Utungaji…
Dakika 16 za kusoma ·
Yaliyomo
Utungaji
Utungaji ni maandishi ambayo yanatokana na akili ya mtu.
Utungaji hurejeshwa kwa fani mbalimbali kama insha, ushairi, tamthiliya na hadithi.
Aina Za Utungaji
Kuna aina mbili za utungaji. Nazo ni
- Utungaji wa mazungumzo
- Utungaji wa maandishi
Katika mada hii, tutajikita zaidi katika utungaji wa kuandika.
Uandishi Wa Barua
Jinsi Ya Kuandika Barua Ya Kirafiki
Barua za kirafiki pia huitwa za kidugu. Huandikwa baina ya watu wa undugu au jamii moja.
Barua za kirafiki kwa ndugu
Barua hizi zaweza kuandikwa kwa watu kama baba, mama, shangazi, mume, mke, mtoto, na kadhalika.
Barua za kirafiki katika jamii
Katika jamii, waandikiwao barua za kirafiki ni kama jirani, rafiki, mpenzi, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mgonjwa, na kadhalika.
Muundo wa barua za kirafiki
Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa barua za kirafiki ni haya
- ANWANI kamili ya mwandishi, katika herufi. Hukaa juu upande wa kulia mwa karatasi.
- TAREHE. Huandikwa chini ya anwani.
- MTAJO wa heshima kwa anayeandikiwa, kama vile mpendwa, mpenzi, na kadhalika. Huandikwa kushoto, baada ya tarehe.
- UTANGULIZI wa barua yenyewe. Kwa desturi huwa ni salamu.
- BARUA YENYEWE. Ndiyo kiini cha waraka.
- SALAMU za kumalizia, pengine kwa jamaa na jamii.
- HITIMISHO, katika aya maalumu. Kwa mfano: "Ni mimi baba yako akupendaye," na kadhalika.
- SAHIHI. Si sharti wala muhimu sana.
- JINA au MAJINA ya mwandishi, mwishoni.
Mfano wa barua ya kirafiki
SHULE YA SEKONDARI SAMATA,
S.L.P 700,
DAR ES SALAAM.
09/07/2018.
Mpendwa rafiki,
Habari yako. Natumaini unaendelea vyema huko nyumbani Makete. Mimi pia ni mzima wa afya.
Dhumuni la kukuandikia barua hii ni kutaka kukufahamisha juu ya maandalizi yangu ya mtihani wa kidato cha nne. Ninakwenda kuufanya ifikapo tarehe tano Novemba.
Nimejiandaa vyema katika masomo yote na ninatumaini nitafaulu vyema. Pia, nimepitia mitihani yote ya taifa iliyopita na nimeona jinsi maswali yanavyotoka.
Mbali na hayo, nimekuwa nikijipima kwa kufanya mitihani mbalimbali. Matokeo yangu ni mazuri sana.
Basi rafiki, naomba nikutakie kila la heri katika maisha yako hapo Makete. Nisalimie wote wanaonifahamu.
Rafiki yako,
Kijoto Bohari.
Jinsi Ya Kuandika Barua Ya Maombi Ya Kazi
Barua ya maombi ya kazi huandikwa kwa malengo ya kuomba kazi.
Kujifunza namna sahihi ya kuandika barua hii hakutakusaidia katika kujibu maswali pekee. Ujuzi huu utakufanya upate kazi halisi wakati utakapohitaji kufanya hivyo.
Mwandishi anasema: Nakumbuka niliwahi kuitwa kufanya kazi katika kampuni ya Global Publishers kwa sababu tu niliandika vyema barua yangu ya maombi ya kazi.
Muundo Wa Barua Ya Maombi Ya Kazi
- Anuani ya mwandishi. Yaani anuani yako wewe unayeandika barua hiyo.
- Tarehe.
- Anuani ya anayeandikiwa.
- Salamu.
- Kichwa cha habari.
- Kiini cha barua.
- Mwisho wa barua.
