Kiswahili · Kidato 4

Uhakiki wa kazi za fasihi andishi

Dakika 25 za kusoma ·

Yaliyomo

Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi Andishi

Dhana Ya Uhakiki

Uhakiki ni shughuli ya kupima kazi za fasihi kwa undani. Lengo ni kuona namna kazi hiyo ilivyo katika maudhui na fani yake. Pia mhakiki huelezea jinsi kazi hiyo inavyohusiana na jamii.

Mhakiki huonyesha dhamira, migogoro, ujumbe, mtazamo, msimamo na falsafa. Kisha hubainisha uzuri au udhaifu wa kazi hiyo. Pia hueleza sababu za uzuri na udhaifu huo.

Muhimu kuzingatia

  • Kuhakiki ni kitendo cha kuchambua kazi ya fasihi.
  • Uhakiki ni hali ya kuchambua kazi ya fasihi.
  • Mhakiki ni mtu anayechambua kazi ya fasihi.
  • Tahakiki ni kitabu kilichoandikwa na mhakiki, ambacho ndani yake kuna uhakiki.

Dhima Au Kazi Ya Mhakiki

  • Huwawezesha wasomaji kuielewa vizuri kazi ya mtunzi. Mfano ni kazi ambazo zimetumia lugha ngumu.
  • Hukuza utunzi bora wa kazi za fasihi.
  • Hukuza uelewa wa mhakiki.

Nafasi Au Umuhimu Wa Mhakiki

Mhakiki ni mtu anayetegemewa sana na watunzi wa kazi za fasihi pamoja na hadhira.

Huwaonyesha watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao.

Sifa Za Mhakiki Bora

  • Awe anafahamu kwa undani nadharia mbalimbali za fasihi. Anapaswa kujua kwa undani fani, maudhui na vipengele vilivyopo ndani yake.
  • Awe anafahamu vyema historia ya mwandishi asilia wa kitabu husika. Pia ajue historia ya jamii anayotoka na anayoiandikia.
  • Awe amesoma tahakiki za watu wengine waliochambua kazi anayotaka kuifanyia uhakiki.
  • Asiwe mtu wa kuyumbishwa na waandishi, maneno ya wahakiki au watu wengine.

Hatua Za Uhakiki

  1. Kuisoma kazi ya fasihi.
  1. Kuainisha mambo muhimu yaliyojitokeza.
  1. Kutoa tathmini, yaani kueleza ubora na udhaifu wa kazi inayohusika.

Vigezo Vya Uhakiki

Vigezo ni mambo mbalimbali yanayochunguzwa na mhakiki katika kutoa hukumu ya kazi ya fasihi. Vigezo hivyo ni:

  • Ukweli wa mambo yanayoelezwa. Mhakiki atajiuliza: Je, ni kweli jambo hilo linafanyika katika jamii?
  • Uhalisia wa watu, mazingira na matukio katika jamii. Mhakiki atajiuliza: Je, jamii hii ina watu wanaotenda kama wale wahusika walio katika kazi hii ya fasihi?
  • Umuhimu wa kazi ya fasihi kwa jamii inayohusika. Mhakiki anaweza kujiuliza maswali yafuatayo:
  • Je, ni kweli kuwa wanakijiji wana maisha bora kuliko wa mjini?
  • Je, wanakijiji hawabughudhiwi na wezi, waporaji au wahalifu wengine?
  • Je, kijana anapokimbilia mjini ana uhakika wa kupata kazi?
  • Je, mwandishi anashauri nini licha ya kusema vijana wabaki vijijini? Na kadhalika.

Maswali mengine ya kujiuliza

  • Je, wahusika wamechorwaje?
  • Je, wana uhalisia?
  • Je, mpangilio wa maneno unavutia hadhira?

Uhakiki Wa Tamthiliya

Tamthiliya ni mchezo wa kuigiza. Unafanyika jukwaani au mahali popote pa wazi, kama vile kwenye sherehe au kwenye burudani yoyote.

