Maendeleo ya fasihi simulizi
Dakika 25 za kusoma ·
Yaliyomo
Uwasilishaji Na Uenezaji Wa Kazi Za Fasihi Simulizi
Fasihi Simulizi:
Fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe fulani kwa watazamaji au wasikilizaji.
Mazungumzo hayo huweza kuwa ya kuimbwa, kutendwa au kuzungumzwa.
Aina hii ya fasihi imepokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo.
Msimulizi katika fasihi simulizi hutumia mdomo wake. Mbali na mdomo, hutumia pia viungo vya mwili kama mikono na miguu. Hutumia ishara mbalimbali katika uso wake na hata kupandisha na kushusha sauti yake.
Kwa ujumla, anaweza kutumia mwili wake mzima katika kuwasilisha na kufanikisha ujumbe wake kwa hadhira yake. Hadhira hiyo huwa ana kwa ana naye.
Isitoshe, anafaulu kutoa picha halisi ya dhana anayotaka kuiwasilisha, kama ni ya huzuni, furaha, kuchekesha n.k.
Zaidi ya kusimulia, kuimba na kuigiza, msanii wa fasihi simulizi ana nafasi ya kushirikisha hadhira yake kama wahusika katika sanaa yake.
Anaweza kutimiza hayo kwa kumfanya mshiriki mmoja kuigiza jambo fulani. Anaweza pia kufanya hadhira yote iimbe au ifanye matendo mbalimbali.
Ufundi wa aina hii huhitaji umahiri wa hali ya juu. Hali hii humpa msanii wahakiki wake hapohapo.
Kwa upande mwingine, hadhira nayo ina nafasi na uhuru wa kushiriki au kuuliza maswali pale ambapo haikuelewa. Vilevile hupata fursa ya kuonyesha hisia zake, kuhimiza na kukumbushana. Kwa hali hiyo, fasihi simulizi ina uwezo wa kufundisha zaidi.
Kwa kuzingatia maoni ya Kirumbi (1976) na maelezo yaliyotangulia, tunakubaliana naye kwamba fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika uwasilishaji wa ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira.
Mazungumzo hayo huwa katika mfumo wa masimulizi, kuimbwa, kutambwa, kughaniwa na kutongolewa.
Fasihi simulizi hueleza jamii kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Huzungumzia mambo yanayozunguka jamii husika.
Fasihi simulizi huathiri malezi ya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo na matendo.
Fasihi simulizi huenda sambamba na mabadiliko ya jamii. Kwa hiyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia mabadiliko ya mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Fasihi simulizi ni utanzu wa kisanaa ulio hai. Hukua na kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na ya mifumo ya jamii.
Hivyo, fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha (mazingira) fulani ya jamii. Muktadha huo hutawaliwa na mwingiliano wa mambo yafuatayo:
Vipengele Vya Muktadha Wa Fasihi Simulizi
- Msimulizi (fanani):
Huyu ni mtu anayetamba hadithi, kuimba wimbo, kutoa methali au vitendawili.
- Wasikilizaji au watazamaji (hadhira):
Hawa ni washiriki katika kutazama au kusikiliza fani za fasihi simulizi. Mara nyingine hutumiwa na fanani kama wahusika wa fani yake.
- Mahali (mandhari):
Hapa ni jukwaa au mahali ambapo tukio la fasihi simulizi linatendeka. Mahali hapo panaweza kuwa nyumbani, uwanjani n.k.
- Tukio:
Ni shughuli ya kijamii ambayo ndiyo muktadha wa utendaji wa sanaa. Mifano ni harusi, kazi fulani, sherehe, msiba, ibada n.k.
Utendaji huo waweza kuwa usimulizi wa hadithi, kutega vitendawili, kuimba wimbo au nyimbo, au kutoa methali.
- Wakati:
Ni muda maalumu wa kihistoria au majira maalumu ya utendaji huo.
Uhifadhi Wa Kazi Za Fasihi Simulizi
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa kwenye maandishi na kanda za sauti kwa madhumuni ya kumbukumbu.
Tunaweza kutambua fasihi simulizi kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo
- Kama ilivyoelezwa hapo awali, inategemea mdomo wa msimulizi (mtendaji) na masikio ya hadhira.
- Fasihi simulizi ni hai kwa sababu inategemea uhusiano wa ana kwa ana wa msimulizi (mtendaji) na hadhira yake. Kwa hiyo lazima uwepo utendaji wa maneno, wa muziki au wa matendo utakaowasilisha tungo za mtendaji kwa hadhira yake. Utendaji huu hutegemea sana kiimbo, shadda, milio na vihisishi.
- Fasihi simulizi inatendwa, hivyo lazima iwe na mtendaji. Huyu anaweza kuwa mwimbaji, msemaji au mtendaji. Kazi yake ni kuanzisha au kueneza tungo, au kazi zote mbili. Mtendaji huyu hutumia vifaa vya kusikika au kuonekana katika kujieleza, kwa mfano wimbo na toni za miondoko. Kwa njia hii anakuwa karibu sana na hadhira yake.
- Kila mtu anaweza kufuatilia kwa kiasi fulani, na fasihi simulizi inategemea kumbukumbu za mtu binafsi. Hadhira inapotumia na kueneza tungo za fanani, huimba, hufanya usanii na kuzijenga tungo hizo kwa namna zake. Jambo hili hufanya kazi ya fasihi ielezwe kwa namna kadha kutegemea mazingira na masimulizi.
- Kukabiliana na hadhira moja kwa moja kuna athari katika tungo za fasihi simulizi. Fanani huweza kubadilisha tungo katika utendaji wake kadri apendavyo. Lengo ni kukuza uzuri wa kazi yake au kuleta athari fulani inayokidhi haja ya wakati ule.