Kiini cha barua
Hii ni roho ya barua yako. Ukikosea mahali hapa, kama unajibu swali katika mtihani, utapoteza alama. Na kama unaomba kazi halisi, utaikosa.
Kiini kina aya nne
- Aya ya kwanza: Eleza kazi unayoomba na mahali ulipoona tangazo la kazi hiyo. Ni katika sehemu hii unaweza kutaja umri wako.
- Aya ya pili: Eleza ujuzi wako kwa ufupi. Usieleze sana. Barua hii haipaswi kuwa ndefu kupindukia.
- Aya ya tatu: Eleza kwa nini upewe kazi hii wewe na si mtu mwingine. Epuka kueleza shida zako binafsi ili upewe kazi. Maneno kama "ninaomba kazi hii ili niweze kumtibia mama yangu mgonjwa kitandani" hayana msaada.
- Aya ya nne: Eleza uko tayari kwa usahili siku gani.
Mwisho wa barua
Mwisho wa barua yako uwe na
- Neno la kufungia. Mfano: Wako mtiifu, au Wako katika ujenzi wa taifa, na kadhalika.
- Sahihi yako.
- Jina lako.
Ni rahisi sana kuandika barua ya maombi ya kazi. Tazama mfano wa barua hii
MTAA WA KIGOGO,
S.L.P 560,
DAR ES SALAAM.
18/10/2017.
MKUU WA SHULE,
SHULE YA SEKONDARI SAMAKI BEACH,
S.L.P 21494,
DAR ES SALAAM.
Ndugu,
Yah: Maombi Ya Kazi Ya Ualimu
Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 24. Najitokeza kuomba kazi ya ualimu katika shule yako. Kazi hiyo ilitangazwa katika gazeti la Raia Mwema siku ya Alhamisi tarehe 23-10-2017.
Nimehitimu shahada yangu ya ualimu kwa masomo ya Historia na Kiswahili mwaka 2016. Pia nimefanya kazi ya kufundisha kwa miezi saba katika shule ya wasichana Kandambili iliyoko Mbagala. Mbali na hayo, nina uwezo mkubwa wa kutumia kompyuta.
Uzoefu wangu wa kazi na uwezo mkubwa wa kufundisha nilionao unanishawishi niamini kuwa ninafaa kufanya kazi katika shule yako.
Ninategemea majibu mazuri kutoka kwako. Pia, nipo tayari kwa usahili siku yoyote nitakayohitajika. Nimeambatanisha nakala ya vyeti vyangu.
Wako mtiifu,
Sahihi
Kilaza Pondaponda
Barua Ya Kiofisi
Barua ya kiofisi huandikwa kwa masuala ya kiofisi. Ufuatao ni mfano wa barua ya kiofisi.
SHULE YA SEKONDARI MWENDAKOMBO,
S.L.P 789,
DAR ES SALAAM.
14/08/2018.
MKUU WA SHULE,
SHULE YA SEKONDARI MWENDAKOMBO,
S.L.P 789,
DAR ES SALAAM.
Ndugu,
Yah: Maombi Ya Ruhusa
Husika na kichwa cha barua hapo juu. Mimi ni mwanafunzi wa kidato cha nne A. Ninaomba ruhusa ya siku tatu kwa sababu ninauguliwa na bibi yangu na mimi ndiye ninayeweza kumuuguza.
Ninaahidi kuwa sitazidisha kiasi cha siku hizo tatu endapo nitapewa ruhusa.
Wako mtiifu,
Sahihi
Suzana Majabala
Jinsi Ya Kuandika Kadi Ya Mwaliko
Kadi ya mwaliko huandikwa kwa lengo la kualika watu kuhudhuria katika sherehe fulani.
Mambo muhimu katika kadi ya mwaliko
- Jina la mhusika wa sherehe
- Jina la anayealikwa
- Madhumuni ya kumwalika
- Tarehe ya mwaliko
- Mahali pa kukutana
- Mahali pa kupeleka majibu kwa wasiofika
Sasa tazama mfano huu kutoka swali la NECTA la mwaka 2009
Swali: Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwako, unahitaji marafiki kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo. Andaa kadi ya mwaliko ili kuwapa taarifa rafiki zako.