Uhakiki wa tamthiliya huchunguza fani na maudhui.

A: Fani

Fani ni jumla ya mbinu, ufundi na upekee anaoutumia mwandishi au msanii kuwasilisha ujumbe.

Vipengele vya fani ni hivi

  • Muundo:

Muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi. Kimuundo, tamthiliya hugawanywa katika maonyesho. Onyesho likiwa refu, hugawanywa katika sehemu kadhaa. Licha ya kugawanyika katika maonyesho, muundo wa tamthiliya unaweza kuwa sahili, rejeshi au changamano.

  • Mtindo:

Mtindo ni namna mwandishi anavyotumia mbinu ili kubaini vionjo vya kazi. Mtindo wa tamthiliya huwa wa dayolojia, yaani mtindo wa majibizano. Majibizano hufanyika kati ya watu wawili au zaidi. Huongea kwa zamu, kwa kufuata utaratibu wa kujibizana.

  • Wahusika:

Kama ilivyo kwa kazi nyingine, tamthiliya lazima iwe na wahusika. Wahusika wanawakilisha wanajamii halisi waliomo katika jamii inayojadiliwa, kwa matendo, kazi na tabia. Hapa tunapata wahusika wakuu, wajenzi na wadogo. Matendo na kauli za wahusika zinaweza kuonyesha nafasi ambayo kila mhusika anaiwakilisha.

  • Matumizi ya lugha:

Matumizi ya lugha katika tamthiliya huhusisha misemo, methali, nahau, tamathali za semi na vitendawili. Lugha ya tamthiliya huwa ya mkato. Wakati mwingine hutumia lugha ya ushairi katika sehemu chache.

  • Mandhari:

Tamthiliya inaweza kuwa na mandhari halisi au isiyo halisi. Kwa hiyo mhakiki hutakiwa kuchunguza na kuonyesha mandhari ya tamthiliya. Pia anabainisha kama ni mandhari halisi au ya kubuni.

  • Ujenzi wa taswira:

Katika uhakiki wa tamthiliya yenye matumizi ya taswira, mhakiki hutakiwa kuchunguza na kuonyesha mambo haya:

  • Aina za taswira zilizotumika.
  • Dhana zinazomaanishwa na taswira hizo.
  • Usahihi wa uhusiano wa taswira hizo na dhana zinazowakilisha.
  • Jina la kitabu:

Tamthiliya yoyote lazima iwe na jina. Jina hilo lazima lihusiane na tamthiliya yenyewe kimaudhui au kifani. Kwa hiyo mhakiki hutakiwa kuchunguza jina la tamthiliya na jinsi linavyohusiana na tamthiliya yenyewe.

B: Maudhui

Maudhui ni jumla ya mawazo yote ya mwandishi katika kazi ya fasihi.

Maudhui hujumuisha dhamira, migogoro, ujumbe, mtazamo, msimamo na falsafa.

  • Dhamira:

Dhamira ni wazo kuu ambalo mtunzi analiwasilisha kwa jamii. Katika uhakiki wa tamthiliya, mhakiki hutakiwa kuchunguza ni wazo gani muhimu kuliko yote linalojitokeza katika tamthiliya inayohusika.

  • Migogoro:

Migogoro ni hali ya mivutano au migongano inayojitokeza kati ya mhusika mmoja na mwingine, au tabaka moja na lingine. Hutokana na kutokubaliana juu ya mambo mbalimbali. Mambo hayo yanaweza kuwa ya kisiasa, kiuchumi au kiutamaduni. Wakati wa kuhakiki kipengele hiki, mhakiki anatakiwa kuhakiki wahusika wa mgogoro, chanzo cha mgogoro na hatima ya mgogoro.