- Mwambatano wa tungo na mazingira maalumu ni muhimu. Mazingira huathiri sana usanii wa tungo na maudhui yake. Zipo tungo zinazoambatana na matukio maalumu. Hata kama zimepitwa na wakati, huweza kugeuzwa zikasadifu kipindi mahususi.
Fasihi simulizi ina tabia ya uhai. Hutegemeana na sanaa za maonyesho na ghibu, yaani sanaa ya muziki. Tabia hii inaitwa hali ya utegemezi.
Hii ni kwa sababu fasihi simulizi huchota uhai wake kutokana na vitendo na vitabia vya fanani, mahadhi, toni za muziki na vipengele vingine vya sanaa za maonyesho.
Bila kuzingatia vipengele hivi vya utendaji, kazi ya fasihi simulizi inaweza kuchapwa. Kwa mfano, wimbo unaweza kukosa uhai wake bila mahadhi, madoido, upigaji ngoma, miondoko ya uchezaji na mazingira ya tukio unamotumiwa.
Tanzu Za Fasihi Simulizi
Kuna makundi mawili muhimu ya tanzu za fasihi simulizi
- Kundi la tanzu zenye mwelekeo wa kishairi.
- Kundi la tanzu za kinathari, au zenye sifa za kihadithi.
Tanzu za kishairi zina sifa nyingi za ushairi kuliko tanzu zenye lugha ya kinathari.
Ushairi aghalabu hutumia lugha ya kitamathali na mkato. Pia ushairi una mizani, ulinganifu wa sauti na mapigo.
Matteru (1987) amesema kwamba katika muktadha wa fasihi simulizi, kuna tanzu zinazotumia mapigo kwa utaratibu maalumu. Mapigo haya yanaweza kuwa ya muziki au yoyote yale yaliyopangwa kwa muwala wa uwazi.
Tanzu kama nyimbo, maghani, methali, vitendawili na misimu hupatikana katika kundi hili la ushairi.
Kwa upande mwingine, Matteru (1987) anasema kwamba tanzu za kinathari zinajumlisha tungo zote za fasihi simulizi zenye kutumia lugha ya kawaida.
Matteru anamalizia kwa kusema kuwa "nathari" hujumlisha tanzu na fani kama hadithi, ngano, tarihi, visasili, vigano na masimulizi.
Masimulizi / Hadithi
Tanzu mbalimbali za hadithi zinaingia hapa, kwa mfano ngano, hekaya n.k.
Pia kuna simulio la kihistoria na la kiasili, kama vile
- Visakale: masimulizi ya kimapokeo, ya wahenga au ya mashujaa.
- Kumbukumbu.
- Visasili: hadithi za zamani zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii.
Hadithi au masimulizi hutumia lugha ya mjazo au nathari. Mtiririko wake huwa mwepesi na sahihi.
Zipo hadithi za kubuni na za kihistoria.
Umuhimu Wa Hadithi Katika Fasihi Simulizi
- Hutumiwa kuipa jamii mwelekeo.
Simulizi au hadithi hufumbata mtazamo wa jamii pamoja na falsafa yake nzima. Ndiyo kielezi cha jamii husika.
- Hutumiwa kuyaendeleza maadili ambayo huwa kama nguzo kuu ya wanajamii.
Kila hadithi huwa na funzo maalum.
- Huonya, huadhibu, huelimisha, huishauri na kuinasihi jamii kupitia wasifu wa wahusika.
- Hutumika kuirithisha jamii elimu, thamani na amali muhimu kutoka kizazi hadi kizazi.
Tanzu za fasihi simulizi huwa nyenzo kuu ya kurithisha elimu ya jadi katika jamii husika.
- Hutumiwa kama burudani.
- Hutumiwa kuendeleza uhusiano uliopo kati ya wanajamii.
Hasa ni uhusiano wa kushirikiana, tofauti na usomaji wa vitabu.
- Hukuza uwezo wa watoto kuyakumbuka mambo.
Huboresha uwezo wao wa kumbukumbu n.k.
Kuhakiki Kazi Za Fasihi Simulizi
Sifa kuu za kimtindo zinazotumika katika uhakiki wa hadithi au simulizi ni hizi
- DHAMIRA NA MAUDHUI
Ndani ya dhamira tunapaswa kulitambua wazo kuu au lengo kuu la hadithi.
Maudhui ni jumla ya mambo yaliyomo ndani ya hadithi hiyo. Mambo hayo huibuka katika kuliendeleza wazo hilo kuu.
- MSUKO
Huu ni muundo wa hadithi yenyewe.
Hapa tunaangalia jinsi matukio ya hadithi yalivyopangwa. Huanza mwanzo kwenye kitangulizi.
Tunaangalia pia mvuto wa hadithi, ambao ni mgogoro kati ya wahusika waliopo.
Kisha tunaangalia kuwepo kwa taharuki, na harakati zao hadi kwenye kilele cha hadithi (upeo), na hatimaye mwisho wake.
- USISIMUZI
Hapa tunachunguza uwezo wa hadithi wa kuiteka hadhira yake.
- URUDIAJI
Kwa kawaida urudiaji unaweza kuwa wa vipengele vya muundo. Mfano: virai, maneno, sentensi, vifungu fulani, nyimbo n.k.
Pia huwepo urudiaji wa mawazo, fikra, maoni n.k.
Sababu za urudiaji ni kufanya mambo yaliyozungumzwa yakumbukwe, au kusisitiza jambo fulani.
