Kiswahili · Kidato 5

Fasihi kwa ujumla

Dakika 11 za kusoma ·

Yaliyomo

Fasihi Kwa Ujumla: Nadharia Ya Fasihi Na Sanaa

Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa.

Umbo hilo ni lile ambalo msanii hulitumia kufikisha ujumbe aliokusudia kwa jamii au hadhira.

Aina Za Sanaa

Sanaa za ghibu (muziki)

Sanaa hii inategemea matumizi ya ala za muziki (vifaa, sauti).

Uzuri wa umbo la sanaa ya muziki upo katika kusikia.

Sanaa hii haimlazimishi fanani (msanii) na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja.

Mtunzi hufanya kazi kwa wakati wake. Hadhira husikiliza kwa wakati wake.

Sanaa za ufundi

Sanaa hizi hutokana na kazi za mikono.

Mifano ni uchoraji, ususi, ufinyanzi, uchongaji, uhunzi, utalizi/udalizi n.k.

Uchoraji hutegemea sana kuwepo kwa kalamu, karatasi, kitambaa, brashi, rangi n.k.

Uchongaji huhitaji mundu, gogo, tupa n.k.

Uzuri wa umbo la sanaa za ufundi upo katika kuona.

Sanaa hii haimlazimishi fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja.

Sanaa za maonesho

Hizi ni kazi mbalimbali za sanaa zinazotegemea utendaji.

Mifano ni ngoma, maigizo, majigambo, matambiko n.k.

Sanaa zilizomo katika kundi la sanaa za maonesho ni lazima ziwe na sifa zifuatazo

  • Fanani
  • Dhana inayotendeka
  • Hadhira
  • Mandhari

Sanaa za maonesho zinamlazimisha fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja.

Sababu ni kwamba uzuri wa umbo la sanaa hii upo katika kuona utendaji.

Fasihi

Sanaa hii inategemea ufundi wa matumizi ya lugha.

Msanii ni lazima awe na uwezo wa kutumia vionjo vyote vya lugha. Mifano ni methali, misemo, tamathali za semi, nahau, vitendawili n.k.

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa hadhira inayokusudiwa.

Sanaa hii pia haimlazimishi fanani na hadhira kuwa pamoja mahali pamoja.

Kielelezo Cha Sanaa

Kila kipengele cha sanaa hutofautiana na kingine kwa umbo na matumizi.

Fasihi ni kipengele cha sanaa kinachotumia maneno kuumba uzuri wa kisanaa.

Tofauti Kati Ya Fasihi Na Tanzu Zingine Za Sanaa

  1. Lugha:

Kazi zote za fasihi huundwa kisanaa kwa kutumia lugha inayotamkika na inayoandikika.

Lugha hiyo hubeba ujumbe fulani. Hii ni tofauti na sanaa zingine, kama vile

  • Ufinyanzi hutumia udongo.
  • Uchoraji hutumia kalamu, rangi, karatasi au kipande cha nguo.
  1. Wahusika:

Kazi ya fasihi hulazimika kuwa na wahusika wake.

Wahusika hao hushiriki katika matukio mbalimbali yanayohusu jamii inayowazunguka.

Hutumika kutoa dhamira ya mwandishi.

Pia hutumiwa kuwasilisha tabia za watu waliomo ndani ya jamii.

  1. Mandhari:

Fasihi huwa na mandhari ambayo huonyesha mahali tukio linapofanyika.

Mandhari inaweza kuwa ya kubuni au ya ukweli.

  1. Utendaji:

Utendaji hujitokeza hasa katika kazi za fasihi simulizi.

Kazi hizi hushirikisha hadhira na fanani mahali pamoja na kwa wakati mmoja.

Hapa fanani anaweza kuonesha matendo katika usimuliaji wake.

  1. Fani na maudhui:

Fasihi ina sehemu mbili, fani na maudhui. Sehemu hizi hutegemeana na hufungamana.

Fani ni namna msanii anavyosema kuhusu kile kinachosemwa.