Mfano wa kadi ya mwaliko
Mimi SUMAKU KOMBO ninayo furaha kukualika Bwana KITALULA KALINGA kwenye sherehe yangu ya kuzaliwa. Sherehe itafanyika siku ya tarehe 16/07/2017 saa 12.00 jioni katika ukumbi wa Godsaria Hall, Kimara.
Tafadhali fika na kadi hii.
Majibu kwa wasiofika
Secilia Kilongo,
S.L.P 123,
Dar es Salaam.
Simu: 0754 89 53 21.
Barua Za Magazetini
Barua hizi huandikwa na wasomaji wa magazeti kwa mhariri. Mhariri huzisoma na kuzichapa katika baadhi ya kurasa za gazeti lake.
Barua hizi huwa na dhumuni moja kuu, nalo ni kufichua maovu. Hata hivyo, dhumuni jingine laweza kuwa kupongeza.
Muundo wa barua za magazetini
- Kichwa cha barua
- Mwanzo wa barua
- Barua yenyewe
- Mwisho wa barua
- Jina la mwandishi, anuani yake na tarehe
Sasa tutazame mfano wa barua iliyoandikwa na msomaji wa gazeti akiwapongeza vijana wa mtaa wake.
Hongera Vijana Wa Kigogo
Mhariri,
Mwananchi.
Natoa pongezi kwa vijana wa Kigogo kwa maamuzi safi waliyofanya ambayo yanachochea maendeleo. Maamuzi yao haya ni sahihi. Yanastahili kupongezwa na yeyote apendaye maendeleo.
Mwisho Wa Barua Ya Kupongeza Vijana Wa Kigogo
Vijana hawa ninawapongeza kwa sababu wameamua kuacha kuvuta bangi na kutumia aina zingine za madawa ya kulevya kama unga na mirungi.
Badala yake, wanajihusisha na ufugaji wa kuku wa kisasa, tena kwa mbinu za kisasa.
Pia, ili kulinda amani ya mtaa, wameamua kuanzisha mfumo wa sungusungu. Sasa Kigogo inalindwa na vijana! Hakuna tena tishio la wizi uliokuwa umekithiri miaka kadhaa nyuma. Hakika vijana wa Kigogo wamefanya maamuzi sahihi.
Jambo jingine ninalowasifia vijana wa Kigogo ni kwamba wanahamasishana kuweka fedha zao benki. Hii itawasaidia kutunza fedha kiduchu wazipatazo kwa jasho lao. Baada ya muda, fedha hizo zitageuka mtaji wa biashara zitakazowatoa kimaisha.
Ninawahamasisha vijana wa mitaa mingine kama Sogodo, Kwa Tumbo na maeneo mengine yote nchini Tanzania waige mfano wa vijana wa Kigogo. Endapo haya yatafanyika, nchi yetu Tanzania itapata maendeleo.
Mwalimu Makoba,
S.L.P 45,
Kinondoni.
Barua Ya Simu
Mfano wa barua ya simu
Barua ya simu ilitumika hapo zamani kabla ya majilio ya simu hizi tulizonazo. Kwa sasa hakuna tena barua ya simu. Hata hivyo, ni vyema kusoma jambo hili ili kujua vyema historia ya mambo.
Jambo kubwa la kuzingatia ni kwamba barua hii hutakiwa kuwa chini ya maneno 10. Ilifanyika hivyo kwa lengo la kupunguza gharama.
Unapoandika barua ya simu, fanya hivi
- Anza na anuani ya unayemtumia barua.
- Weka ujumbe.
- Maliza kwa kuweka jina lako.
Tazama mfano huu wa barua ya simu
Slp 235 Dar Es Salaam Tuma Hela Mama Mgonjwa James
Uandishi Wa Matangazo Ya Biashara Magazetini
Matangazo ya gazetini huandikwa kwa lengo la kutangaza biashara.