  • Ujumbe:

Ujumbe ni jumla ya taarifa ambazo mtunzi wa kazi ya fasihi analenga kuziwasilisha kwa jamii. Taarifa hizo hulenga zaidi kutoa ushauri, maono na kadhalika. Mhakiki anatakiwa kubaini ni mambo gani mtunzi angependa jamii iyatekeleze. Hapo ndipo hubaini ujumbe wa tamthiliya husika.

  • Mafunzo:

Mafunzo ni jumla ya mambo ambayo msomaji wa kazi ya fasihi hujifunza baada ya kuisoma.

  • Mtazamo:

Mtazamo ni namna mtunzi wa kazi ya fasihi anavyojadili jambo au mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika kazi hiyo. Kuna aina mbili za mitazamo:

  • Mtazamo wa kidhaifu: Husuluhisha jambo kwa amani.
  • Mtazamo wa kiyakinifu: Husuluhisha jambo kwa njia zote.

Katika uhakiki wa mtazamo, mhakiki huchunguza kama mambo anayojadili mtunzi yanahalisika au hayahalisiki.

  • Msimamo:

Msimamo ni mawazo au mwelekeo wa jumla wa mawazo yaliyojadiliwa katika kazi ya fasihi. Msimamo wa mtunzi unaweza kuwa wa kimapinduzi au wa ukasuku.

Msimamo wa kimapinduzi ni kujadili jambo katika uhalisia wake.

Msimamo wa ukasuku ni kujadili jambo bila kuzingatia ukweli wake.

Kwa hiyo mhakiki hutakiwa kuchunguza kama msimamo wa mtunzi ni wa kimapinduzi au wa kikasuku.

  • Falsafa:

Falsafa ni imani ya mwandishi. Mhakiki hujadili kile anachoamini mwandishi kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika kazi ya fasihi.

Uhakiki Wa Tamthiliya

Jina la kitabu: ORODHA

Mtunzi: STEVE REYNOLDS

Mchapishaji: MACMILAN AIDAN, DAR ES SALAAM.

Utangulizi

Tamthiliya ya Orodha ni tamthiliya inayohusu suala zima la ugonjwa wa UKIMWI na madhara yake katika jamii.

Mwandishi anaweka wazi kuhusu gonjwa hili.

Mhusika mkuu Furaha anaathirika na gonjwa hili na kufariki dunia.

Kimaudhui, tamthiliya hii imesawiri maisha ya sasa ya jamii ya Watanzania, kwani ugonjwa huu bado ni tishio.

Kwa upande wa fani

  • Mwandishi amewaumba vyema wahusika wake.
  • Muundo wake unamvutia msomaji kujua ni nini kingeendelea mbeleni.
  • Ameteua lugha nzuri ya kisanaa.

Haya yote yanajielekeza katika uchambuzi tutakaoufanya.

Muundo

Mwandishi ametumia muundo changamano.

Katika sehemu ya 1 na 2 anatuonesha mazishini, ambapo yanafanyika mazishi ya Furaha.

Sehemu ya 3 hadi 20 anaanza kutueleza juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo chake. Huu ni msago, au muundo sahili.

Halafu sehemu ya 17 hadi 19 na ya 20 anatuonesha mzozo wa orodha na hatima ya mazishi ya Furaha.

Mwandishi ameweka kazi yake katika onyesho moja.

Katika onyesho hilo ameweka sehemu ndogondogo ishirini. Sehemu hizo zinajengana kukamilisha tamthiliya nzima.

