Kiswahili · Kidato 5

Utumizi wa Lugha

Dakika 13 za kusoma ·

Yaliyomo

Rejesta

Rejesta ni matumizi ya lugha kutokana na muktadha maalumu.

Siku zote, matumizi ya lugha hutofautiana kutokana na mambo mengi.

Mambo Ya Kuzingatia Unapotumia Lugha

Wakati unatumia lugha, kuna mambo ya kuzingatia kama yanavyoelezwa hapa chini.

  1. Mazingira

Mazingira humwamulia mtu namna ya kutumia lugha. Kwa mfano, lugha ya hotelini ni tofauti na lugha ya kanisani.

Kutokana na mazingira, tunaweza kupata lugha ya

  • hotelini
  • shuleni
  • ofisini
  • kanisani
  • mitaani
  1. Uhusiano baina ya wahusika

Uhusiano baina ya wahusika hufanya matumizi ya lugha yabadilike.

Mfano, lugha ya marafiki vijana imejaa misimu mingi na maneno yasiyo na adabu. Lugha ya baba na mtoto ina maneno yenye heshima.

Pia, uhusiano baina ya wahusika unatupatia lugha ya

  • mtu na mpenzi wake
  • mwalimu na mwanafunzi wake
  • meneja na wafanyakazi wa chini yake
  • n.k.
  1. Mada ya mazungumzo

Mada ya mazungumzo ndiyo inayokuamulia maneno ya kusema.

Kutokana na mada ya mazungumzo tunapata lugha ya

  • kibiashara
  • kitaaluma
  • mahubiri
  • kisiasa
  • kisheria
  • n.k.
  1. Madhumuni ya mazungumzo

Watu wanapotumia lugha huwa na lengo. Kutokana na malengo hayo, lugha inayotumiwa hubadilika ili kuendana na lengo la mzungumzaji.

Kama lengo la mzungumzaji ni kuomba msaada fulani, atatakiwa kutumia lugha ya unyenyekevu kama "tafadhali", "samahani" n.k.

Kama lengo ni kutoa amri, lugha ya mzungumzaji itakuwa na maneno yenye kuashiria amri kama vile ondoka, cheza, soma, imba n.k.

  1. Utanzu wa mawasiliano

Utanzu wa mawasiliano una nafasi kubwa katika uteuzi wa lugha.

Kama ni utanzu wa hotuba, majadiliano, masimulizi n.k., matumizi ya lugha lazima yaendane na utanzu huo.

  1. Mila na desturi

Mila na desturi humlazimisha mzungumzaji kubadili lugha yake ili aendane nazo.

Kutokana na mila na desturi za Waswahili, matusi hayapaswi kuzungumzwa waziwazi. Hivyo, mzungumzaji anapaswa kutumia tafsida.

Mitindo Mbalimbali Ya Lugha Kutokana Na Mazingira

Mtindo wa lugha ni mabadiliko katika kutumia lugha.

Lugha moja ina mitindo tofauti kutokana na mazingira. Mfano, lugha inayotumika kanisani ni tofauti na lugha ya msikitini.

Ifuatayo ni mitindo mbalimbali ya lugha.

  1. Mtindo wa shughuli za kiofisi na kikazi

Mtindo huu huweza kupatikana ofisini, mikutano, vikao n.k.

Miongoni mwa sifa za mtindo huu ni

  • usahihi wa mambo yanayojadiliwa
  • matumizi ya msamiati unaoonesha vyeo vya watu
  • kutotumika kwa mafumbo, lahaja na nahau
  1. Mtindo wa mambo ya kitaaluma na kisayansi

Mtindo huu unatumika katika mambo ya kitaaluma, kama vile Kiswahili, Kemia, Bailojia na Fizikia.

Sifa za mtindo huu ni

  • usahihi na ukweli wa mambo yanayojadiliwa
  • kuwepo na mantiki katika jambo linalojadiliwa
  • uendeshaji wa mjadala bila kuonesha upendeleo wa mwandishi
  • matumizi ya istilahi za kitaaluma na kisayansi
  • sifa nyinginezo
  1. Mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa

Sifa za mtindo huu ni

  • upendeleo wa wazi wa mzungumzaji
  • kuwepo kwa mantiki katika jambo linalozungumzwa
  • matumizi makubwa ya istilahi maalumu za magazetini na shughuli za kisiasa
  1. Mtindo wa mazungumzo ya kawaida ya kila siku

Mtindo huu ni wa maongezi yasiyo rasmi, yaani maongezi ya kawaida yanayofanyika nyumbani na mahali pengine pa kawaida.

Mazungumzo haya yanaweza kuwa kati ya baba, mama, mtoto n.k.