Magazeti yana wasomaji lukuki. Kwa hiyo njia hii hudhaniwa kuwa miongoni mwa njia rahisi zaidi za kuwafikia watu wengi. Watu hao hapo baadaye hugeuka wanunuzi wa bidhaa inayotangazwa.
Uandishi mzuri zaidi wa matangazo ndiyo utakaofanya bidhaa yako inunuliwe. Uandishi mbovu hugeuka kero kwa watu.
Mambo muhimu ya kuzingatia
- Kichwa cha habari. Kiandikwe kwa herufi kubwa.
- Taja aina ya biashara.
- Taja bidhaa unazouza na bei zake.
- Taja mahali inapopatikana bidhaa yako.
- Taja mawasiliano yako. Mawasiliano yanaweza kuwa ya simu, barua n.k. Hata hivyo, simu ni bora zaidi, kwa sababu mawasiliano yake ni ya haraka.
Mfano wa tangazo
Tunauza Nafaka Zote
Tunauza nafaka aina zote kama mchele, maharage na mahindi. Bei zetu ni nafuu na uhakika.
Duka letu linapatikana Kinondoni Manyanya, mkabala na shule ya sekondari Kambangwa.
Mawasiliano
0754 89 53 21
0653 25 05 66
Jinsi Ya Kuandika Hotuba
Hotuba ni maelezo ambayo hutolewa na mtu mbele ya watu kuhusu mada fulani.
Muundo wa hotuba
- Mwanzo. Huu huambatana na salamu.
- Utangulizi. Hutaja watu na kuwatambulisha kulingana na vyeo vyao.
- Kati. Hiki ni kiini cha hotuba. Mawazo yote makuu hukaa hapa.
- Mwisho. Ni muhtasari wa yale yaliyoelezwa. Pia, msemaji hupata nafasi ya kuaga na kushukuru.
Sasa tazama mfano halisi wa hotuba. Umeandikwa kama jibu la swali la nane la mtihani wa kumaliza kidato cha nne 2010.
Swali: Eleza tofauti iliyopo kati ya hotuba na risala. Andika hotuba kuhusu "Maji ni Uhai."
Kwa kuwa mjadala wetu ni hotuba, risala haitazungumziwa. Badala yake, nitajikita katika kuonyesha mfano wa hotuba.
Maji Ni Uhai
Wanakijiji oyeeeeeeh!
Ndugu Mwenyekiti wa Kijiji, ndugu Katibu wa Kijiji, ndugu wanakijiji wote, mabibi na mabwana.
Ninafurahi kusimama mbele yenu na kuzungumza. Nikiwa mwanaharakati wa muda mrefu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, leo nasimama tena kuwaeleza na kuuthibitishia umma huu kuwa maji ni uhai.
Asilimia sabini ya miili yetu ni maji. Hivyo bila maji mwanadamu hawezi kuishi hata kwa mwaka mmoja. Sisi ni maji, kwa hiyo lazima tuishi kwa tahadhari kubwa ili kuyanusuru maji haya yasipotee tukaadhirika.
Laiti tungepata nafasi ya kutembelea watu waishio jangwani, tukawaona jinsi wanavyopata shida ya maji, tungejifunza kitu. Kuna visa kadhaa vimekuwa vikiripotiwa katika vyombo vya habari kuhusu watu na wanyama waliokufa kwa ukosefu wa maji.
Ukiachilia mbali matumizi yetu, hata viumbe wengine kama mamba, samaki, viboko na pweza wanategemea maji hayahaya ili waendelee kuishi. Ndugu zangu, lazima sasa tukubaliane kuwa maji ni uhai.
Ni kipi kisichohitaji maji? Hata viwanda tunavyovitegemea kwa uzalishaji wa bidhaa haviwezi kufanya kazi bila maji ya kupozea mitambo yake.
Mwaka jana nikiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kijiji hiki, tulikumbwa na kasheshe ya kuharibikiwa na injini ya gari letu. Tulipochunguza, tukagundua ilichemka kupita kiasi kwa kukosa maji!
