Kiswahili · Kidato 3

Maendeleo ya kiswahili

Dakika 8 za kusoma ·

Yaliyomo

Maendeleo Ya Kiswahili

Kiswahili ni lugha iliyoanza kuzungumzwa katika upwa wa pwani ya Afrika Mashariki.

Ilizungumzwa katika maeneo mbalimbali kama vile Lamu, Pate, Mombasa, Bagamoyo, Kilwa, na kadhalika.

Tabia Za Lugha

Lugha ni chombo cha msingi cha mawasiliano kati ya watu katika jamii kwa ujumla.

Lugha zina tabia zifuatazo

  1. Lugha ina asili au chimbuko lake.
  1. Lugha huweza kufa. Mfano: Kilatini ni lugha mfu kwa sasa.
  1. Lugha huweza kukopa msamiati wa lugha nyingine, au kukopesha msamiati wake kwenye lugha nyingine.
  1. Lugha ina tabia ya kukua kadri muda unavyozidi kwenda. Hii ni kutokana na maendeleo na uvumbuzi wa mambo mapya katika jamii zetu.
  1. Lugha huweza kuwa katika makundi tofauti. Kwa mfano, inaweza kuwa katika kundi la lugha za Kibantu. Hivyo maneno mengi katika lugha hizo yanaweza kukaribiana kimaana na kimatamshi.

Mfano wa neno "mtu" katika lugha mbalimbali

  • Kiswahili: mtu
  • Kiha: umuntu
  • Kinyaturu: muntu
  • Kihehe: munu
  • Kisukuma: muntu
  • Kihaya: omuntu

Asili Ya Kiswahili

Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999:3), neno asili linamaanisha jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza.

Hivyo, asili ya Kiswahili maana yake ni namna lugha ilivyotokea au ilivyoanza.

Kwa ujumla, kujua asili ya Kiswahili ni kujua lugha hiyo imetokea wapi, wakati gani, na ilianzia wapi.

Inaaminika kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu. Lugha hizi zinazungumzwa katika pwani ya Afrika Mashariki kuanzia Somalia, Pate, Mombasa, Lamu, Bagamoyo, Dar es Salaam, Kilwa, Ras Delgado hadi Msumbiji.

Wataalamu mbalimbali walichunguza lugha na vipengele vingine vya utamaduni wa Wabantu. Uchunguzi huo unaonyesha kuwa chimbuko la Wabantu ni Afrika ya Magharibi.

Uchunguzi huo pia unaonyesha kuwa Wabantu walihama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Walihama kwa vipindi tofauti na kwa muda mrefu.

Wabantu walianza kusambaa katika sehemu tofauti. Mfano: walingia nyanda za kati za Afrika Mashariki mnamo karne ya kwanza na ya pili B.K. Walitokea eneo la kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, sehemu za Katanga.

Walipokuja Afrika Mashariki, walikuja kwa makundi na katika nyakati tofauti.

Makundi hayo yalianza kugawanyika na kusababisha makundi mbalimbali katika upwa wa pwani ya Afrika Mashariki. Baadhi ya makundi hayo yalisambaa katika nyika za tambarare za Afrika Mashariki.

Siku zilivyozidi kwenda, tofauti zilianza kujitokeza katika uzungumzaji wa lugha zao. Hii ilitokana na athari ya mazingira ya pwani.

Wakazi wa sehemu mbalimbali walianza kutofautiana katika maumbo ya maneno na matamshi. Tofauti hizi zilisababisha kuzuka kwa lahaja au vilugha vya Kiswahili.

Lahaja zilizotumika ni pamoja na

  • Kiunguja na Kimakunduchi: vinazungumzwa katika kisiwa cha Unguja.
  • Kipemba: kinazungumzwa katika kisiwa cha Pemba.
  • Kimafia: kinazungumzwa katika kisiwa cha Mafia.
  • Kivumba na Kimtang'ata: vinazungumzwa katika sehemu za kaskazini mwa Tanga.
  • Kijomvu, Kimvita na Chichifundi: vinazungumzwa sehemu za Malindi.
  • Kibajuni (Kigunya, Kitikuu): vinazungumzwa kusini mwa Somalia na kaskazini mwa Kenya.
  • Chimiini: kinazungumzwa sehemu za pwani ya Somalia.
  • Kingazija na Kinzwani: vinazungumzwa katika visiwa vya Komoro.

Ubantu Wa Kiswahili

Asili ya Kiswahili ni suala lililozua mjadala wa muda mrefu miongoni mwa wanaisimu wengi.

Wapo wanaodai kuwa Kiswahili ni lugha inayotokana na vizazi vya Waarabu na Waswahili.

Wataalamu hawa wanadai kuwa watoto waliozaliwa katika vizazi vya Waarabu na Waafrika hawakuzungumza Kiarabu wala lugha zao za Kiafrika. Badala yake walizungumza lugha ya kati, yaani Pijini. Pijini ilichanganya baadhi ya maneno ya Kiarabu na lugha za Kiafrika.