Maudhui ni kile kinachosemwa na msanii.

Usanaa Wa Fasihi

Usanaa wa fasihi hujitokeza katika vipengele vifuatavyo

  1. Mtindo

Sanaa katika fasihi hujidhihirisha katika namna ya kueleza jambo.

Hapa kinachoangaliwa zaidi ni mbinu mbalimbali anazotumia msanii kueleza jambo husika.

Jambo linaweza kuelezwa kwa fumbo kupitia shairi, tamthiliya, hadithi, kitendawili n.k.

  1. Muundo

Huu ni mpangilio mzuri wa visa na matukio.

Matukio katika kazi za fasihi hupangwa kiufundi ili yaweze kuwasilishwa vizuri kwa hadhira au jamii husika.

  1. Uteuzi mzuri wa lugha

Lugha hujaa vionjo mbalimbali kama vile nahau, misemo, tamathali za semi, taswira na ishara.

Lugha inaweza kuchekesha, kukosoa, kukejeli, kubeza, kushawishi n.k.

  1. Uundaji mzuri wa wahusika

Wahusika huumbwa kulingana na nia na lengo la mwandishi kwa hadhira yake.

  1. Ujenzi mzuri wa mandhari

Kazi ya fasihi ni lazima iwe katika mandhari maalumu.

Mandhari ikijengwa vizuri, husaidia sana kujenga hisia aliyokusudia mwandishi kwa hadhira yake.

Pia husaidia kufikisha ujumbe mahususi uliokusudiwa.

Fasili Za Fasihi

  1. Fasihi ni kioo:

Fasihi inafananishwa na kioo.

Kioo katika maisha ya kawaida humwonesha binadamu mazuri aliyonayo au mapungufu aliyonayo. Hivyo anaweza kujikubali au kujikataa.

Fasihi pia ina uwezo wa kuonyesha mazuri au mapungufu yaliyomo ndani ya jamii.

Inaweza kuyaonyesha kwa jamii nzima, au kwa baadhi ya vikundi ndani ya jamii ambavyo vinaweza kuwa tofauti na mahitaji ya jamii nzima.

Udhaifu

Fasihi ina uwezo wa kuonesha mambo kama ni mabaya au mazuri.

Lakini haina uwezo wa kuonesha njia ya kutatua matatizo hayo, kama ilivyo kioo.

  1. Fasihi ni mwamvuli:

Fasihi inafananishwa na mwamvuli kwa jinsi mwamvuli unavyoweza kumhifadhi binadamu dhidi ya jua au mvua.

Msingi halisi wa kufananisha fasihi na mwamvuli ni kwamba fasihi ina uwezo wa kulinda amali za jamii zisipotee.

Pia huzilinda ili ziweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

Udhaifu

Fasili hii inaonesha udhaifu wa fasihi, yaani kutokuwa na uwezo wa kulinda amali za jamii. Amali hizo ni mila na desturi zilizopotea.

Sababu ni kwamba mila na desturi ndani ya jamii huenda na wakati. Hubadilika kulingana na mahitaji ya wakati huo.

  1. Fasihi ni hisi:

Dhana hii ilimaanisha kwamba msanii anapoleta kazi ya fasihi, ni lazima awe ameguswa na jambo fulani. Ndipo aweze kuandika kazi hiyo.

Udhaifu

Je, ni mara ngapi mwanafasihi ataguswa ndipo aweze kuandika kazi ya fasihi?

Je, ni mwandishi pekee ndiye anayetakiwa kuguswa?

Ukweli ni kwamba si kazi zote zinazoandikwa zinatokana na mguso unaompata mwandishi.

  1. Fasihi ni kielelezo cha kisanaa:

Fasihi inatazamwa kama ubunifu au ufundi wa aina fulani unaojidhihirisha katika maandishi.

Udhaifu

Fasili hii huzingatia zaidi utoaji wa burudani tu.

Haizungumzii lolote kuhusu uelimishaji wa nini kifanyike juu ya tatizo alilolionesha msanii.