Dhima Ya Rejesta Katika Lugha

Katika lugha, rejesta ina dhima (matumizi) mengi. Miongoni mwa dhima hizo ni hizi zilizoelezwa hapa chini.

  1. Kukidhi haja ya mawasiliano ya uwanja fulani maalumu

Kila eneo lina namna yake ya uzungumzaji. Ili uweze kufikisha ujumbe kijiweni, ni lazima kutumia mtindo wa kijiweni.

Pia, huwezi kufikisha ujumbe kanisani kwa kutumia mtindo wa lugha za mitaani. Hivyo, rejesta inasaidia kufikisha mawasiliano katika uwanja fulani maalumu.

  1. Kutambulisha wazungumzaji kuwa wao ni wa kundi fulani

Rejesta huweza kutambulisha kuwa watu fulani ni wa kanisani, msikitini, kijiweni, au pengine ni wavuvi, kutokana na mtindo wa mazungumzo yao.

  1. Kupunguza ukali wa maneno

Rejesta inapotumiwa na kundi fulani, hupunguza ukali wa maneno kwa kutumia tafsida.

Kwa mfano, badala ya kusema "naenda chooni", wazungumzaji wengi husema "naenda ofisini".

  1. Kupamba lugha

Rejesta hufanya lugha ivutie. Lugha ya kawaida inaweza isiwe na mvuto kama pale rejesta inapotumika.

Kwa mfano, badala ya kuuliza "nani kaagiza wali na kuku?", muuzaji huuliza "nani wali kuku?". Maneno haya yana mvuto wa aina yake.

  1. Kukuza lugha

Yapo maneno yaliyotokana na rejesta na baadaye yakawekwa katika msamiati wa lugha ya Kiswahili. Hivyo yanasaidia katika ukuzaji wa lugha hii.

Mifano ya maneno hayo ni

  • shangingi
  • kibaka
  • mlokole
  • dingi
  1. Kuficha ujumbe

Baadhi ya watu huongea kwa rejesta zao ili kuficha maana kwa wale wasiohusika.

Kwa mfano, wanafunzi darasani wanaweza kusema "naamsha majeshi", wakiwa na maana ya kutoroka shule.

Misimu

Misimu ni semi za muda na mahali maalumu ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalumu.

Aina Za Misimu

  1. Misimu ya pekee

Ni misimu ambayo hutumika katika eneo moja. Wale wasiohusika katika eneo hilo hawawezi kuelewa wala kuitumia.

Mfano: Wanafunzi wa shule moja wanaweza kuwa na aina ya misimu yao. Katika shule ya Kigoma Sekondari, wanafunzi wa shule hiyo wana msimu uitwao "ugu", wakiwa na maana ya kuamka usiku kusoma. Msimu huu huwezi kuukuta katika shule zingine.

  1. Misimu ya kitarafa

Hii ni misimu ambayo huweza kufahamika kwa ngazi ya tarafa, kata, wilaya na hata mkoa. Misimu hii huweza kupatikana kutokana na vitu na watu waliopo katika eneo hilo.

Mfano: Mkoani Dar es Salaam kuna msimu uitwao "maji ya Kandoro", ukiwa na maana ya maji yaliyofungwa katika mfuko mweupe wa plastiki. Mikoa mingine haina msimu huo.

  1. Misimu zagao

Ni misimu ambayo huenea nchi nzima na wakati mwingine huvuka mipaka ya nchi.

Misimu kama wafurukutwa, wapambe na ngangari ni misimu zagao.

Utumizi Wa Lugha

Sifa Za Misimu

  1. Huzuka na kutoweka

Misimu huzuka na kutoweka kwa sababu ya kupita kwa wakati.

Mfano: kipindi cha ujamaa kulikuwa na misimu mingi kama "kupe" na mingineyo. Yote hii haipo leo.

  1. Ni lugha isiyo sanifu

Misimu huwa nje ya lugha rasmi.

Sababu yake ni kwamba huzushwa na watu wa kundi fulani kwa sababu zao maalum.

  1. Ni lugha ya mafumbo

Ni vigumu kuelewa misimu kama huhusiki katika kundi linaloitumia.

Sababu yake ni kwamba misimu imejaa mafumbo, na wasiohusika hushindwa kuelewa.

  1. Ina chuku nyingi

Misimu imetiwa chumvi, yaani ina sifa zilizopitiliza.

Ni rahisi kukuta vijana wakimwita mwenzao "mwamba" hata kama amefanya jambo dogo.

  1. Hupendwa na wengi

Wengi hupenda misimu.

Wengi huitumia ili kuonesha uhodari wao katika lugha.

