Kiswahili · Kidato 3

Uandishi wa insha na matangazo

Dakika 5 za kusoma ·

Yaliyomo

Kuzungumza Na Kusikiliza

Insha ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumzwa au kuandikwa.

Insha inaweza kuwa ndefu au fupi. Insha inaweza kuwa aya moja au zaidi. Kawaida kila aya hubeba wazo maalum.

Muundo Wa Insha

Muundo wa insha huzingatia mambo yafuatayo

  1. Kichwa cha insha. Huandikwa kwa herufi kubwa, juu ya insha. Huandikwa kwa ufasaha na kwa muhtasari. Huzingatia wazo kuu la insha.
  1. Mwanzo. Huzingatia jambo linalozungumzwa.
  1. Kiini cha insha. Hii ndiyo sehemu kuu ya insha.
  1. Mwisho wa insha. Hutoa msisitizo kwa yaliyojadiliwa. Huwa na maoni na mapendekezo ya mwandishi.

Mambo Ya Kuzingatia Katika Uandishi Wa Insha

  1. Kuzingatia kichwa cha habari na maelezo kama yapo.
  1. Kuandika kwa kutumia taratibu za uandishi na lugha fasaha.
  1. Kutotumia lugha ya mkato. Kwa mfano, usiandike "n.k." badala ya "nakadhalika".
  1. Kuandika utangulizi unaovuta umakini wa wasomaji au wasikilizaji.
  1. Kuandika kiini cha insha kwa mpangilio unaofaa.
  1. Kuandika mwisho wa insha unaovutia.

Aina Za Insha

Kuna aina mbili za insha

  1. Insha za kisanaa.
  1. Insha zisizo za kisanaa.

Insha za kisanaa hutumia lugha ya kifasihi. Maneno ya kawaida hubadilishwa na kuwa ya kisanaa.

Insha zisizo za kisanaa huitwa pia insha za kiada. Hutumia lugha isiyo ya kifasihi. Lugha ya kisanaa hubadilishwa na kuwa lugha ya kawaida.

AU

Insha za kiada ni insha zisizo za kisanaa. Huwa na lugha ya kawaida, bila semi na mbinu nyingine za kisanaa.

Insha za kiada au insha zisizo za kisanaa zinaweza kuwa insha za hoja au za wasifu.

Insha za hoja ni insha zinazotetea mawazo fulani.

Insha za wasifu huelezea sifa za watu, vitu na wanyama.

Dhana Ya Uandishi Na Alama Za Uandishi

Dhana ya uandishi

Uandishi ni upangaji wa maneno katika karatasi kwa namna itakayomwezesha msomaji kupata maana iliyokusudiwa.

Kuna mambo makuu mawili ya kuzingatia ili kufikisha ujumbe kwa maandishi

  1. Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.
  1. Kutumia kwa usahihi alama za uandishi, kama vile nukta, mkato na ulizo.

Alama Za Uandishi

Alama za uandishi huweza kuwekwa mwisho wa sentensi au ndani ya sentensi.

Alama zinazokaa mwisho wa sentensi ni nukta, alama ya kuuliza na alama ya mshangao.

Zifuatazo ni alama tofauti za uandishi

  1. Nukta (.)

Hii ni alama inayowekwa mwisho wa sentensi kuashiria kukamilika kwa taarifa.

  1. Ulizo (?)

Hii ni alama inayoashiria kuuliza swali.

  1. Alama ya mshangao (!)

Hii ni alama inayoonyesha hisia kali, kama vile mshtuko, hasira na kushangazwa na jambo.

  1. Mkato (,)

Alama hii inaonyesha pumziko fupi katika sentensi. Pia hutumika kutenganisha vitu vilivyo katika orodha.

  1. Nukta pacha (:)

Hutumika kuashiria kuwa baada yake inafuata orodha.

  1. Nukta na mkato (;)

Alama hii hufanya kazi kama kiunganishi, yaani huunganisha tungo zaidi ya moja.

  1. Alama za kufungua na kufunga semi (" ")

Ni alama zinazotumiwa kurejea maneno yaliyotamkwa na mzungumzaji wa kwanza.

  1. Kistari (-)

Ni alama inayotumika kuashiria maelezo zaidi, yaani maelezo yanayofafanua jambo lililosemwa kabla yake.

Matangazo

Tangazo ni taarifa ya wazi inayotoa ujumbe fulani kwa wanaohusika na ujumbe huo.

Kwa mfano, tangazo la mkutano linalenga kuwataarifu wahusika kwamba kutakuwa na mkutano siku fulani, mahali fulani, muda fulani na kuhusu mada fulani.