  1. Fasihi:

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha. Msanii huitumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa.

Fasihi huwa na umbo timilifu. Kwa mfano, kazi ya fasihi inaweza kuwa tamthiliya (igizo), hadithi au ushairi.

Uhai wa lugha katika kazi ya fasihi huongeza mvuto.

Lugha inaweza kupewa uhai huo kwa kutumia tamathali za semi kama vile tashibiha, tasfida, sitiari, kejeli, dhihaka, balagha, kijembe n.k.

Vipengele vingine vinavyotawala ufasihi ni uundaji wa wahusika, matumizi ya picha, mandhari, utendaji n.k.

Mfano

Mtoto aloumbika, mara mtoto laini

Shingo yake ya birika, watabasamu moyoni

Kweli asali tamu, wajua ilivyoundwa

Hapa unaweza kupata ujumbe kwa kupitia maswali mbalimbali

  • Mhusika ameumbwaje?
  • Shingo yake inafananishwa na nini?
  • Uzuri wa mtoto umeoneshwaje?
  • Asali imetumika kwa sababu gani?
  • Swali lililo kwenye mstari wa mwisho limeulizwa kwa sababu gani?

Madhumuni Ya Fasihi

Fasihi ni kazi inayotokana na jamii na ipo kwa ajili ya jamii.

Kazi ya fasihi na fasihi yenyewe huathiriwa na mazingira na maendeleo ya jamii.

Madhumuni Ya Fasihi

Fasihi hushughulikia mahusiano ya jamii. Kwa hiyo fasihi

  1. Hueleza ukweli wa maisha ya jamii.
  2. Hujenga udadisi wa kujielewa na kuelewa watu wengine.
  3. Huendeleza, hudumisha na kurithisha utamaduni wa jamii.
  4. Huonyesha jamii njia na mitindo mbalimbali ya kujieleza.
  5. Huburudisha kupitia mvuto uliomo ndani ya LUGHA, MUUNDO na MAUDHUI yake.
  6. Huijenga jamii kifikra na kisiasa. Hii huiwezesha kutoa maamuzi na kuwa na msimamo wa maamuzi hayo.

Dhima Ya Fasihi

  1. Huelimisha:

Hufanya hivyo kupitia maonyo (huonya). Huhamisha ukweli, huelekeza, hutoa mawaidha na huonyesha mwanga wa migogoro.

  1. Huburudisha:

Hufanya hivyo kupitia maliwazo (huliwaza). Hufundisha, hubembeleza, huhamasisha na hutuliza mawazo.

Dhima Ya Mwanafasihi

  1. Huelimisha:

Hufanya kazi ya kuelimisha kwa kukosoa, kutia hamasa, kuonya, kueneza mawazo na kueneza falsafa za jamii.

  1. Huburudisha.
  1. Huhifadhi na kurithisha amali za jamii.
  1. Hudumisha na kuendeleza lugha.

Matumizi Ya Fasihi

Matumizi ya fasihi hutegemea sana msimamo na mikabala ya wasimulizi na waandishi.

Kwa kawaida mtunzi hujiambatisha na tabaka lake. Ndiyo maana

  1. Mwandishi wa tabaka la watawala hutetea tabaka hilo kwa kulisifia.
  2. Mwandishi wa tabaka la wakandamizwaji huandika maudhui ya kujikomboa, yaani kulikomboa tabaka lake.
  3. Mtunzi anayetokana na udhamini hulazimishwa kutetea tabaka lisilo lake. Hufanya hivyo kwa hofu, kwa malipo, au kwa yote mawili pamoja.

Uhuru Wa Mtunzi Wa Kazi Za Kifasihi

Uhuru wa mtunzi ni hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi kutoa mawazo na hisia zake kwa jamii bila kupingwa na tabaka lolote.

Au ni hali ya kutunga au kuandika kazi yake bila kushinikizwa na mtu, watu au taasisi yenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kitawala.