Wanyama na mimea tunaowategemea kwa chakula ili tuendelee kuishi wanategemea maji. Kilimo bila maji hakuna kitu. Bila maji wote tutakwisha na kusahaulika mara moja.
Niwaombe ndugu zangu, tuiache mara moja tabia mpya iliyozuka. Tabia ya kunywesha mifugo katika vyanzo vya maji itatuletea balaa.
Pia, kuna mkasa mwingine wa watu kukata miti hovyo. Hatukatazi kukata miti. Lakini hakikisha unapokata mti una kibali maalumu, na pia, kata mti panda mti. Vijana wa siku hizi wamebadili msemo huu. Wanasema panda mti ndipo ukate mti! Nawaunga mkono.
Ni matumaini yangu makubwa kwamba mtayafanyia kazi yote niliyoyasema. Msingi zaidi, tuhakikishe tunaepuka tabia zote ambazo zitatuharibia vyanzo vyetu vya maji.
Mwisho, niwashukuru wote kwa kunisikiliza. Nasema asanteni sana.
Jinsi Ya Kuandika Risala
Risala ni hotuba fupi iliyo katika maandishi. Husomwa mbele ya mgeni rasmi ikielezea kuhusu mafanikio, changamoto na maombi ya kundi fulani.
Muundo Wa Risala
Utungaji: Risala Na Insha
Muundo Wa Risala
Risala ina vipengele vitatu: utangulizi, kiini na hitimisho.
Utangulizi
Katika kipengele hiki, cheo cha kiongozi (mgeni rasmi) hutajwa.
Pia kundi linalowakilishwa hutajwa.
Kiini
Kiini kina mambo haya
- Mafanikio ya kundi
- Changamoto za kundi
- Mapendekezo na ushauri
Hitimisho
Kipengele hiki hukaa shukrani.
Sasa hebu tazama mfano huu wa risala.
Mfano Wa Risala
Swali
Jifanye wewe ni mwanafunzi wa kidato cha nne na umechaguliwa kuandaa risala itakayosomwa mbele ya mgeni rasmi siku ya mahafali yako ya kumaliza kidato cha nne. Andika risala utakayoisoma siku hiyo.
Jibu
Risala Ya Shule Kwa Mgeni Rasmi Kwenye Mahafali Ya 11 Ya Kidato Cha Nne, Octoba 3, 2018
Ndugu mgeni rasmi, waalimu, wazazi, wanafunzi wenzetu, wageni waalikwa, mabibi na mabwana.
Ndugu mgeni rasmi, tuna furaha kukualika leo katika sherehe yetu ya mahafali haya ya kidato cha nne. Tunataka usherehekee pamoja nasi. Pia tunataka usikie mafanikio yetu pamoja na changamoto zinazotukabili.
Ndugu mgeni rasmi, awali ya yote tunapenda kutoa shukrani kwa uongozi mzima wa shule yetu. Wamekuwa wazazi bora. Wametuongoza katika misingi imara ambayo itatusaidia sana hata baada ya kumaliza elimu yetu.
Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 60. Kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo maradhi, utoro na ukosefu wa fedha, tumebaki wanafunzi 40. Wavulana ni 15 na wasichana ni 25.
Ndugu mgeni rasmi, miongoni mwa mafanikio tuliyonayo katika shule yetu ni umiliki wa mradi wa miti ya matunda. Mradi huu umetusaidia sana sisi wanafunzi. Tunapata matunda katika kila mlo tunaokula, na hivyo tuna afya bora.
Ndugu mgeni rasmi, mafanikio mengine ni uwezo wetu mkubwa kitaaluma. Ni kweli kuwa uwepo wa waalimu bora ndiyo sababu ya shule yetu kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yote ya kujipima tunayofanya na shule za mkoa wetu.
Ukiachilia mbali kuwa wa kwanza, tumepata maarifa stahiki ambayo tulipaswa kuwa nayo. Tunatumaini yatatusaidia sana katika kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii yetu.
Ndugu mgeni rasmi, mbali na mafanikio hayo, kuna changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikitusumbua.