  1. Ina maana nyingi

Mara kwa mara msimu huwa na maana zaidi ya moja.

Mfano: msimu unaotumika Mbeya unaweza kuwa na maana tofauti ukitumika Dar es Salaam.

Mfano mwingine: mtumiaji wa misimu akisema "kausha", msimu huu unaweza kuleta maana zaidi ya moja. Kwanza, unaweza kumaanisha "nyamaza". Pia unaweza kumaanisha kukausha chakula aina ya "chipsi mayai".

Umuhimu Wa Kutumia Misimu Katika Lugha

Misimu ina umuhimu wake katika lugha, kama ifuatavyo

  1. Kukuza lugha

Baadhi ya maneno huanza kama misimu kisha huwa lugha rasmi.

Mifano ya maneno yaliyoanza kuwa misimu na sasa ni maneno rasmi: magendo, marupurupu, chungu nzima, daladala na mtumba.

  1. Kupamba lugha

Misimu hupamba lugha na kuwafanya watu wafurahi wanapozungumza.

Mfano: mzungumzaji anaweza kusema, "Leo Yanga hawahemi, tuna mashambulizi chungu nzima ya kuwashikisha adabu 'visura' hawa!"

  1. Kufanya mawasiliano yawe mafupi na yanayoeleweka

Misimu husaidia kufupisha mawasiliano. Hutumia maneno machache, hivyo ujumbe hueleweka kwa haraka.

Mfano: daladala ni msimu unaoeleweka kwa haraka na unaookoa muda.

Ni tofauti na mtu kusema, "magari madogo yanayobeba abiria ambayo husafiri kutoka sehemu moja ya mji mpaka nyingine lakini ndani ya mji huohuo."

  1. Kupunguza ukali wa maneno

Misimu hutumika kupunguza ukali wa maneno katika mada tofauti, kama vile mapenzi na mazungumzo ya kila siku.

Mfano: mtu husema "nakwenda ofisini" badala ya kusema "chooni".

  1. Kuhifadhi historia ya jamii

Misimu huhifadhi historia ya jamii. Hii ni kwa sababu ya wakati ambao misimu hiyo ilianza kutumika.

Kipindi cha ujamaa, misimu iliyotumika ilikuwa: ubepari, ubeberu, ukupe, unyonyaji, ujamaa na utaifishaji.

Wakati wa ubepari, ilitumika misimu hii: ubinafsishaji, uwekezaji, vitega uchumi na utandawazi.

Wakati wa mfumo wa vyama vingi, misimu hii ilikuwa maarufu: chama tawala, mkereketwa, mfurukutwa, mpambe, wazawa, ngangari na mgombea mwenza.

  1. Kuwaunganisha watu wa makundi mbalimbali

Misimu huwaunganisha watu wa makundi yote. Huwaunganisha maprofesa, madaktari, walimu na watu wengineo.

Misimu kama daladala, ubepari, vitega uchumi na utandawazi hutumiwa na watu wa matabaka yote.

Changamoto Za Kutumia Misimu Katika Lugha

  1. Huharibu lugha sanifu

Misimu huwa nje ya lugha inayohusika.

Hivyo huharibu lugha sanifu kwa kuweka maneno mapya yasiyo sanifu.

  1. Huleta msamiati wenye matusi

Matusi ni sehemu ya misimu. Misimu mingi huambatana na maana zenye matusi.

Mfano: ngunguri ni msimu unaomaanisha mtu asiyetumia akili.

  1. Ni lugha ya mafumbo

Si rahisi kuelewa misimu.

Ni lugha ya mafumbo, na hueleweka kwa kikundi kidogo cha watu.

  1. Imetiwa chumvi nyingi

Kwa sababu ya kutiwa chumvi nyingi, misimu haiaminiki katika jamii.

Wakati mwingine misimu huweza kupotosha.

  1. Huzuka na kutoweka

Kuzuka na kutoweka kunasababisha misimu iwe na mchango mdogo katika kukuza lugha.

Ni misimu michache sana ambayo hufikia hadhi ya kuwa maneno rasmi.

  1. Ina maana nyingi

Kwa sababu maana ni nyingi, misimu hushindwa kueleweka. Kila mtu huielewa kivyake.

Hii ni kwa sababu misimu haina maana moja.

Mfano: ni vigumu kuelewa kama "beki tatu" ni mfanyakazi wa ndani au ni mchezaji wa mpira anayecheza safu ya ulinzi.

Umahiri Wa Lugha

Umahiri wa lugha ni ujuzi wa hali ya juu wa lugha katika stadi nne za lugha. Stadi hizo ni: kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.