Wataalamu hawa wanaamini kuwa baadaye Pijini hiyo ilikomaa na kuwa Krioli. Krioli hiyo ndiyo Kiswahili tulichonacho leo.

Hata hivyo, kuna ushahidi unaopinga dhana hiyo. Ushahidi huo unadai kuwa Kiswahili si Pijini wala Krioli, bali ni Kibantu.

Uthibitisho Kuwa Kiswahili Ni Kibantu

  1. Msamiati wa msingi:

Msamiati wa msingi ni maneno yanayotaja vitu au dhana zinazopatikana katika jamii.

Misamiati mingi ya Kiswahili inafanana na ile ya Kibantu. Hii inathibitisha kuwa Kiswahili ni Kibantu.

Mifano

  • Mwana: Kiswahili mwana, Kiha umwana, Kinyaturu mwana, Kihehe umwana.
  • Jua: Kiswahili jua, Kiha izu?a, Kinyaturu yu?a, Kihehe lisuva.
  • Mtu: Kiswahili mtu, Kiha umuntu, Kinyaturu muntu, Kihehe munu.
  1. Nomino:

Umoja na wingi

Katika nomino nyingi za Kiswahili na lugha za Kibantu, maumbo ya umoja na wingi yanashabihiana.

Mifano

  • Kiswahili: mtu (umoja), watu (wingi).
  • Kihehe: munu (umoja), vanu (wingi).
  • Kizaramo: munu (umoja), wanu (wingi).
  • Kichaga: mndu (umoja), wandu (wingi).
  1. Upatanisho wa kisarufi:

Nomino za Kiswahili hudhihirisha upatanisho wa kisarufi kwa namna inayofanana kabisa na lugha nyingine za Kibantu.

Mifano ya nomino na kitenzi

  • Kiswahili: Mtoto anakwenda.
  • Kihehe: Mwana ibita.
  • Kigogo: Mwana alibita.
  1. Vitenzi:

Mwanzo wa vitenzi

Vitenzi vya Kiswahili mwanzoni huwa na viwakilishi vya nafsi. Jambo hili hubainika pia katika vitenzi vya lugha nyingine za Kibantu.

Mifano

  • Kiswahili: wanalima
  • Kigogo: valilima
  • Kibena: vilima
  • Kihehe: vilima

Mwisho wa vitenzi

Kama ilivyo kwa mwanzo wa vitenzi, kuna mfanano mkubwa kati ya viishio vya vitenzi vya Kiswahili na vya lugha nyingine za Kibantu. Vyote huishia na irabu.

Mifano

  • Kiswahili: anacheza
  • Kibena: akwihesiga
  • Kipare: acheza
  1. Mnyambuliko:

Utaratibu unaotumika kunyambulisha vitenzi vya Kiswahili ndio ule ule unaotumika katika vitenzi vya lugha nyingine za Kibantu.

Mifano

  • Kiswahili: cheka, chekwa, chekesha.
  • Kipare: theka, thekwa, thekeza.
  • Kisukuma: seka, sekwa, sekesha.
  1. Viambishi:

Katika vitenzi vya Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu, viambishi vinaendana. Yaani kuna viambishi awali, kiini na viambishi tamati.

Mifano (neno: kiambishi awali, kiini, kiambishi tamati)

  • Kiswahili: analima: a-na-, -lim-, -a
  • Kihehe: ilima: i-, -lim-, -a
  • Kinyaturu: ukulima: u-ku-, -rim-, -a
  • Kindali: akulima: a-ku-, -lim-, -a
  • Kigogo: alilima: a-li-, -lim-, -a
  1. Miundo ya sentensi:

Mpangilio wa maneno katika sentensi za Kiswahili unafanana na ule wa sentensi katika lugha za Kibantu.

Kiima ni nomino. Kiarifu kina kivumishi na kitenzi.

Mifano (nomino, kivumishi, kitenzi)

  • Kiswahili: Wana wawili wanaoga
  • Kingoni: Vana bavili visamba
  • Kichaga: Wana wawi wakesamba
  • Kizigua: Wana waidi wahaka
  • Kihaya: Abana babili m'boga

Sentensi hizi hazifanani tu kwa mpangilio wa maneno. Pia zinabainisha upatanisho wa kisarufi kati ya kiima na maneno mengine kwenye kiarifu.

Maendeleo Ya Kiswahili

Kiswahili Katika Enzi Ya Waarabu

Kabla ya kuja wageni wowote katika pwani ya Afrika Mashariki, wenyeji wengi wa pwani hiyo walikuwa tayari wakizungumza lugha ya Kiswahili.

Mnamo karne ya 10 B.K, Waarabu walifika katika upwa wa Afrika Mashariki.

