Utungaji wa kazi za fasihi
Dakika 3 za kusoma ·
Yaliyomo
Utungaji wa ushairi wa kimapokeo
Mtungaji wa mashairi ni binadamu, kwa hiyo hana uwezo wa kuyachora maisha yote kwa mapana na marefu. Hivyo basi mshairi anapotunga shairi jambo la kwanza ni kukagua jambo moja la kuzungumzia, Mfano; umasikini, matabaka, mvutano kati ya ukale na usasa nk.
Hatua za utungaji wa ushairi.
- Kuwa na jambo la kuzungumzia (mada).
- Mshairi lazima ajue hadhira yake anayoitungia ushahirihuo.
- Mshairi lazima awe na sababu ya kutunga ushairi.
Kanuni za utunzi wa mashairi ya kimapokeo
Mashairi ya kimapokeo ni mashahiri ambayo yalianza kale sana. Mtunzi wa aina hii ya mashairi huitwa malengo, Mashairi haya hutungwa kwa kufuata kanuni maalum.
Shairi la kimapokeo linatakiwa liwe na :-
KICHWA; Kichwa cha shairi hutokana na jambo linalojadiliwa katika shairi, Kichwa hicho huandikwa kwa maneno machache yasiyozidi matano.
BETI ; Vifungu vya maelezo au mistari katika shairi huitwa beti . idadi ya beti hutegemea utashi wa mtunzi, hata hivyo shairi zuri ni lile ambalo idadi ya beti zake hazizidi kumi.
MUUNDO ; Muundo wa shairi ni namna shairi lilivyogawanyika katika beti zenye idadi maalum ya mistari. Mfano
Mistari 4; Tarbia
Mistari 5; Takhamisa nk
MIZANI ; Ni silabi zinazounda mistari ya beti za mashairi.
Mfano: Si leo toka zamani, mkulima mtu duni
Ana tabu maishani, tena hapewi thamani
Yafaa tutizameni, kasha tuyachunguzeni
Hivyo basi, ubeti huo una mistari yenye mizani 16 kila mmoja, kama ifuatavyo;
Si Le O To Ka Za Ma Ni M Ku Li Ma M Tu Du ni
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Mbinu za kupata ulinganifu wa mizani katika mistari ya mashairi ni pamoja na kutumia maneno ya mkato. Mfano: “alosema” badala ya aliyesema.
VINA ; Ni silabi zinazofanana sauti katika shairi, katika shairi la kimapokeo, vina hutokea katikati na mwishoni mwa kila mstari wa ubeti wa shairi au utenzi.
KITUO ; Ni ubeti mstari wa mwisho katika kila ubeti wa shairi. Kwa maana nyingine hujulikana kama kibwagizo.
UTOSHELEZI ; Utoshelezi wa ushairi ni namana kila ubeti wa shairi unavyotoa ujumbe unaoeleweka bila kutegemea ubeti mwingine, Mfano.
MUWALA ; Ni mtiririko wa maelezo ya shairi ambayo yanatolewa kwa kuzingatia utangulizi, kiini na mwisho, na si kiini utangulizi na mwisho au mwisho, utangulizi na kiini.
LUGHA YA KISHAIRI ; Lugha nzuri ya shairi ni ile ambayo in a matumizi ya misemo na semi tofauti kama vile nahau, lakabu , methali, mafumbo, tamathali za semi, picha, maneno ya mkato na uchezeshaji wa maneno.
Mfano: wa ubeti unaoonyesha namna ya uchezeshaji wa maneno
Oa utukuze cheo, na jina lipate kuwa,
Oa upate mkeo,aambiwe meolewa,
Oa kama waoao, moyo usikie ngowa,
Oa ujue kukuwa, mpendane na mkeo
(Kutoka Ijaribu na ulikarabati, OUP Kenya, 2006)
URARI WA MISTARI ; Hii ni namna kila mstari katika beti unavyotokea katika nafasi yake sahihi kulingana na maelezo yaliyomo katika mstari huo. Yaani ubeti hupangiliwa kwa kufuata mtiririko wa mawazo kutika wazo la kwanza hadi la mwisho.
Taswira Au Picha
Ili shairi liweze kuwa na mvuto, ni muhimu kutumia lugha yenye picha. Hii ni mbinu ya kuunda picha yenye ya jambo linaloongelewa katika shairi.
Mfano: Njiwa nilipompata, moyo ulifurahika
Kwani tabu sikupata, mazoea aliweka
Kadumu miaka sita, bila kuleta mashaka
Njiwa ameshanitoka, nipate wapi mwingine
Katika ubeti huo, neno njiwa kwa maana ni mwanamke.
RIDHIMU; Ni mapigo asilia ya lugha
Ridhimu ya ushairi na muziki hutokana na mlingano wa vipande vya mapigo ya lugha ya sauti. Vpande hivyo vya sauti ni lazima vilingane kabisa.
MSISITIZO ; Hii ni hali ya kushadidiwa katika utungo. Msisitizo unaweza kuwa na wima au na ulalo.
Maswali
1.Shairi bora lina sifa zipi?
2.Kichwa cha shairi hutegemea nini?
3.Eleza tofauti iliyopo kati ya Tathnia na Tathlitha.
4.Ngonjera ni mashairi pia ni maigizo.Toa sababu.
5.Nini tofauti kati ya mashairi ya kimapokeo na mashairi ya kisasa?