- MATUMIZI YA NYIMBO
Nyimbo hutumika kwa kiasi kikubwa katika hadithi. Hufanya kazi zifuatazo
- Kuonyesha au kusisitiza kiini au wazo kuu katika hadithi au simulizi inayohusika.
- Hushirikisha hadhira katika hadithi inayotambwa.
- Huongeza uhai wa usimulizi kwa kushirikisha hadhira.
- Huwapambanua wahusika mbalimbali wanaopatikana katika hadithi hiyo.
- Kuondoa ukinaifu unaotokana na kutumia mtindo wa aina moja kwa kipindi kirefu.
- Kuwazindua wasikilizaji ambao huenda wamelala au kusinzia wakati hadithi inatambwa.
- Hutumika kama kiliwazo katika hadithi za kitanzia.
- VILIWAZO / UCHESHI
Kiliwazo ni sehemu ya hadithi iliyokusudiwa kuituliza hadhira kidogo. Hasa katika hadithi zinazozungumzia masuala ya kusikitisha au ya kitanzia.
Kiliwazo kinaweza kuwa kifungu kilichojaa ucheshi. Kimekusudiwa kuondoa kwa muda hali ya kusikitisha.
Nyimbo hutumiwa pia kama kiliwazo.
- TAMATHALI ZA SEMI
Hadithi huwa na ufundi wa kisanaa. Ufundi huu hujitokeza kwa matumizi ya lugha yenye mvuto, iliyochanganya tamathali mbalimbali za semi.
Mfano: sitiari, tashibiha, tashititi, tashihisi, tafsida n.k.
- USIMULIZI – HAKIKI / TUNDUIZI
Mtambaji wa hadithi hutoa maoni kuhusu hadithi anayoisimulia.
Msimulizi anaweza kutoa maoni yake kuhusu wahusika wanaopatikana hadithini. Anaweza pia kutoa maoni kuhusu matukio fulani yaliyomo hadithini.
Kwa kiasi fulani maoni hayo huweza kuathiri usimulizi huu.
- WAHUSIKA
Kuna wahusika wa aina mbili katika hadithi
- Wahusika binadamu.
- Wahusika wanyama ambao wanapewa sifa za binadamu (mazimwi, majitu n.k.).
Katika usimulizi wa hadithi, mpaka kati ya ulimwengu wa kawaida wa binadamu na wanyama hufutwa.
Binadamu wanaweza kulingana, kujadiliana, kuzungumza na kuhusiana kwa jumla na wanyama.
Katika hadithi simulizi, wanyama wakubwa huweza kushindwa na wanyama wadogo. Hii ni namna ya kuwakejeli wasiotumia akili zao.
Viumbe wakubwa wanaodhaniwa kama mazimwi na majitu husawiriwa kama viumbe wanaoongozwa na tamaa kubwa, ulafi na uovu uliokithiri.
Hii ni njia mojawapo ya kuakisi sifa zinazoonekana mbaya katika jamii.
Aidha, kuna hadhira za aina mbili
- Hadhira tendi.
- Hadhira tuli.
Hadhira tendi hushiriki katika usimulizi wa hadithi. Mfano: katika nyimbo, kupiga makofi, kucheza, kuitikia, kubadilisha wasimuliaji, kuuliza na kujibu maswali.
Hadhira tuli haishiriki kwa namna yoyote ile. Husikiliza tu.
- TANAKALI SAUTI
Mtambaji katika utambaji wake huweza kutumia sauti zinazoeleza hisia au kuchora picha ya kutokea kwa jambo fulani.
Pia hutumiwa kutia utamu, mvuto na msisimko wa lugha ya mtambaji.
Mfano: "mara cheche akatwaa zumavi akapiga, kanga pia singizia moto, ti, ti, ti......., nikamtwaa nikamfungafunga na majani ya mgomba nikampiga pu, pu, pu,..."
- ISHARA NA TASWIRA
Ishara ni matumizi ya vitu fulani kuvisimamia vingine. Yaani huashiria vitu vingine tofauti.
Mfano: mti mkubwa kuashiria uhusiano uliopo kati ya watu na miungu katika jamii kadhaa.
Taswira ni matumizi ya lugha yanayomfanya msikilizaji au hadhira iweze kuunda picha akilini.
Mtumiaji anaweza kutumia picha au tamathali za semi, mfano sitiari, kuunda picha hizi.
- UTOKAJI KANDO
Utokaji kando ni mbinu ambayo mtambaji au msimulizi anatoka kando ya utambaji wake. Hutoa maoni kuhusiana na kitu kisichohusiana na hadithi moja kwa moja.
Kuna aina mbili za utokaji kando
- Utokaji kando wa nje: unatokana na sababu zilizo nje ya hadithi yenyewe, mfano kutokana na hadhira.
- Utokaji kando wa ndani: unasababishwa na nia ya kutoa maoni kuhusu tukio fulani au kitu fulani katika hadithi yenyewe. Hii inahusiana na usimulizi tunduizi.
Maigizo (Drama) – Sanaa Za Maonesho
Maigizo hutumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine. Lengo ni kuburudisha na kutoa ujumbe fulani.
Ni sanaa inayopatikana katika makabila.
Drama za Kiafrika huambatana na ngoma, utambaji, hadithi, nyimbo na matendo ya kimila (jando na unyago).
Kuna maigizo yanayofungamana na michezo ya watoto, matanga, uwindaji, kilimo n.k.
Maigizo Ya Watoto
Watoto wanapocheza hufanya maigizo ya matendo ya kimaisha wanayoyaona katika jamii zao. Mfano: kulima, kufanya biashara, harusi, matanga n.k.
Hizi ni sanaa za maonesho zenye kuwaburudisha na kuwaelimisha watoto. Pia hukuza vipaji vyao vya ubunifu.