Mtunzi wa kazi ya fasihi anakuwa na uwezo binafsi wa kufanya maamuzi juu ya fani na maudhui ya kazi yake.

Nguzo Kuu Za Dhana Ya Uhuru Wa Mtunzi Wa Kazi Za Kifasihi

  1. UTASHI:

Utashi ni hali ya kuamua, kuazimia au kukusudia jambo bila kushurutishwa au kuyumbishwa.

Moja ya dhima ya mtunzi ni kuiamsha jamii itambue unyonyaji, ukandamizaji na uonevu uliomo ndani yake. Hii huiwezesha jamii kuchukua hatua ya kukomesha hali hizo.

Mtunzi anapotimiza dhima hii, anaweza kukabiliana na tabaka kandamizi.

Hapo ndipo utashi wake unaweza kumwelekeza katika mojawapo ya njia hizi

  • Kusonga mbele na jukumu lake.
  • Kuwa kasuku wa kusifia tabaka tawala au kandamizi, kwa kufunika maovu ya tabaka hilo.
  • Kujiondoa kabisa kwenye ulingo wa fasihi.

Mfano: Ngugi wa Thiong'o aliwahi kuhukumiwa na serikali ya Kenya alipoandika tamthiliya ya "THIS TIME TOMORROW", akikosoa uovu wa tabaka tawala. Utashi umemfanya aendelee na msimamo wake ule ule hadi leo.

  1. FALSAFA:

Mwandishi anapaswa kuwa na falsafa moja inayoeleweka. Falsafa hiyo huyafanya maandishi yaonekane kama kazi moja yenye mwelekeo maalum.

Mwandishi akipoteza uhuru, huweza kuyumbishwa kirahisi.

Mfano: Mwandishi anaweza kuandika kuhusu ujamaa leo, kesho akaandika kuhusu mapenzi, kesho kutwa akaandika kuhusu ubepari.

Mwandishi asiye huru ni mtumwa wa hali mbalimbali za maisha. Hali hizo humfanya ayumbeyumbe huku na kule.

  1. SANAA:

Mwandishi anapaswa kuwa na weledi wa misingi ya aina ya utunzi wa sanaa anayotaka kuitumia kufikisha ujumbe wake.

Mfano: Akitaka kufikisha ujumbe kwa njia ya riwaya, ni lazima ajue barabara misingi ya uandishi wa riwaya.

Vinginevyo msanii hatakuwa na uhuru wa kisanaa. Hatakuwa na namna yenye nguvu ya kusema kile alichonacho.

  1. LUGHA:

Msanii asiye na weledi wa lugha na misingi ya lugha anayoitumia, ni lazima atajikuta amefungwa.

Hatakuwa na uhuru wa kusema kile kilichomo nafsini mwake kwa ufasaha na kwa mafanikio.

Dhima Ya Uhuru Wa Mwandishi

  1. Mwandishi awe huru kuikosoa jamii au tabaka lolote linalokwenda kinyume na maadili ya jamii.
  2. Mwandishi awe na falsafa inayoeleweka na utashi.
  3. Kuikomboa jamii kutoka katika fikra mbovu za kukandamizwa, kunyonywa na kuonewa na tabaka tawala.
  4. Uandishi wa kikasuku kupungua.
  5. Unaifanya fasihi kuwa chombo cha kuikomboa jamii KIUCHUMI, KISIASA, KIUTAMADUNI, KIJAMII NA KIFIKRA.
  6. Mwandishi anakuwa na uhuru wa kuisukasuka jamii bila matatizo yoyote.

Udhamini

Udhamini wa kazi ya fasihi ni kitendo cha mtu au chombo fulani kukubali kufadhili au kugharamia kazi ya mtunzi.

Lengo ni kazi hiyo iweze kuchapishwa, kisha isambazwe mahali mbalimbali hadi iwafikie walengwa.