Sehemu Za Tamthiliya

  • Sehemu ya kwanza: Inaanza kwa kuonesha vifani vinne vimeganda. Katika kifani cha kwanza, wahusika wameganda katika mikao inayotambulisha wasifu wao. Kifani cha pili kinaonesha wagonjwa wakiwa katika mateso. Kifani cha tatu kinaonesha wagonjwa wakiwa katika maumivu makali sana.
  • Sehemu ya pili: Hapa inaelezwa juu ya siku ya msiba wa Furaha. Mama yake Furaha anawaeleza watu kuwa Furaha aliacha orodha ambayo alitaka isomwe hadharani katika mazishi yake. Suala hili linazua mgogoro na hofu kuu kwa watu. Padre James anaweka juhudi kuzuia barua isisomwe.
  • Sehemu ya tatu: Tunaonyeshwa maisha ya Furaha nyumbani kwao, na baba, mama na wadogo zake. Baba yake anaonekana kutofurahishwa na mwenendo wa Furaha. Anamkanya kwa maneno makali ya laana, kama vile kwamba hatapata mtu wa kumuoa. Anamuasa Furaha aonyeshe mfano mzuri kwa wadogo zake.
  • Sehemu ya nne: Furaha kwa mara ya kwanza anatoroka nyumbani kwao usiku wa manane pamoja na Mery kwenda baa. Mdogo wake anabaini kitendo hicho na anatishia kushtaki kwa wazazi. Hata hivyo, Furaha anamtishia kumchinja.
  • Sehemu ya tano: Mery na Furaha wanaonekana wako baa wakinywa pombe na kucheza na wanaume. Hapa Furaha anajifunza mambo mapya mabaya, kama vile ulevi, kupitia rafiki yake Mery. Pia anaanza mahusiano ya mapenzi na wanaume, kwa mfano Bw. Ecko.
  • Sehemu ya sita: Furaha anamwendea Padre James kwa ajili ya maungamo, kwani alikunywa pombe na kulala na wanaume. Padre James anamwambia aende kesho yake katika chumba chake cha kujisomea nyuma ya kanisa, na kwamba taa zitakuwa zimezimwa kuficha utambulisho. Hapa ndipo Furaha anapozini na Padre, kwani Padre alishikwa na tamaa.
  • Sehemu ya saba: Baba na Mama Furaha wanamkanya Furaha kuhusu tabia yake ya umalaya na ulevi. Furaha anaomba msamaha.
  • Sehemu ya nane: Furaha anakutana na Kitunda anapokwenda sokoni, ametumwa na mama yake. Anamkuta Kitunda akisikiliza muziki, naye Furaha anashawishika. Kitunda anamshawishi zaidi, hata avute bangi, ila Furaha hakubali. Pia wanazungumzia juu ya jiji la Dar es Salaam. Habari hizo zinampagawisha Furaha na anatamani sana kwenda.
  • Sehemu ya tisa: Salim anarudi kutoka masomoni Dar es Salaam. Anaonana na mpenzi wake wa zamani, Furaha. Wanasalimiana kwa hamu na furaha tele.
  • Sehemu ya kumi: Salim na Furaha wanakutana na kuelezana habari za kitambo, kwani walitengana kwa muda mrefu. Wanapanga mipango juu ya mahusiano yao.
  • Sehemu ya kumi na moja: Wanakijiji wanazungumzia tabia ya umalaya ya Furaha. Pia wanazungumzia mahusiano ya Furaha na Salim. Hawapendezwi na tabia ya Furaha, na wanaamua kumtaarifu mama yake.
  • Sehemu ya kumi na mbili: Mama Furaha anachukua jukumu la kumhoji mwanawe juu ya tabia yake. Furaha hakubaliani na lolote. Hali ya Furaha inaanza kudhoofu na mama yake anaingiwa hofu.
  • Sehemu ya kumi na tatu: Furaha yupo sebuleni akisali. Baba yake anamuonya zaidi na kumshauri aolewe na Salim, kwani ni kijana mzuri anayefaa.
  • Sehemu ya kumi na nne: Hali ya Furaha inazidi kutetereka. Anachukuliwa vipimo vya damu na kugundulika kuwa ana virusi vya UKIMWI. Hali hii inamshtua sana mama yake. Anamuhoji kama aliwahi kutembea na mwanaume yeyote, na anamweleza njia za kupata UKIMWI. Furaha anaanza kulia kwa kutambua kosa lake.
  • Sehemu ya kumi na tano: Wanakijiji wanapata habari juu ya kuumwa kwa Furaha na wanazieneza. Juma, Kitunda, Padre James, Salim na Bw. Ecko nao wanapata habari hizi. Wanaingiwa na hofu kubwa: je, wameambukizwa UKIMWI, au majina yao yamo kwenye orodha?
  • Sehemu ya kumi na sita: Salim anaamua kumtembelea Furaha nyumbani. Akiwa katika hali mbaya sana ya ugonjwa, Furaha anamweleza wazi Salim juu ya kuathirika kwake kwa UKIMWI. Salim anaingiwa hofu. Anamuomba Furaha barua yenye orodha kwa shauku, lakini hampatii. Hali hii inamuudhi Salim. Hapa ndipo Furaha anapokata roho.
  • Sehemu ya kumi na saba: Tunaelezwa juu ya juhudi za Bw. Ecko na Juma za kutaka kuiba barua yenye orodha katika chumba alicholazwa maiti ya Furaha. Hawafanikiwi. Familia ya Furaha inaamini kuwa kuna mizimu katika chumba cha maiti, kutokana na kelele za Juma, Bw. Ecko na Kitunda.
  • Sehemu ya kumi na nane: Padre James anaomba kusomewa barua hiyo kabla ya mazishi, lakini Mama Furaha anakataa. Anaamua kuitafuta mwenyewe sebuleni bila mafanikio.
  • Sehemu ya kumi na tisa: Ni asubuhi ya siku ya mazishi. Ecko, Juma na Salim wanaonekana wakitafuta suluhu ya namna ya kuzuia orodha isisomwe, lakini hawafanikiwi.
  • Sehemu ya ishirini: Ni siku ya mazishi, ambapo Mama Furaha anaisoma barua ya orodha. Padre James anajitahidi kumpinga Mama Furaha asiisome orodha, lakini hafanikiwi. Salim anapora barua na kuchana baadhi ya sehemu, lakini hiyo haiharibu kitu. Anaunga vipande na kusoma mbele ya wanakijiji wote. Ndani ya orodha hakuna jina la mtu yeyote lililotajwa. Kuna mambo yatakayosaidia kuuepuka UKIMWI.