Maigizo Ya Msibani
Katika baadhi ya makabila, watani au wajukuu wa marehemu hupaswa kufanya maigizo yanayohusiana na maisha, matendo au tabia za marehemu.
Hii huwapunguzia wafiwa huzuni yao. Pia hutoa mafunzo fulani kwa watu waliopo msibani.
Mfano: kwa tabia mbaya, maigizo hayo hupinga tabia mbaya.
Maigizo Ya Sherehe
Sherehe kuu za jamii ni kama hizi
- Kuzaliwa kwa mtoto.
- Mtoto kupewa jina.
- Jando na unyago.
- Harusi.
- Kubadilisha rika.
- Kuanua matanga.
- Sherehe za kisiasa, mfano kutawazwa kwa mtemi.
- Sherehe za kidini, mfano kuwakaribisha mwezi mwandamo.
- Na nyinginezo.
Kila sherehe huwa na sanaa zake za maonesho. Wakati mwingine sanaa hizo huambatana na maigizo.
Maigizo Ya Kidini
Maigizo haya hufanywa wakati wa ibada, matambiko na shughuli nyingine za kidini.
Katika maigizo ya aina hii, mzimu au miungu ndiyo hadhira ya igizo linalofanyika.
Uigizaji Katika Fasihi Simulizi
Uigizaji ni muhimu sana katika fasihi simulizi. Katika uigizaji, watendaji huiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kutoa ujumbe fulani.
Uigizaji huu unaweza kuwa na nia ya kukejeli, kudhihaki, kukosoa au hata kuburudisha.
Uigizaji hautegemei sauti tu. Pia hutumia maliba mahususi kama majusoo au barakoa (maski).
Pia kuna matendo yasiyoambatana na sauti, kama michezo bubu. Michezo hii inatilia mkazo mkubwa kwenye matendo.
Utambaji wa hadithi huwasilishwa kwa hadhira kwa utendaji wa kisimulizi au kitambaji. Mashairi ni uigizaji au dhana ya aina fulani.
Mviga ni sherehe za kiutamaduni na huweza kuhusisha matambiko. Miviga hufumbata maigizo ya aina fulani kutegemea sherehe inayohusika.
Vitanzu Au Vipera Vya Maigizo Au Drama
- Michezo ya jukwaani:
Hapa kuna mpangilio na mazungumzo baina ya watu pamoja na matendo yao.
Mazungumzo hayo hujenga kisa kinachoonesha mgogoro fulani.
Kuna michezo inayoambatana na sauti na isiyoambatana na sauti, kama vile ucheshi bubu, michezo bubu n.k.
Onyesho bubu: kimsingi, vitanzu hivi huhusisha utendaji unaotegemea ishara za mikono na sehemu nyingine za mwili bila maneno.
- Majigambo:
Haya ni maigizo yanayoonesha kujitapa (yaani kujigamba) kwingi kwa mtu ambaye labda ni shujaa au ametenda mambo ya kishujaa au yenye uzito fulani.
Wahusika wanaopatikana katika majigambo ndio watambaji au wasimuliaji wa majigambo yenyewe.
Ni kawaida ya majigambo kuwa na lugha nzito iliyojaa tamathali zenye taswira au picha za undani, na yenye nia na mawazo mazito.
- Vichekesho:
Vichekesho ni mpangilio wa maneno unaowasilisha ujumbe fulani maalum kwa njia ya kuchekesha au kufurahisha.
Kimuundo, vichekesho huwa vifupi. Havihitaji uchambuzi mpevu au wa ndani ili kupata maana nyingine ya ndani.
Lugha yake huweza kuwa nyepesi na iliyojaa picha ambazo watazamaji wana uwezo wa kuzitambua.
- Ngonjera au ushairi wa kimazungumzo:
Ngonjera ni mpangilio wa tungo za kishairi za kujibizana.
Ili ushairi huu uwe sehemu ya maigizo, lazima uambatane na utendaji. Yaani wanaohusika hutumia ishara za mikono, mwili, uso na nyingine ili kuwasilisha ujumbe wao.
Ikiwa ngonjera haziambatani na matendo au utendaji, haziwi tena sehemu ya maigizo bali sehemu ya ushairi.
Mshairi mmoja anaweza kutunga ubeti na kutenda matendo yanayoambatana na kiini cha ubeti wake.
Ngonjera huweza kutumiwa kuwatia watazamaji au hadhira hamasa ya kutenda jambo, au hata kuwasilisha maarifa fulani kwao.
- Mazungumzo:
Mazungumzo ni maongezi ya kimajibizano yanayotokea baina ya watu wawili au zaidi.
Kigezo kikuu cha kuyafanya yawe ya kifasihi ni kuwapo kwa usanii na ufundi katika muundo wake na jinsi yanavyowasilisha ujumbe wake.
Tumeona kuwa mazungumzo ni sehemu muhimu ya michezo ya jukwaani, lakini yanaweza pia kuangaliwa kivyake.
Katika jamii nyingi, mazungumzo hupatikana kwa njia mbalimbali. Njia kuu za kimsingi ni
- hotuba
- malumbano kati ya watani
- ulumbi au usemaji wa kiufundi wa wanajamii tofauti
- mawaidha
Hivi ni vipengele vyepesi kueleweka kwa sababu vimeenea katika jamii nyingi.
Vipera Vya Tanzu Ya Hadithi Katika Fasihi Simulizi
- Ngano:
Hizi ni hadithi za kimapokeo zinazotumia wahusika kama wanyama, majoka, binadamu, mawe, miti n.k.
Fanani wa ngano hutumia maneno ya kuvuta hadhira. Huanza na "PAUKWA" na hadhira hujibu "PAKAWA".
