tungo inayotoa taarifa kamili ambayo imeundwa kwa kiima na kiarifu.
Kwa msingi huu, vishazi huru vyote ni sentensi kwa kuwa vinatoa taarifa kamili.
Kiima (K)
Kiima ni sehemu ya sentensi ambayo huonyesha mtenda au mtendwa wa kitenzi cha sentensi.
Mfano
- Masumbuko hajaacha ulevi. (Kiima: N)
- Joyce na Fatuma ni maadui. (Kiima: N + N)
- Mashati meusi huchukiza sana. (Kiima: N + V)
- Hawa mbuzi wanauzwa. (Kiima: V + N)
- Wale pale wanafahamu aliko. (Kiima: W + V)
Kiarifu (A)
Kiarifu ni sehemu ya sentensi inayotoa taarifa kuhusu kiima.
Yaani, kinaeleza mtenda alitenda nini au mtendwa alitendwa nini, lini, wapi, kwa vipi, na kwa nini.
Kiarifu kinaweza kuundwa na vipashio mbalimbali. Vipashio hivyo ni kitenzi kikuu, shamirisho na chagizo.
Mifano
- Benjamin amelala (T)
- Huyu ni mwimbaji (t + Sh)
- Bahati amefungua mgahawa (T + Sh)
- Kobe anatembea polepole (T + Ch)
- Sisi tulimwona mwalimu mjini (T + Sh + Ch)
Kumbuka
Shamirisho (Sh) ni nomino au kikundi nomino kinachotokea baada ya kitenzi ili kujibu swali la mtenda katenda nini.
Mfano: Golikipa alidaka mpira. Neno mpira ni shamirisho linalojibu swali "golikipa alidaka nini?"
Chagizo (Ch) ni neno au maneno yanayotokea baada ya kitenzi na kufanya kazi kama kielezi.
Mfano: Jogoo aliwika asubuhi. Neno asubuhi ni chagizo linaloeleza muda wa kuwika.
Aina Za Sentensi
Kuna aina nne za sentensi
- Sentensi sahili (S.S)
- Sentensi changamano (S.Ch)
- Sentensi ambatano (S.A)
- Sentensi shurutia (S.Sh)
Sentensi sahili (S.S)
Sentensi sahili ni sentensi inayoundwa na kishazi huru kimoja.
Sentensi ya aina hii huwa na kitenzi kikuu kimoja. Hata hivyo, inaweza kuwa na kitenzi kisaidizi kimoja au zaidi, au ikawa na kitenzi kishirikishi.
Mifano
- Watoto wanaimba (T)
- Mrisho alikua amelala (Ts + T)
- Sisi tumekuwa tunahitaji kuzungumza naye (Ts + Ts + T)
- Wale ni maadui zangu (t)
Vilevile, sentensi sahili inaweza kuundwa kwa kitenzi kikuu peke yake, au kwa kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu.
Mifano: Anakula, tuliwahi, tutakuwa tumeondoka.
Sentensi changamano (S.Ch)
Hii ni sentensi inayoundwa na kishazi huru na kishazi tegemezi.
Vishazi hivi vinaweza kuwa kimoja au zaidi.
Mifano
- Mkate uliotupatia umeharibika. (Uliotupatia = KTg; umeharibika = KHr)
- Mtoto aliyetuletea chakula ofisini anaitwa Salimu. (Aliyetuletea chakula ofisini = KTg; anaitwa Salimu = KHr)
Sentensi ambatano (S.A)
Sentensi ambatano ni muunganiko wa sentensi mbili au zaidi.
Sentensi hizi zinaweza kuwa sahili, au changamano, au changamano na sahili.
Mifano
- Dada ataimba au kaka ataimba. (Sahili + Sahili)
- Mtu aliyepotea ameonekana na wale wanaomtafuta hawajarudi. (Changamano + Changamano)
- Mwizi aliyekamatwa amehukumiwa lakini amekata rufaa.
Sentensi shurutia (S.Sh)
Sentensi hii huundwa na viambishi kama vile -NGELI-, -NGE- na -NGALI-.
Mifano
- Ningeli mwambia angelinisaidia japo kidogo.