Aina Za Udhamini

  1. Udhamini wa kishawishi:

Huu ni udhamini ambao mdhamini humshawishi mtunzi wa kazi ya fasihi. Anamshawishi kwa fedha au kwa masilahi mengine.

Hali hii humfanya mtunzi kuingia katika udhamini kwa hiari yake.

  1. Udhamini wa nguvu:

Huu ni udhamini unaotolewa na vyombo vya dola. Mtunzi huingia katika udhamini huu kwa lazima.

Dola hudhamini watunzi ili waandike kile ambacho dola imeagiza.

Hivyo mtunzi huandika na kuingia katika udhamini huu kwa nguvu ya dola. Anafanya hivyo kwa kuogopa kwamba kazi zake zinaweza kuzuiwa au kuondolewa kabisa katika ulimwengu wa fasihi.

  1. Udhamini wa mtunzi mwenyewe:

Huu ni udhamini ambao mtunzi mwenyewe hujisimamia binafsi. Hugharamia gharama zote za uhariri, uchapaji na usambazaji wa kazi zake.

Mara nyingi hufanywa na watunzi wenye uwezo.

  1. Udhamini wa makampuni ya uchapishaji:

Yapo makampuni mbalimbali ya uchapishaji yanayopokea miswaada. Kisha yanaithamini, yanaihariri, yanaichapisha na kuisambaza kwa wasomaji.

Makampuni haya hutoa fedha kwa ajili ya mambo hayo yote. Yanatarajia kurudisha fedha hizo pamoja na faida wakati wa mauzo ya kazi husika.

Dhima Ya Udhamini Wa Kazi Ya Fasihi

  • (a) Kuwawezesha watunzi wasio na uwezo wa kifedha kuchapisha kazi zao na kuzifikisha kwa hadhira.
  • (b) Kuibua vipaji vya watunzi. Kwa kawaida kuna watu wengi wenye vipaji, lakini hawavitendei haki kwa kuwa hawana uwezo wa kuendelea na hatua za mbele kama uchapishaji na usambazaji.
  • (c) Mdhamini hujitangaza. Udhamini humwezesha mdhamini kujitangaza kibiashara, au kupata heshima miongoni mwa jamii.
  • (d) Ni njia ya kuleta kipato kwa wadhamini. Kwa mfano, makampuni ya uchapishaji.
  • (e) Kuwapatia watunzi fedha za haraka kabla na baada ya kazi kuuzwa.
  • (f) Kuwainua watunzi chipukizi kwa kuwawezesha kufikisha kazi zao kwa hadhira, ili ujumbe uliokusudiwa uwafikie waliokusudiwa.
  • (g) Kuwafanya watunzi chipukizi kufahamika.

Athari Za Udhamini Wa Fasihi

Udhamini wa kazi za fasihi una athari mbalimbali. Zifuatazo ni baadhi ya athari hizo

  • (a) Mtunzi huandika kazi yake kulingana na matakwa ya mdhamini. Kwa mfano, udhamini ukitolewa kwa kazi zilizo katika lugha ya Kiingereza, msanii anayetumia Kiswahili kuandika kazi zake hawezi kufaidika na udhamini huo.
  • (b) Mtunzi hushindwa kuandika mambo kulingana na mtazamo wake halisi juu ya jamii inayomzunguka.

Mtunzi hushindwa kukosoa uovu, hasa unapomhusu mdhamini wa kazi yake. Kwa mfano, serikali au tabaka tawala.

  • (c) Fasihi pendwa hukua, kwa mfano riwaya pendwa. Fasihi dhati hudumaa, kwa mfano riwaya dhati. Hali hii inatokana na msukosuko wa kibiashara.

Fasihi pendwa huuzwa kirahisi sokoni kwa kuwa ina maudhui yenye msisimko. Mifano ni upelelezi, usambazaji, mauaji, mapenzi n.k.

  • (d) Mapana ya kijiografia na utafiti wa fasihi kabla ya kuandikwa hutegemea uwezo wa kifedha wa mdhamini.
  • (e) Uhuru wa mwandishi hutoweka.