Fanani huanza kusimulia hadithi baada ya utangulizi huo. Utangulizi huwavutia na kuwachangamsha hadhira, na huwafanya waache kazi nyingine au kusinzia, wasikilize ngano hiyo.
Mtambaji wa ngano akiendelea kuhadithia anaweza kuuliza hadhira yake, "Niendelee? Au nisiendelee?" Kauli hiyo huwafanya hadhira wasisimke na kuitikia kwa sauti, "ENDELEA!!!"
Ngano hufuata muundo rahisi na wa moja kwa moja.
Kwa kawaida, lengo kuu la ngano ni kuwaasa watoto. Ndiyo maana humalizia kwa kuwatia moyo, kama vile "wakaishi kwa raha mstarehe", "wakazaa na kuzaa", "maisha yakawa mazuri", "amani ikatawale" n.k.
- Tarihi (visakale):
Hizi ni hadithi zinazosimuliwa kutokana na matukio ya kihistoria.
Matukio hayo huundwa kisanaa ili kuvutia watu katika jamii.
Tarihi inahusu matukio yanayoweza kuwa ya furaha au huzuni. Ni za kusisimua ili kuwakumbusha watu walikotoka.
Fanani wa tarihi mara nyingi pia huanza kusema "paukwa" na hadhira huitikia "pakawa".
Baadhi ya masimulizi ya tarihi huanza kwa nyimbo au majigambo. Hayo huwafanya wasikilizaji kuwa makini na matukio yanayosimuliwa.
Mara nyingi wahusika wa tarihi ni binadamu. Hupewa uwezo mkubwa au mdogo mno ili kuyakinisha matukio yanayozungumziwa na kuyawekea mantiki.
Tarihi anaweza kusimulia kuhusu
- historia ya mfalme
- koo za kitawala
- kumbukumbu za kutokea kwa ukoo fulani
- magonjwa
- vita
- njaa
- Visasili:
Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii kuhusu
- asili ya ulimwengu na mwenendo wake
- asili yao wenyewe
- maana na shabaha ya maisha yao
Hadithi hizi husimulia mambo yanayohusiana na maumbile ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai.
Wahusika wa visasili ambao si binadamu hupewa hadhi na uwezo wa binadamu.
Kwa mfano, hadithi inayohadithiwa chanzo cha chura kuwa na mabakamabaka, au jongoo kuwa na mwili ung'aao na mwororo, ni kisasili.
Visasili husimulia mianzo au asili ya matendo ya kufikirika, imani au mtazamo fulani katika jamii.
Usimulizi wa visasili pia huambatana na nyimbo.
- Vigano:
Hizi ni hadithi fupi zinazosimuliwa kwa lengo la kuelezea makosa au uovu wa watu fulani na kutoa maadili yanayofaa.
Hadithi hizi hutumia sana nahau na methali katika kutoa maadili kwa hadhira iliyokusudiwa.
Maadili hayo hutolewa kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu.
Wahusika katika vigano ni wanadamu na hata wanyama.
Kwa kawaida vigano hujengwa juu ya tukio moja. Tukio hilo hutumiwa kuelezea maisha halisi katika jamii husika.
Mara nyingi vigano havienei sana kwa jamii kwa sababu hutumiwa katika muktadha wa mazungumzo.
Tamthiliya
Tamthiliya Ni Nini?
Tamthiliya au drama ni fani iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani. Kwa lugha ya kawaida, tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza.
Kwa kawaida, tamthiliya huwa na masimulizi. Masimulizi hayo huigizwa na wahusika wa pande mbili au zaidi zinazogongana.
Mgongano huo husababisha mgogoro. Mgogoro ukisuluhishwa na kutanzuliwa, mchezo huwa umemalizika.
Tamthiliya ni sanaa ya maneno. Hivyo ina sifa za kawaida za sanaa za maonesho, ambazo ni
- Dhana inayotendeka
- Watendaji
- Hadhira
- Kusudio la kisanaa
- Uwanja au jukwaa
- Muktadha wa kisanaa
- Ubunifu au umathilishaji
Tofauti Kati Ya Tamthiliya Na Sanaa Nyingine Za Maonesho
Mlama anaeleza tofauti kati ya tamthiliya na sanaa nyingine za maonesho kama ifuatavyo
"Tamthiliya ni aina moja wapo ya sanaa za maonyesho ambazo usanii wa utendaji wake hutegemea zaidi MATENDO na UONGEAJI, tofauti na aina nyingine kama ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji muziki. Tamthiliya ni ule utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa, ambao unaliweka wazo linalotaka kuwasilishwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira."
Kwa mujibu wa maelezo hayo, kitu kikubwa kinachotofautisha tamthiliya na sanaa nyingine za maonesho kama ngoma ni msisitizo wake kwenye VITENDO na MAZUNGUMZO YA WAHUSIKA.
Istilahi ya tamthiliya inatokana na neno "mithali". Neno hilo lina maana ya mfano au ishara ya kitu fulani.
Hivyo, katika tamthiliya kitu kimoja humathilishwa au huwasilishwa na kitu kingine.
Mfano ni mchezo wa KINJEKITILE. Mwigizaji wa sehemu ya Kinjekitile huwakilisha mhusika aitwaye Kinjekitile katika mchezo. Mhusika huyo wa mchezo huwasilisha kwa kiasi fulani Kinjekitile wa historia.
Aina Za Tamthiliya
Zipo aina nyingi za tamthiliya, kama ifuatavyo.
- TANZIA
Tamthiliya ya kijadi ya Ulaya ilikuwa na matawi mawili makuu: TANZIA na KOMEDIA.