Changamoto ya kwanza ni ukosefu wa vitabu vya kutosha. Tatizo hili limetufanya tusome kwa shida, kwani kitabu kimoja kinachangiwa na wanafunzi saba.
Ndugu mgeni rasmi, tatizo jingine ni uhaba wa vifaa vya maabara. Uhaba huu unasababisha wanafunzi wengi kushindwa kusoma sayansi kwa vitendo. Badala yake tunaisoma kwa nadharia tu.
Ndugu mgeni rasmi, tunatumaini umesikia mafanikio yetu na changamoto zetu. Tunatumaini utatusaidia kadri ya uwezo wako ili shule yetu iendelee kuwa sehemu salama ya kujipatia elimu.
Pia tunakushukuru kwa kufika mahali hapa. Ulikuwa na shughuli zako muhimu, lakini umeweza kupata muda wa kujumuika nasi.
Asante na karibu sana.
Jinsi Ya Kuandika Insha
Insha ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumziwa au kuandikwa.
Urefu au ufupi wa insha hutegemea mada husika inayojadiliwa.
Muundo wa Insha
Insha bora inatakiwa iwe na mambo haya
- Kichwa cha insha
- Mwanzo wa insha
- Kiini cha insha
- Mwisho wa insha
Aina za insha
Zipo aina tatu za insha
- Insha za wasifu
- Insha za hoja
- Insha za kisanaa
Katika kipengele hiki hatutajadili aina za insha. Tutatazama namna ya kuandika insha kwa ujumla.
Baada ya kutazama mambo hayo, sasa soma mfano huu wa insha iliyoandikwa.
Mfano Wa Insha
Swali la nane, mtihani wa NECTA mwaka 2009
Andika insha yenye maneno 250 kuhusu moja ya mada zifuatazo
(a) Aisifuye mvua imemnyeshea.
(b) Elimu ya msingi ina umuhimu wake katika jamii.
(c) Maradhi yanavyorudisha nyuma maendeleo ya familia hatimaye Taifa.
(d) Kuelimika kwa msichana ni kuelimika kwa jamii.
(e) Wanyama pori.
Katika swali hilo, ni vyema mwanafunzi atulize kichwa. Achague swali ambalo ana uhakika ataweza kulijibu vyema ikilinganishwa na maswali mengine.
Kama ningekuwa mimi ninafanya mtihani huo, ningechagua swali (b). Ningeandika kama inavyooneshwa hapa:
Elimu Ya Msingi Ina Umuhimu Wake Katika Jamii
Elimu ya msingi ni elimu inayotolewa kwa mtu ili kumwandaa kukabiliana vyema na jamii yake.
Mara nyingi elimu ya msingi hutolewa kwa watoto wadogo. Hata hivyo, si mara zote. Zipo hali ambapo watu wazima hupatiwa elimu hiyo ambayo waliikosa walipokuwa watoto.
Elimu ya msingi ni muhimu katika jamii kama inavyoelezwa hapa chini.
Kufundisha kusoma, kuandika na kuhesabu
Elimu ya msingi huwafundisha wanafunzi kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mwanafunzi anayeyaelewa mambo haya matatu huwa na uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii yake.
Mtu asiyejua kusoma huhesabiwa kuwa mjinga.
Kuwaandaa wanafunzi kuitumikia jamii
Elimu ya msingi huwaandaa wanafunzi kuitumikia jamii yao.
Yapo mengi yanayofundishwa. Miongoni mwayo ni kilimo na stadi za kazi. Mambo haya hugeuka msaada mkubwa hata mwanafunzi anapomaliza masomo yake.
Kuandaa wanafunzi wa sekondari
Elimu ya msingi hutumika kuandaa wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari.
Wanafunzi wanaofaulu darasa la saba huchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari ili kupata maarifa ya juu zaidi.
Kuandaa wanafunzi wa vyuo vya ufundi
Elimu ya msingi huandaa watu watakaojiunga na vyuo mbalimbali vya ufundi, kama VETA na vinginevyo.
Wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na elimu ya sekondari hujiunga na vyuo vya ufundi ili kujipatia ujuzi.
Kufundisha historia na tamaduni za Kiafrika
Elimu ya msingi hufundisha historia na tamaduni za Kiafrika.
Urithishaji huu wa amali za jamii una umuhimu mkubwa, hasa katika zama hizi. Jamii yetu imevamiwa na wimbi kubwa la ongezeko la tamaduni kutoka Ulaya na Asia.
Kuandaa wananchi wa kulitumikia taifa
Elimu ya msingi huandaa wananchi watakaolitumikia taifa lao.
Taifa linahitaji watu walio tayari kufuata sheria na kanuni zilizowekwa. Hii ni ili kuhakikisha usalama na kusaidia maendeleo ya nchi.
Hitimisho
Elimu ya msingi ina umuhimu mkubwa katika jamii.
Serikali na jamii kwa ujumla zinatakiwa ziboreshe mazingira ya utoaji wa elimu hii.
Jinsi Ya Kuandika Kumbukumbu Za Kikao
Unapoandika kumbukumbu za kikao, hakikisha unazingatia mambo manne. Hayo ndiyo sehemu za kumbukumbu za kikao:
- Kichwa cha habari
- Waliohudhuria
- Wasiohudhuria
- Ajenda
Ajenda imegawanyika katika mambo manne
- Kufungua kikao
- Maandalizi
- Mengineyo
- Kufunga kikao
Mfano Kutoka Swali La Necta Mwaka 2011
Swali
Andika kumbukumbu za kikao cha wanafunzi kuhusu sherehe ya kumuaga mkuu wenu wa shule aliyepata wadhifa wa kuwa Afisa Elimu wa Mkoa.
Jibu
MUHTASARI WA KIKAO CHA KAMATI YA WANAFUNZI KUANDAA SHEREHE YA KUMUAGA MKUU WA SHULE KILICHOFANYIKA 24/06/2011 KATIKA UKUMBI WA SHULE KUANZIA SAA 5.00 ASUBUHI MPAKA 7.00 MCHANA.
- WALIOHUDHURIA (wawakilishi wa madarasa)
- Beatrice Ngonyani IA
- Stella Oswald IIA
- Mkolosai Emsii IIIB
- Ahmed Juma IV B
- Manwa Kigoma (Mwenyekiti)
- Rashid Abubakar (Katibu)
- WASIOHUDHURIA
- BALQIS KOROFI (bila taarifa)
- LUJJAYNA MWEUPE (kasafiri)
- AJENDA
- Kufungua kikao
- Maandalizi
- Mengineyo
- Kufunga kikao
- Kufungua kikao:
Mwenyekiti alifungua kikao mnamo saa tano. Aliwakaribisha wajumbe na kuwaomba wawe huru kuchangia katika kikao hicho.
- Maandalizi:
Ili kufanikisha sherehe hiyo, wajumbe waliamua kuchagua kamati ndogo ambayo ingesaidia kufanikisha sherehe.
Wajumbe wa kamati waliochaguliwa ni
- Beatrice Ngonyani IA
- Stella Oswald IIA
- Mkolosai Emsii IIIB
- Ahmed Juma IV B
- MENGINEYO:
Wajumbe walikubaliana kuchangia kiasi cha shilingi 1,000/= ili kumnunulia zawadi mkuu wa shule.
Pia, walikubaliana kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi katika sherehe ya kumuaga mkuu wa shule.
- KUFUNGA KIKAO:
Mwenyekiti alifunga kikao kwa kuwaomba wajumbe wawafikishie taarifa wanafunzi wote kuhusu yaliyokubaliwa katika kikao. Pia aliwaomba watoe ushirikiano ili kufanikisha sherehe.
Kikao kilifungwa saa 7.00 mchana.
Sahihi: ............................
Manwa Kigoma (Mwenyekiti)
Tarehe 24/06/2011
Sahihi: ..................................
Rashid Abubakar (Katibu)
Tarehe 24/06/2011
