Ufahamu…
Dakika 3 za kusoma ·
Yaliyomo
Ufahamu
Ufahamu ni hali ya kulijua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea kwa ufasaha bila kupoteza maana yake ya msingi.
Ufahamu unahusisha kuona, kusikiliza na kusoma.
Dhima au kazi ya ufahamu
- Ufahamu huelimisha.
- Ufahamu hukuza ustadi katika kusoma, kusikiliza na kutafakari.
- Huendeleza ujuzi wa lugha katika vipengele vya msamiati, sarufi na matumizi.
- Huleta burudani kwa msomaji au msikilizaji.
- Huokoa muda na kupunguza gharama.
A: Ufahamu Wa Kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni ule ambao mhusika anapata taarifa kwa kusikiliza habari fulani.
Habari hiyo inaweza kupatikana kwa kusikiliza (kusimuliwa) au kwa kusomewa.
Ili kupata habari inayosikilizwa au inayosomwa, msikilizaji lazima azingatie yafuatayo
- Kuwa makini kwa kile kinachosimuliwa au kusomwa.
- Kuhusisha mambo muhimu na habari husika.
- Kujua matamshi ya mzungumzaji.
- Kubainisha mawazo makuu.
Msikilizaji atalazimika kuwa katika hali ya utulivu. Mawazo yako yote yanatakiwa yawe katika mazingira hayo ili neno lisikupite.
Hata kama una matatizo mengi, usiyafikirie wakati unapotakiwa kusikiliza.
Ikiwezekana, mwangalie usoni mtu unayemsikiliza.
Mbinu za kujibu maswali yanayotokana na habari ya kusikiliza
- Kubaini mawazo makuu.
- Kubaini maana ya maneno na misemo.
- Kusikiliza kwa utulivu.
Ufupisho Wa Habari Ya Kusikiliza
Ufupisho ni maelezo mafupi yaliyoandikwa kutokana na habari ndefu bila kupoteza maana ya msingi ya habari hiyo.
Wakati wa kufupisha habari, ni muhimu kuzingatia njeo, kauli na nafsi kama ilivyotumiwa katika matini ya awali.
Hatua za kufupisha habari
- Kuisoma au kuisikiliza habari kwa makini ili kuielewa vizuri.
- Kutambua au kubaini mawazo makuu yanayojitokeza katika kila aya.
- Kuyaunganisha mawazo makuu, kisha kuandika au kuelezea habari hiyo kwa maneno yako mwenyewe.
- Kuhesabu idadi ya maneno ya ufupisho ili kuyapunguza ikiwa yanazidi idadi inayotakiwa.
- Kuandika idadi ya maneno mwisho wa ufupisho, upande wa kulia chini kidogo.
B: Ufahamu Wa Kusoma
Ufahamu wa kusoma ni ule unaotokana na njia ya kusoma. Kwa mfano, kusoma kitabu, gazeti na kipeperushi.
Usomaji upo wa aina kuu mbili: kusoma kwa sauti na kusoma kimya.
Kusoma kwa sauti
Ni aina ya usomaji ambayo msomaji hutoa sauti. Msomaji hupata ujumbe kwa kuweza kutamka kwa lafudhi ya Kiswahili sahihi.
Msomaji hana budi kukwepa athari za lugha nyingine katika usomaji wa Kiswahili.
Kusoma kimya
Ni njia ambayo msomaji anapitisha macho kwenye maandishi kwa haraka bila kuzingatia kwa kina.
Kwa kusoma kimya, msomaji anasoma haraka. Mfano: usomaji wa magazeti na majarida.
Kusoma kwa makini
Huu ni usomaji kimya ambao msomaji huzingatia maana ya kila neno, sentensi na aya kwa makini.
Lengo la usomaji kwa njia hii ni kupata uelewa kamili na wa undani.
Usomaji huu huhitaji muda, utulivu katika mawazo na mazingira yanayomzunguka.
Mfano: mwanafunzi akipewa kazi ya kuchambua kitabu cha hadithi, atalazimika kusoma kimya na kwa makini, ukurasa hadi ukurasa.
Mbinu za kujibu maswali ya ufahamu
- Kuwa mtulivu. Fikira zote ziwe kwenye kile unachokisoma.
- Kusoma kwa makini habari au matini husika.
- Kuelewa swali.
Aina Za Maswali
Maswali marefu
Haya ni maswali yanayomtaka mtahiniwa kujieleza. Mara nyingi maswali ya aina hii hujitokeza zaidi kwenye vipengele vinavyohusiana na utungaji au ufahamu.
Maswali mafupi
Haya ni maswali yasiyofikirisha sana. Aghalabu maswali ya aina hii huulizwa kwa kutumia mitindo tofauti.
Mfano
- a. Kweli au si kweli.
- b. Kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
- c. Kuoanisha.
- d. Kuelewa maana ya maneno na misemo.
- e. Kujibu kwa ufupi.
Maswali
- Eleza maana ya ufahamu.
- Taja dhima za ufahamu.
- Ufupisho ni nini?
- Orodhesha
- Taja mbinu za kujibu maswali ya ufahamu.