Tanzia ni tamthiliya ya majonzi kuhusu anguko la mhusika mkuu.
Anguko au kifo hicho huweza kusababishwa na
- Udhaifu wake binafsi wa kitabia
- Kosa fulani alilofanya
- Mazingira fulani yaliyomzidi uwezo
- Mchanganyiko wa baadhi ya sababu hizo
Mfano ni anguko la Kinjekitile. Ni matokeo ya kosa lake binafsi (kuwafanya watu kuyaamini zaidi maji). Pia ni matokeo ya mazingira ya kihistoria, yaani ya kisiasa na kijamii, ambayo hana uwezo nayo.
- KOMEDI / RAMSA
Komedi au ramsa ni kinyume cha tanzia. Hii ni tamthiliya inayoishia katika furaha.
Mhusika mkuu hupambana na matatizo ya kila aina, kiasi cha kukaribia kushindwa. Hata hivyo, hatimaye hushinda na kufanikiwa katika malengo yake.
Mifano ni tamthiliya za Shakespeare: "Mabepari wa Venisi" na "Shida ni Ramsa".
Komedi hupendwa sana na vijana na hata watu wazima. Huwa na mvuto na ucheshi. Huweza kuelimisha bila kuleta majonzi au kukatisha tamaa.
Zipo pia tamthiliya zinazochanganya sifa za tanzia na komedi.
- VICHEKESHO
Vichekesho ni aina ya tamthiliya gezwa au faraguzi. Hizi ni tamthiliya zinazotungwa papo kwa papo bila kuandikwa.
Tamthiliya hizi zilianza miaka ya 1920. Lengo lilikuwa kuburudisha wakazi wa mijini wakati wa mapumziko.
Kwa kawaida zilikuwa na vituko vya kuchekesha. Ziliwasuta watu waliofikiriwa kuwa WASHAMBA, WAJINGA na WASIOSTAARABIKA.
Hivyo mara nyingi zilimwonyesha mhusika anayetoka shamba na kuja kuzuzuka mjini.
Vichekesho viliendelea hata baada ya uhuru, na bado vipo. Dhamira zake zimebadilika.
Baadhi ya vichekesho siku hizi huigizwa radioni, kwenye televisheni na kwenye vilabu vya pombe.
- MICHEZO BUBU
Hii ni aina ya tamthiliya isiyotumia maneno. Waigizaji hutumia ishara na vitendo tu. Hadhira hujua kinachotokea kwa kuzisoma ishara hizo.
Tamthiliya hizi hufaa sana katika jamii zenye mchanganyiko wa watu wasiozungumza lugha moja.
Zikiandaliwa vizuri na kuchanganywa na sauti za muziki au ngoma, huvutia sana.
- DRAMA NGANO
Zipo drama ngano za aina mbili.
Aina ya kwanza ni tamthiliya gezwa ambazo watoto au watu wazima huzibuni kutokana na ngano zetu za Kiafrika.
Ngano au hadithi simulizi huigizwa jukwaani kama drama, badala ya kutambwa au kusimuliwa tu. Hii ni njia nzuri sana ya kupata michezo ya vijana shuleni.
Watoto wenyewe huweza kuitunga na kuiigiza michezo hiyo. Hii ni kwa sababu ngano nyingi huhusu wanyama. Watoto hujipamba kwa maleba, sauti na kadhalika ili kuigiza wahusika wanaowapenda, kwa mfano sungura.
Siku hizi televisheni za Ulaya zinatumia sana mbinu hii. Hasa katika filamu za vikatuni na vikaragosi au wanasesere (puppets).
Aina ya pili ni tamthiliya za kimajaribio. Hizi hujaribu kuigiza fani za jadi za Kiafrika katika umbo la tamthiliya za Kizungu.
Katika tamthiliya hizo, anaweza kuwepo mtambaji anayeanza kwa kusema PAUKWA. Mwitikiaji hujibu PAKAWA. Kisha mchezo huendelea kwa njia ya masimulizi na maigizo.
Mifano mizuri ni
- Tamthiliya za E. Hussein: "Jogoo Kijijini" na "Ngao za Jadi"
- Tamthiliya za Penina Mhando: "Lina Ubani" na "Nguzo Mama"
- DRAMA NGOMA
Drama ngoma ni maigizo yanayoambatana na kufungamana na uchezaji wa ngoma (dansi).
Hadithi ya drama huigizwa kwa miondoko ya ngoma na nyimbo, badala ya masimulizi na mazungumzo ya wahusika.
Hii ni fani inayokubaliana sana na sanaa za maonesho za Kiafrika. Kwa vyovyote huweza kuwavutia na kuwasisimua watoto.
Aidha, hutoa nafasi kwa hadhira yenyewe kushiriki katika igizo badala ya kuwa watazamaji tu.
- MICHEZO YA REDIO
Michezo ya redio ni tamthiliya zinazotegemea sauti zaidi kuliko macho. Hivyo zinahitaji mbinu maalum za kuvutia sikio ili zifanikiwe.
Hadhira huwasikiliza waigizaji wanapoongea. Husikia sauti au vishindo vya mambo yanayotendeka. Hata hivyo, haiwaoni watu hao wala kushuhudia matukio hayo.
Njia hii ya maigizo huweza kuwafikia watu wengi katika eneo kubwa.
- MICHEZO YA SINEMA NA RUNINGA
Hizi ni tamthiliya za kisasa zilizokusudiwa kuoneshwa katika sinema au televisheni kwa hadhira pana.
Utunzi wake unahitaji ufundi maalum. Huhitaji maelekezo mengi kuhusu jukwaa, mandhari na matendo ya wahusika.
Mazungumzo ya wahusika huwa machache kuliko katika mchezo wa redio au katika tamthiliya ya kawaida.