Nchini Tanzania, watu wengi ni mahiri wa lugha za makabila yao, kama vile Kisukuma, Kimakonde, Kiha, Kifipa na makabila mengine.

Pia, watu wengi ni mahiri wa lugha ya Kiswahili. Kiswahili ndiyo lugha inayowaunganisha watu wote.

Mambo Yanayomwezesha Mtu Kuwa Mahiri Wa Lugha

  1. Kusomea lugha kwa kiwango cha juu

Mtu anaposomea lugha fulani, hupata ujuzi katika msamiati, sarufi, matamshi pamoja na maana.

Hiyo humfanya awe mahiri wa lugha hiyo.

  1. Kutumia lugha kila siku

Mtu anayetumia lugha kila siku, uwezo wake huongezeka. Hilo humfanya aweze kuimudu lugha husika.

Mfano: mtu anayetumia Kiswahili kila siku katika mazungumzo yake lazima atakuwa mahiri wa lugha ya Kiswahili.

  1. Kuwa karibu na wajuzi wa lugha

Mtu akiwa karibu na wajuzi wa lugha, hufaidika. Hufundishwa matumizi ya lugha hiyo na huiga jinsi wajuzi wanavyoitumia.

Mfano: mtu anayetoka Uingereza, akifika Tanzania na kuwa karibu na wajuzi wa lugha, huweza kujifunza lugha hiyo na hatimaye kuwa mahiri.

  1. Kuwakosoa na kuwasahihisha waharibifu wa lugha

Anayekosoa huwa mahiri kwa kuonesha uwezo wake na kuwa bora zaidi.

Pia, wanaokosolewa huweza kuwa mahiri kwa kujifunza njia sahihi za kutumia lugha.

Athari Za Umahiri Wa Lugha

Umahiri wa lugha una athari zake.

Watu ambao ni mahiri wa lugha zaidi ya moja hukumbwa na athari hizi

  1. Matamshi

Matamshi huweza kumbainisha mtu anatoka wapi.

Mfano: mahiri wa lugha ya Kikurya na Kiswahili hushindwa kutofautisha r na l.

Unaweza kumsikia Mkurya akisema, "twende mbere tukarare."

  1. Msamiati

Mahiri wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza hujikuta wakichanganya msamiati wa lugha hizo.

Mfano: msemaji anaweza kusema, "tunatakiwa kuwa serious kwa sababu hii application ina wahusika wengi."

  1. Sarufi

Muundo wa lugha ya kwanza unaweza kumwathiri mahiri katika kuzungumza lugha ya pili.

Katika lugha ya Kinyamwezi, mtu anayezungumza na mtu wanayeheshimiana sana hutumia wingi badala ya umoja.

Hivyo, mahiri huyu anaweza kuchukua muundo huo na kuuweka katika lugha ya pili. Anaweza kutengeneza sentensi hii: "Baba ndiyo mmefika?"

Katika mfano huo, baba ni mmoja lakini mzungumzaji ametumia wingi kwa sababu ya athari za umahiri.

Maana

Kuna athari ya maana kwa watu wanaozungumza zaidi ya lugha moja.

Mfano, katika Kinyamwezi, neno igolo lina maana ya kesho na keshokutwa. Kwa hiyo, mnyamwezi anaweza kuathiriwa na kujikuta akisema, "nitakwenda jana." Au "nilikwenda keshokutwa."

Mambo Yanayopoteza Umahiri Wa Lugha

Yapo mambo yanayoweza kupoteza umahiri wa lugha. Miongoni mwa mambo hayo ni haya

  1. Kutotumia lugha hiyo kwa matumizi ya kila siku

Mahiri akiacha kutumia lugha kwa matumizi yake ya kila siku, umahiri hupotea.

Watanzania wengi wamepoteza umahiri wa lugha zao za kikabila kwa sababu ya kutozitumia kila siku.

  1. Kutosomea lugha hiyo kwa kiwango cha juu

Usiposomea lugha kwa kiwango cha juu, utapoteza umahiri. Hii ni kwa sababu ya kufanya makosa mbalimbali ya kimatamshi, kisintaksia, kisemantiki na kimuundo.

Mfano, Watanzania wengi ni mahiri wa lugha ya Kiswahili. Lakini wanapoteza umahiri wao kwa sababu hawajasomea lugha hiyo kwa kiwango cha juu.

  1. Hamahama ya watu

Watu wanapohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hujifunza lugha ya eneo wanalokwenda. Hii hupoteza umahiri wa lugha yao ya awali.

Mfano, watu wengi wanaohama kutoka kijijini kwenda mjini hupoteza umahiri wa lugha zao za kikabila.