Waarabu walikuja Afrika Mashariki kufanya biashara. Wakati huo huo walianza kusambaza dini ya Kiislamu katika mwambao wa Afrika Mashariki na visiwa vyake.

Kwa kujihusisha na biashara, Waarabu walifanikiwa kupenya hadi ndani ya Tanzania bara, kwa mfano mikoa ya Tabora na Kigoma.

Pia Waarabu walifanikiwa kufunga ndoa na wenyeji ambao ni Waswahili, na kuzaa watoto.

Baadaye, Waarabu waliishi kwa wingi katika visiwa vya Zanzibar kama watawala wa kikoloni.

Kwa hiyo, kutokana na uhusiano wa kibiashara, kiutawala, kidini na kifamilia uliokuwepo katika enzi za Waarabu, lugha ya Kiswahili ilizidi kupanuka. Ilipanuka kimsamiati, katika idadi ya wazungumzaji, na hata katika maeneo ya kuzungumzwa, yaani kuanzia pwani hadi bara.

Maneno ya Kiarabu yaliyoingia katika Kiswahili

Kuna maneno mengi yaliyoingia kwenye lugha ya Kiswahili kutoka katika lugha ya Kiarabu. Ifuatayo ni mifano ya maneno hayo:

  • Mashariki, Magharibi, Jahazi
  • Hakimu, shekhe, madrasa, inshaallah
  • Kurani, kadhi, sheha, sheria na sultani
  • Thamani, thelathini na thumuni

Pia kuna maneno mengine mengi.

Kiswahili Katika Enzi Ya Wajerumani

Ikumbukwe kwamba uwepo wa Waarabu katika upwa wa Afrika Mashariki haukuenea nchi nzima.

Wajerumani walipokuja nchini kwetu kama watawala wa kikoloni, walikuta lugha ya Kiswahili imesambaa kwa kiasi kikubwa kuliko enzi za Waarabu walipoanza kuingia kwa mara ya kwanza.

Tofauti na Waarabu, utawala wa Wajerumani ulienea nchi nzima. Sababu ni kwamba lengo lao lilikuwa kutawala.

Walianzisha shughuli za kiuchumi kama vile mashamba na migodi. Vilevile walijenga ofisi za kiutawala, shule na mahakama.

Juu ya hayo, Wajerumani walikuwa watawala wasimamizi wa hali ya juu na wakali sana kwa Waafrika. Hawakutaka watu legelege.

Hivyo, ili kuendesha shughuli zao za kiutawala kwa urahisi na kwa ufanisi, serikali ya kikoloni ya Kijerumani iliazimia kuanzisha mambo yafuatayo yanayohusu lugha ya Kiswahili:

  1. Lugha itakayotumika katika ofisi zote za serikali iwe Kiswahili.
  2. Shule zilizofunguliwa kufundisha watu weusi ili wawe wasaidizi katika utawala wa Wajerumani zilifundisha masomo kwa lugha ya Kiswahili.
  3. Watawala wa Kijerumani pia walijifunza Kiswahili ili kupata urahisi wa kuwasiliana na wenyeji wao.
  4. Kila akida alilazimika kufahamu lugha ya Kiswahili ili aweze kupelekwa kusimamia shughuli mbalimbali za kiutawala za Kijerumani, na si pale alipozaliwa tu.

Kwa hiyo, lugha ya Kiswahili ilipewa msukumo mkubwa na utawala wa Kijerumani, ikaweza kuenea na kusambaa kwa kasi kubwa. Hii ni kwa sababu shughuli zote za uzalishaji na za kiutawala zilizofanywa na Wajerumani zilitumia lugha ya Kiswahili.

Tofauti ya utawala wa Kiarabu na utawala wa Kijerumani

Waarabu walisaidia zaidi katika kukuza msamiati wa lugha ya Kiswahili.

Wajerumani walisaidia zaidi katika kueneza na kusambaza lugha ya Kiswahili katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu walifungua mashamba makubwa kila kona ya nchi, na lugha iliyotumika ilikuwa Kiswahili. Pia watawala na viongozi wengine wote walizungumza Kiswahili.

Hivyo, utawala wa Kijerumani ulisaidia sana kueneza lugha ya Kiswahili nchini kwetu.

Maneno ya Kijerumani katika Kiswahili

Baadhi ya maneno ya Kijerumani yaliyomo katika lugha yetu ya Kiswahili ni shule, hela na bruda.

Kazi Ya Nyumbani

  1. Kiswahili ni Kibantu. Thibitisha.
  2. Lugha zina tabia mbalimbali. Taja tabia tano za lugha.
  3. Fafanua mambo yaliyosaidia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili enzi za Waarabu na Wajerumani.

Maswali

  1. Eleza asili ya lugha ya Kiswahili.
  2. Kiswahili ni Kibantu. Jadili.
  3. Eleza mchango wa Waarabu katika kukuza Kiswahili.
  4. Taja tabia za lugha.
  5. Taja maneno matano ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 31