Kusoma kwa ufahamu na
Dakika 3 za kusoma ·
Yaliyomo
Kufupisha Habari
Ufahamu ni sehemu katika somo la lugha. Sehemu hii inatoa maarifa kuhusu kuelewa habari zilizoandikwa au zilizozungumzwa.
Kuelewa kifungu cha habari ni uwezo wa akili. Uwezo huu unamwezesha mtu kufafanua au kueleza kwa ufasaha jambo alilosoma au alilosikia.
Aina Za Ufahamu
Kuna aina mbili za ufahamu
- 1. Ufahamu wa kusoma.
- 2. Ufahamu wa kusikiliza.
Ufahamu Wa Kusoma
Huu ni ufahamu unaotokana na kusoma habari zilizoandikwa katika vitabu, majarida, vipeperushi, n.k.
Wataalamu wanasema kusoma kwa kimya ni bora zaidi kuliko kusoma kwa sauti. Kusoma kimya kunaongeza kazi ya usomaji.
Ili kuwa na ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo
- 1. Kubaini mawazo makuu.
- 2. Kuzingatia mawazo makuu.
- 3. Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali.
- 4. Kutilia maanani vidokezo vya maana.
Zifuatazo ni maana mbalimbali za maneno yanayodokeza maana hizo
- a. Kuanza: kwanza, kabla ya yote, jambo la kwanza, n.k.
- b. Kuongeza: pia, vilevile, zaidi ya hapo, n.k.
- c. Mtiririko: kwanza, pili, tatu, n.k.
- d. Kutofautisha: lakini, isipokuwa, hata hivyo, n.k.
- e. Kuhitimisha: hata hivyo, hivyo, mwisho, hatimaye, n.k.
Ufahamu Wa Kusikiliza
Huu ni ufahamu unaopatikana kutokana na kumsikiliza mtu anayezungumza.
Mtu huyo anaweza kuwa kiongozi anayeongea jukwaani. Anaweza kuwa mwalimu anayefundisha darasani. Anaweza pia kuwa mwelimisha rika anayetoa elimu kuhusu kujikinga na magonjwa mbalimbali kama UKIMWI, Kifua kikuu, n.k.
Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo
- 1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kusikia kwa makini kila kinachozungumzwa.
- 2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini kama msemaji anaongea jambo jipya, anafafanua, anatofautisha au anahitimisha jambo.
- 3. Kuandika kwa ufupi mambo yanayozungumzwa.
- 4. Kuwa makini na ishara mbalimbali za mwili anazotumia mzungumzaji. Ishara huchangia katika maana nzima ya mazungumzo.
Kufupisha Habari
Ufupisho wa habari ni kitendo cha kuandika habari ndefu kwa maneno machache.
Ufupisho unatakiwa kuwa na sifa zifuatazo
- 1. Huwa mfupi kuliko habari ya mwanzo.
- 2. Huwa na maana ileile iliyokuwa kwenye habari ya mwanzo.
- 3. Hujumuisha mawazo makuu yaliyochukuliwa kutoka kwenye habari ya mwanzo.
- 4. Mawazo huwa yamepangwa kimantiki ili maana iwe wazi na ya ufasaha.
Hatua Za Kufuata Katika Kuandika Ufupisho
Ili kuandika ufupisho, kuna mambo muhimu ya kuzingatia kama ifuatavyo
- Soma habari mara mbili au zaidi ili kuielewa kwa ufasaha.
- Bainisha mawazo makuu kutoka kwenye habari.
- Andika ufupisho kwa lugha ya ufasaha, na mtiririko wa hoja wenye mantiki unaoeleweka.
- Hesabu maneno ili kuhakikisha hujazidisha idadi ya maneno uliyopangiwa.
- Pitia habari tena kwa umakini. Pitia pia ufupisho ili kurekebisha na kuhakikisha hujaacha taarifa muhimu.
Mfano Wa Ufupisho
Swali: Fupisha makala ifuatayo kwa maneno 27.
Makala
Rais wa jamhuri ya Mawenzi, Mheshimiwa Abdulrazak Athumani, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo (CHAMA) kinachotawala, amesema kuwa hatakuwa na urafiki au upendeleo wowote katika kuunda baraza lake la mawaziri.
Msimamo huu ni tofauti sana na uvumi ulioenea kama moto katika mbuga.
Rais Abdulrazak alitoa kauli hiyo ya kuvunja ukimya wa muda mrefu, ukimya uliokuwa unatishia kuleta vurugu. Alizungumza na waandishi wa habari wa Malaika Redio, Mshale na Sauti ya Watu katika ikulu hiyo ya White House, jijini Mbala.
Ufupisho
Rais wa Mawenzi, Mheshimiwa Abdulrazak, amesema kuwa hatakuwa na upendeleo katika uteuzi wa mawaziri kinyume na uvumi. Rais alisema haya alipowahutubia waandishi wa habari ikulu jijini Mbala.
Maswali
- Kwa ufupi eleza tofauti iliyopo baina ya ufahamu wa kusoma na ufahamu wa kusikiliza.
- Taja mambo muhimu ya kuzingatia katika ufahamu wa kusikiliza.
- Eleza maana ya ufupisho.
- Bainisha hatua za kufuata katika kuandika ufupisho.
- Andika mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandika ufupisho.