  1. Mfumo wa elimu

Shule za msingi hutumia lugha ya Kiswahili kufundishia. Hivyo, wanafunzi hupoteza umahiri wa lugha zao za kikabila.

Pia, umahiri wa Kiswahili hupotea wanafunzi wanapoanza kusoma shule za sekondari. Huko lugha ya Kiingereza hutumika kufundishia.

  1. Kutokuwa karibu na wajuzi wa lugha hiyo

Mtu anapokuwa mbali na wajuzi wa lugha, umahiri wake hupungua. Hii ni kwa sababu anakosa msukumo wa kuzungumza lugha kwa ufasaha.

Mfano, mtu anapotoka mjini kwenda kijijini, umahiri wa lugha ya Kiswahili unaweza kupungua. Sababu ni kwamba kijijini watu wengi hutumia lugha za kikabila.

  1. Kasumba

Baadhi ya mahiri wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza wana kasumba ya kudharau lugha ya Kiswahili na kuitukuza lugha ya Kiingereza.

Hii hufanya umahiri wao wa lugha ya Kiswahili kupungua.

Utata Katika Mawasiliano

Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja.

Kwa mfano, sentensi "mtoto anaendesha" ina utata kwa sababu maana mbili zinaibuka. Maana ya kwanza ni kuendesha chombo cha barabarani kama gari. Maana ya pili ni kwamba ana maradhi ya tumbo la kuhara.

Sababu Za Utata

Zipo sababu nyingi za utata katika mawasiliano. Miongoni mwa sababu hizo ni hizi zinazoelezwa:

  1. Neno kuwa na maana zaidi ya moja

Yapo maneno mengi ya Kiswahili yenye maana zaidi ya moja. Baadhi ya maneno hayo ni: kaa, nyanya na paa.

  • Kaa ina maana ya kukaa chini, lakini pia inaweza kuwa na maana ya mdudu.
  • Nyanya ni kiungo, hata hivyo maana nyingine ya nyanya ni bibi.
  • Paa ina maana ya kitendo cha kuelea angani, au paa ni mnyama aishiye msituni.
  1. Kutozingatia taratibu za uandishi

Alama za uandishi hufanya maana ibadilike hata kama maneno katika sentensi ni yaleyale.

Mfano, "Tulimkuta baba na mtoto wake, Rajabu." Sentensi hiyo ina maana kwamba tulimkuta baba akiwa na mtoto wake aitwaye Rajabu.

Kama mkato usingewekwa, maana ingebadilika. Ingekuwa, tulimkuta baba akiwa na mtoto wa Rajabu.

  1. Utumiaji wa maneno yenye maana iliyofichika

Maneno yenye maana ya picha huleta utata.

Mfano, "Ninalo ua nyumbani kwangu." Sentensi hii ina utata kwa sababu inawezekana ua ni mmea, au ua ni msichana.

  1. Kuwepo kwa mofimu yenye kauli ya kutendea

Mfano, "amempigia ngoma." Katika sentensi hiyo, maana nyingi zinaibuka

  • Amepiga ngoma ili amfurahishe.
  • Amempiga kwa kifaa kiitwacho ngoma.
  • Amempiga kwa sababu ya ngoma.
  1. Matumizi ya vimilikishi

Vimilikishi navyo ni sababu ya utata.

Mfano, matumizi ya kimilikishi ake katika sentensi hii yanasababisha utata: "Ali atajenga kibanda chake."

Hapo haijulikani kama Ali atajenga kibanda chake mwenyewe, au atajenga kibanda cha mtu mwingine.

  1. Makosa ya kisarufi na kimantiki

Mfano wa makosa hayo ni: "Wewe mama, mwanao amerudi shule?"

Sentensi hiyo ina maana mbili. Kurudi shule kunaweza kumaanisha kitendo cha kwenda tena shule. Au kurudi shule kunaweza kumaanisha kurudi nyumbani kutoka shule.

Jinsi Ya Kuondoa Utata Katika Mawasiliano

Zipo njia nyingi za kuondoa utata katika mawasiliano. Miongoni mwa njia hizo ni

  1. Kuwe na mkazo wa sauti unaoonyesha dhahiri neno gani lipewe uzito zaidi. Hii itumike katika lugha ya mazungumzo.
  1. Kutumia kwa usahihi alama za uandishi kama mkato, kituo na alama nyinginezo.
  1. Kuepuka makosa ya kimantiki na kisarufi. Miongoni mwa makosa hayo ni kosa la kuacha maneno.

Mfano, "Damasi ameondoka kazini." Badala yake, useme "Damasi ameondoka kwenda kazini."