- TAMTHILIYA GEZWA / FARAGUZI (IMPROVISED DRAMA)
Hii ni michezo inayoandaliwa bila kuandikwa. Waigizaji hujitungia maneno yao papo kwa papo wakati wa onesho.
Njia hii hufaa sana vijijini na shuleni. Hupunguza sana matatizo ya ukosefu wa tamthiliya zilizoandikwa.
Aidha, hakuna lazima ya kukariri. Watoto na vijana wanaweza kujitungia michezo yao na kuigiza bila msaada wa mtu mzima.
Hii ni njia nzuri ya kupata tamthiliya nyingi za watoto na vijana.
Hata hivyo, tamthiliya hizi hudai ubunifu na uwezo mkubwa wa lugha kutoka kwa waigizaji.
Vijenzi Vya Tamthiliya
Kwa mujibu wa kanuni za ki-Aristotle, tamthiliya yoyote kwa kawaida huwa na vipengele vifuatavyo:
- hadithi (simulio)
- vitendo
- waigizaji wanaomathilisha wahusika wa hadithi
- dayalojia (mazungumzo)
Siku hizi dayalojia yaweza kuwa ya maneno au ishara.
Hadithi (Simulio)
Tamthiliya husimulia hadithi au kisa fulani.
Hadithi hiyo yaweza kuwa ya kubuni. Yaweza kuwa tukio la kweli la kihistoria. Pia yaweza kuwa mchanganyiko wa yote mawili.
Hadithi hiyo kwa kawaida huhusu mzozo fulani unaohusisha pande mbili
- upande wa mbabe (shujaa wa hadithi) au nguli (mtendaji mkuu)
- upande wa mpinzani wa mbabe au nguli
Hadithi hiyo husukwa kwa namna inayoujenga mgogoro wa pande hizo mbili hadi kufikia mwisho wake.
Mtiririko wa matukio kwa kawaida huwa na umbo la piramidi lenye hatua.
Hatua A: Chanzo
Katika hatua hii ndipo huwa mwanzo au utangulizi wa mchezo.
Katika hatua hii mambo yafuatayo hujitokeza
- Usuli wa mgogoro wa tamthiliya huelezwa.
- Hali ya tamthiliya (ya majonzi, ya miujiza, ya nderemo) hudhihirishwa.
Vitendo
Tamthiliya hugawanyika katika sehemu kuu ziitwazo vitendo.
Kila kitendo (act) huzingatia tendo kuu ndani ya mchezo.
Kwa mfano, katika mpangilio wa matukio ulioelezwa hapo juu, kila kipengele kingeweza kuwa kitendo kimoja.
Hivyo tamthiliya yenye mpangilio huo kijadi ilitakiwa kuwa na vitendo vitano.
Katika tamthiliya ya Kigiriki, kumalizika kwa kitendo kuliashiriwa na kuingia kwa wazumi (chorus) jukwaani.
Siku hizi zipo tamthiliya zenye kitendo kimoja, vitendo viwili, vitatu, vitano, na hata zaidi.
Onesho
Kila kitendo hugawanyika katika sehemu ndogo ziitwazo "maonesho".
Onesho moja kwa kawaida huwasilisha tukio moja linalotendeka mahali pamoja.
Onesho moja hutenganishwa na jingine kwa kuzingatia mantiki ya kile kinachosimuliwa. Tukio moja likimalizika, onesho nalo huwa linamalizika.
Wakati wa maigizo, mabadiliko ya maonesho jukwaani huashiriwa kwa njia hizi
- kufunga pazia
- kuzima taa
- wahusika kuondoka jukwaani
Wahusika Na Waigizaji
Usawiri wa wahusika wa tamthiliya hufanywa kwa njia ya matendo na mazungumzo. Sababu ni kwamba fursa ya kutoa maelezo marefu haipo.
Wahusika wa tamthiliya hawana tofauti kubwa na wahusika wa hadithi. Wanaweza kuwa mviringo, bapa, watu wa tabaka la juu, wanyonge n.k.
Tamthiliya huwa na wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika wakuu
Mbabe au nguli: Huyu ni shujaa wa tamthiliya. Matendo mengi yanahusu maisha na majaliwa yake. Katika KINJEKITILE (E. Hussein, 1969), Kinjekitile ndiye mbabe au nguli (protagonist), yaani mhusika kiini au mtenzi mkuu.
Katika tanzia ya kijadi, mbabe aghalabu alikuwa mtu wa tabaka la juu. Aliangamia kwa moja ya sababu hizi:
- hila (dosari) fulani katika tabia na maamuzi yake
- kusaka na mazingira yanayomzidi uwezo
- yote mawili, kama mfalme Odipade
Mkinzani (antagonist): Ni mhusika mkuu anayepambana na mbabe au nguli.
Muwi (villain): Ni mhusika muovu. Mfano ni Shylock wa Shakespeare, katika Mabepari wa Venis.
Wahusika wadogo
Hawa aghalabu huwa ni wengi. Baadhi yao huwa na jukumu dogo tu katika tamthiliya. Wanaotokea mara kwa mara ni hawa:
Mfoili: Ni mhusika anayewekwa sambamba na nguli. Ana sifa tofauti na za nguli. Lengo ni kumpambanua nguli vizuri zaidi.
Msimulizi: Ni mhusika anayetumiwa na mtunzi kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu matendo na matukio katika michezo. Katika baadhi ya michezo, mhusika huyu hupewa jina jingine, kama mwimba.
Chizi (clown): Ni mhusika mcheshi. Hufanya vitu vya kipumbavu na kusema maneno ya kijingajinga ili kuiburudisha hadhira. Wakati mwingine hutoa ujumbe fulani.