Dhamira

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi

Hii ni dhamira kuu iliyojadiliwa katika tamthiliya hii.

Mwandishi analenga mapambano ya Ukimwi hasa katika maeneo ya vijijini. Huko elimu kuhusu ugonjwa huu bado haijafika vyema.

Anamtumia mhusika Furaha kutuonesha jinsi binti huyu mdogo wa kijijini anavyopata ugonjwa huu na hatimaye kufa. Furaha bila kujua alijiingiza katika mapenzi na wanaume tofautitofauti. Mfano ni Bwana Ecko, Padre James, Salim, Kitunda na wengine.

Mwandishi anaona kuna umuhimu wa jamii kueleweshwa vyema kuhusu mambo yanayopelekea kupatikana kwa ugonjwa huu hatari, kama vile kuwa na mahusiano na wapenzi wengi.

Mwandishi anapendekeza mambo ambayo anaona ni suluhisho la kuenea zaidi kwa ugonjwa huu. Mambo hayo ni:

  • uwazi na ukweli katika hili
  • kutolewa kwa elimu juu ya Ukimwi
  • uadilifu
  • uaminifu katika ndoa
  • ngono salama
  • upendo kwa wagonjwa wa Ukimwi
  • msamaha na welewa

Haya yanapitia katika barua ya Furaha aliyoiacha isomwe katika mazishi yake. Uk. 44-45

“Nawashukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika, kukua kama mtu; hata ninapokuwa ninakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna orodha ya vitu ambavyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama tafadhali wasomee watu wote orodha hii.”