- Angaliomba msamaha angalisamehewa.
- Wazazi wetu wasingetulea katika maadili mema tusingekuwa na maisha mazuri.
Pia sentensi shurutia hutumia kiambishi -ki-.
Mifano
- Wakikimbia tutawakimbiza.
- Nikiwaona nitawaeleza kinagaubaga.
- Akila samaki huyu, atatoka vidonda.
Kuchanganua Sentensi
Uchanganuzi wa sentensi ni kubainisha viambajengo vinavyounda sentensi.
Viambajengo ni vipashio vinavyotumika kuijenga sentensi hiyo.
Muundo wa sentensi huanzia neno, kirai, kishazi, hadi sentensi kamili.
Njia za kuchanganua sentensi
Sentensi huweza kuchanganuliwa kwa njia nne
- Kuchanganua sentensi kwa njia ya maneno.
- Kuchanganua sentensi kwa njia ya majedwali.
- Kuchanganua sentensi kwa njia ya matawi.
- Kuchanganua sentensi kwa njia ya mshale.
Lakini katika kidato cha tatu, uchanganuzi unaweza kufanywa kwa njia mbili. Njia hizo ni majedwali na matawi.
(a) Kuchanganua sentensi kwa njia ya majedwali
- Makoba atakuwa amelewa (S.S)
- K (kiima): Makoba = N
- A (kiarifu): atakuwa = Ts, amelewa = T
- Kijana mweupe amenunua gari jeusi. (S.S)
- K (kiima): Kijana = N, mweupe = V
- A (kiarifu): amenunua = T, gari = N, jeusi = V
- Gari jeusi ni shamirisho (Sh).
- Watoto waliokuja leo wataondoka kesho jioni. (S.Ch)
- K (kiima): Watoto = N, waliokuja leo = KTg (kishazi tegemezi), ambapo waliokuja = V na leo = E
- A (kiarifu): wataondoka = T, kesho jioni = Ch, ambapo kesho jioni = E
- Ochincho ataenda shuleni na Wambura ataenda sokoni. (S.A)
- S1: Ochincho ataenda shuleni. K = Ochincho (N); A = ataenda (T) shuleni (E)
- U (kiunganishi): na
- S2: Wambura ataenda sokoni. K = Wambura (N); A = ataenda (T) sokoni (E)
(b) Kuchanganua sentensi kwa njia ya matawi
- Fatuma ameanguka bafuni. (S.S)
- K: N = Fatuma
- A: T = ameanguka, E = bafuni
- Mama amepika chakula. (S.S)
- K: N = Mama
- A: T = amepika, Sh = chakula
- Mwizi aliyetusumbua sana amekamatwa kichakani. (S.Ch)
- K: N = Mwizi; KTg = aliyetusumbua sana (V = aliyetusumbua, E = sana)
- A: T = amekamatwa, E = kichakani
- Mariamu alipika chakula na Nasri alienda shambani. (S.A)
- S1: K = Mariamu (N); A = alipika (T) chakula (Sh)
- U (kiunganishi): na
- S2: K = Nasri (N); A = alienda (T) shambani (E)
Kazi Ya Nyumbani
Changanua sentensi zifuatazo kwa njia ya matawi na majedwali
- Amina ana haraka lakini Juma ana penda kutulia.
- Mtoto mdogo analima shambani.
- Dada aliyepotea jana amekutwa kauawa.
- Nipatie kalamu na daftari.
- Mariam amefungua duka.
- Watu wote walimsikiliza Rais kwa makini.
- Mwanafunzi aliyefaulu zaidi alipatiwa cheti.
Maswali
- Eleza maana ya sentensi.
- Eleza maana ya maneno yafuatayo:
- Kirai
- Kishazi
- Kishazi huru
- Kishazi tegemezi
- Tunga sentensi kwa kutumia vijenzi vifuatavyo:
- N + T
- T + E
- N + Ts + T + E
- Kuna utofauti gani kati ya tungo na sentensi?
- Eleza maana ya kiima na kiarifu.
- Tunga sentensi tano na uonyeshe:
- Virai nomino
- Virai vitenzi