Waigizaji
Waigizaji pengine huitwa wamathilisha. Ni watu wanaotokea jukwaani mahali pa wahusika wa mchezo. Kwa vitendo na tabia zao, huwamathilisha wahusika hao.
Waigizaji hawana budi kuteuliwa vizuri. Hivyo wataweza kuwakilisha na kuwasilisha sawasawa mambo haya ya wanaowamathilisha:
- umbo
- hali
- hisia
- tabia
- mawazo
- matendo
Daiolojia (Mazungumzo Ya Wahusika)
Hadithi ya tamthiliya husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika.
Mazungumzo ya wahusika ndiyo huitwa daiolojia.
Mafanikio ya michezo mingi hutegemea jinsi mtunzi anavyofaulu kuweka daiolojia inayovutia na kuaminika.
Daiolojia ni lazima iwe na maneno machache yaliyoteuliwa vizuri. Maneno hayo huisogeza mbele hadithi au kudhihirisha jambo fulani alilokusudia mtunzi.
Baadhi ya tamthiliya huwa na monolojia pia. Katika monolojia, mhusika huzungumza mwenyewe ili kudhihirisha mawazo aliyonayo moyoni.
Zipo pia tamthiliya zinazotumia masimulizi. Hapo msimulizi husimulia mambo yaliyotokea, mithili ya mtambaji wa hadithi au utendi. Mbinu hii hutumika katika drama tendi.
Baadhi ya tamthiliya za Kiswahili zimetumia mbinu hizi. Mfano ni MKWAWA WA UHEHE ya M. Mulokozi.
Mbinu Nyinginezo
Mbinu nyinginezo zinazotumiwa na watunzi wa tamthiliya zimekwisha elezwa.
Tamthiliya za Kiswahili, hasa zile zilizoandikwa, zimeiga baadhi ya mbinu za kimagharibi. Nyingi zina muundo wa ki-Aristotle. Zinatumia daiolojia, zina vitendo, maonyesho na migogoro inayosuluhishwa mwishoni.
Baadhi ya tamthiliya zimejaribu kuiga mbinu za sanaa za maonyesho za jadi za Kiafrika.
Miongoni mwa wanamajaribio hao wa mwanzo ni Ebrahim Hussein. Alijaribu kutumia mbinu za utambaji wa ngano katika maigizo yake NGANO ZA JADI na JOGOO KIJIJINI. Mpaka sasa wataalamu hawajakubaliana kama tungo hizo mbili ziitwe tamthiliya au tendi.
Penina Mhando pia alijaribu kutumia utambaji wa ngano katika tamthiliya zake LINA UBANI na NGUZO MAMA.
Mbinu ya majigambo ilitumiwa na watunzi hawa
- Mhando na wenzake katika HARAKATI ZA UKOMBOZI
- Mbogo katika SUNDIATA
Mbinu ya tendi simulizi ilitumiwa na Mulokozi katika MKWAWA WA UHEHE.
Hii ni mifano ya baadhi ya mbinu ambazo watunzi wa tamthiliya wanaweza kutumia. Mbinu hizi huzifanya tungo zikaribiane zaidi na utamaduni wa wale walioziandika.
Kutunga Kazi Za Fasihi Simulizi
Dhana ya utungaji
Kutunga ni kitendo cha kutoa mawazo ubongoni, kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyasimulia.
Hatua za mwanzo za kuzingatia katika kutunga kazi za kifasihi
- Kuwa na jambo unaloona linasababisha mvuto au lina mvuto kwa jamii. Kisha unalifanyia utafiti ili kujua chanzo chake na kwa nini linaendelea kuwepo.
- Baada ya utafiti, fanya maamuzi ya njia au tanzu gani utatumia kufikisha ujumbe. Chaguo ni ushairi, hadithi, semi na maigizo.
- Chagua kipera cha kutumia kutoka katika tanzu uliyochagua. Mfano, kama ni ushairi, atumie nyimbo au ngonjera.
- Jenga jambo hilo katika fani na maudhui ili kupata mbinu sahihi ya kuwasilisha kazi yako kwa hadhira.
- Mtunzi ajikite hasa katika maudhui ya jambo analotaka kuliwasilisha. Mfano, dhamira yako ni nini?
- Mtunzi aangalie namna ya kuwasilisha maudhui yake. Hapa anashughulikia vipengele vya fani, yaani muundo, mtindo, mandhari, wahusika na matumizi ya lugha. Anatakiwa atumie ufundi na ubunifu wa hali ya juu ili kazi yake ielimishe na kusisimua.
- Baada ya fani na maudhui kushughulikiwa, mtunzi aangalie namna ya uwasilishaji wake. Aangalie kanuni na taratibu za kipera alichotumia.
- Mtunzi aanze kuandika yale anayotaka kuelimisha jamii kwa kufuata taratibu za uandishi.
- Mtunzi asome kuangalia kama kile alichokidhamiria ndicho alichokitunga.
- Afanye mazoezi ya namna ya kuwasilisha kazi hiyo.
Mfano: Namna ya kutunga igizo la fasihi simulizi
- Kwanza, teua wahusika watakaosawiri matendo ya tabia zao:
- Mhusika mkuu hujitokeza mara kwa mara, na matendo mengi yanamhusu yeye.
- Wahusika wadogo huwa wengi.
- Teua waigizaji wazuri watakaofanya vizuri katika kuliwasilisha igizo.
- Wahusika wajengwe kwa kuzingatia utendaji wao.
- Teua lugha itakayotumika.
- Teua mandhari nzuri katika uwasilishaji wake.
- Angalia muundo na mtindo wa igizo lako.