Matangazo mengine ni ya bidhaa tofauti kama sabuni, unga na pipi. Hutangazwa kushawishi watu kununua bidhaa hizo. Pia hutangazwa kuonyesha kuwa ni bidhaa bora kabisa kuliko nyingine.

Malengo ya matangazo

  1. Kutoa taarifa

Matangazo yanayotoa taarifa ni kama vile alama za barabarani, mialiko ya mikutano, kupotelewa na vitu, matangazo ya zabuni na kutangaza bidhaa.

  1. Kuonya

Matangazo yanayoonya ni kama vile matangazo kuhusu hatari ya UKIMWI, uvutaji wa sigara na mwendo kasi barabarani.

  1. Kupata wateja

Haya ni matangazo yanayotolewa kwa lengo la kuwashawishi wateja kununua bidhaa fulani. Bidhaa hizo zaweza kuwa biskuti, simu ya mkononi, vinywaji vya kula na zana za ufundi.

Matangazo haya pia yanaweza kuwa ya kutafuta wateja wa shule, vyuo na tiba.

Mifano Ya Matangazo

Mfano wa kwanza

Kozi Kozi Kozi

CHUO CHA KILIMO KILICHOPO MOROGORO KINAWATANGAZIA NAFASI ZA KOZI YA KILIMO CHA MAZAO YA AINA ZOTE.

MUDA WA KOZI NI MIAKA MIWILI.

ADA YA KOZI NI SHILINGI MILIONI MBILI.

KUNA WALIMU WENYE UJUZI NA UTAALAMU WA HALI YA JUU.

NJOO UPATE UJUZI UTAKAOKUSAIDIA KUJIAJIRI MWENYEWE.

KWA MAELEZO ZAIDI FIKA CHUONI MOROGORO AU WASILIANA NASI KWA NAMBA.

WANAFUNZI ISHIRINI WA MWANZO WATAPATIWA PUNGUZO LA BEI LA ASILIMIA THELATHINI.

Wahi Sasa, Nafasi Ni Chache!

WOTE MNAKARIBISHWA.

Mfano wa pili

Semina Semina Semina

Chama Cha Walimu Tanzania (Cwt)

KINAWATANGAZIA WALIMU WOTE NCHINI KUWA KUTAKUWA NA SEMINA KUHUSU UFUNDISHAJI KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA, YAANI TEHAMA.

Semina Hiyo Itaendeshwa Kwa Mikoa Kama Ifuatavyo:

  • MKOA WA TANGA, PWANI NA DAR ES SALAAM: 03/05/2018 – 09/05/2028
  • MKOA WA MTWARA, LINDI, RUVUMA, RUKWA NA SONGEA: 10/05/2018 – 19/05/2018
  • MKOA WA MBEYA, IRINGA, RUKWA NA MOROGORO: 20/05/2018 – 29/05/2018
  • MKOA WA DODOMA, SINGIDA, TABORA NA SHINYANGA: 30/05/2018 – 08/06/2018
  • MKOA WA MWANZA, KAGERA NA MUSOMA: 09/06/2018 – 18/06/2018

WOTE MNAKARIBISHWA.

IMETOLEWA NA MKURUGENZI MKUU WA ELIMU TANZANIA.

Mambo Ya Kuzingatia Katika Uandishi Wa Matangazo

  1. Kichwa cha habari. Ni muhimu tangazo liwe na kichwa cha habari ili mlengwa akione mara moja anapotazama tangazo hilo.
  1. Aina ya bidhaa au huduma. Tangazo lazima lionyeshe wazi aina ya bidhaa au huduma inayotangazwa.
  1. Mahali ambapo huduma au bidhaa inapopatikana.
  1. Njia za mawasiliano. Mfano: anwani ya posta, namba za simu au barua pepe.

Mbinu Mbalimbali Zinazotumika Katika Uandishi Wa Matangazo

  1. Uwekaji wa picha.
  1. Maneno machache yasiyomchosha mlengwa.
  1. Lugha ya kisanii. Mfano: "nzuri sana", "punguzo ni kubwa halijawahi kutokea" na kadhalika.
  1. Watu maarufu. Mfano: tangazo la kinywaji cha Pepsi limemwonyesha mchezaji maarufu Messi akinywa kinywaji hicho.

Maswali

  1. Insha ni nini?
  1. Eleza mambo ya kuzingatia katika uandishi wa insha.
  1. Fafanua dhana ya uandishi.
  1. Unafikiri kuna umuhimu wowote wa kufuata alama za uandishi? Kwa nini?
  1. Taja malengo matatu ya matangazo.
  1. Orodhesha mbinu mbalimbali zinazotumika katika uandishi wa matangazo.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 31