Mmomonyoko wa maadili

Mmomonyoko wa maadili ni pale wanajamii wanapoenda kinyume na makubaliano ya jamii yao. Makubaliano hayo ni taratibu, kanuni, mila na desturi zao.

Mwandishi anaona kuwa mmomonyoko wa maadili ni kichocheo cha maovu katika jamii.

Anawatumia wahusika Mery na Furaha. Ni vijana wadogo kabisa, lakini wanajiingiza katika tabia zisizofaa. Jamii yao iliwasema juu ya hili kwa sababu walipotoka.

Wazazi wa Furaha wanalipigia kelele suala hili, lakini kijana wao tayari alishaharibika. Mfano ni uk. 11, ambapo baba Furaha analaumu tabia ya Furaha. Anasema: “nilichokuwa nafahamu …. Hadi sasa Furaha… ni kwamba umekuwa ukitoroka nyumbani wakati wa usiku wa manane! Kuna jambo lingine ambalo anapaswa kulifahamu.” Anaendelea kusema: “kutoroka… bila ruhusa… baa wanaume.. wewe …. Malaya usiye na shukrani!”

Katika jamii ya leo, wazazi wanapewa ujumbe huu. Kuwaangalia watoto na kufuatilia nyendo zao ni jambo la msingi sana, hasa katika kipindi kigumu cha makuzi.

Kwa kufanya hivyo, jamii itaokolewa kutoka katika hatari ya kupoteza vijana wengi zaidi.

Uaminifu katika ndoa na mahusiano

Mhusika Bwana Ecko hakuwa mwaminifu kwa mkewe. Alikuwa malaya, na aliwaharibu mabinti wadogo waliokuwa kama watoto wake wa kuwazaa kwa umri.

Furaha anarubuniwa na kujikuta akitumbukia katika mapenzi na baba huyu. Mfano uk. 6, Bwana Ecko anasema: “karibuni kwenye baa yangu. Karibuni kae nami, wapenzi! Bia mbili kwa ajili ya wasichana warembo.”

Vilevile katika kitabu, Furaha anaelezwa kukosa uaminifu. Licha ya kutembea na Bwana Ecko, alijihusisha pia na wanaume wengine kama Kitunda na Salim. Hivyo alisababisha kuenea zaidi kwa ugonjwa huu.

Upotofu wa uaminifu ni janga katika jamii ya leo. Watu wazima badala ya kuwa mstari wa mbele kuwasaidia mabinti wadogo kimaadili, wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuharibu maisha yao.

Ni tabia mbaya na inapaswa kupigwa vita.

Umaskini na hali ngumu ya maisha

Katika kitabu tunaona kuwa sababu mojawapo iliyopelekea Furaha kupata maambukizi ya Ukimwi ni umaskini.

Furaha alitamani vitu vizuri. Hakujua madhara yake wala namna ya kuvipata. Alifurahia kuvipata na kujiona mwenye bahati.

Mery anasema uk. 7-8: “nimekwambia hawa jamaa ni burudani…hata yule mshamba Juma. Sikia, pata burudani na kuwa mwema, kwa Ecko. Anaweza kukununulia vitu vingi sana! Unadhani wasichana wadogo hapa mjini wanapataje viatu vipya, magauni na mabegi mapya ili wapendeze….wapendeze kiasi cha kuwavutia vijana wazuri wa kiume?”

Mwandishi anaonesha hili kwa sababu wasichana wengi hutumbukia katika janga la Ukimwi kutokana na umaskini.

Anaona kuna haja ya watu kuelimishwa kuwa kila jambo lina wakati wake, hasa kwa mabinti. Wanapaswa kushauriwa juu ya njia mbadala za kujipatia pesa, na si kujirahisisha kwa wanaume.

Kwa hiyo, elimu ya Ukimwi inapotolewa katika jamii, ni muhimu pia watu, hasa vijana, waelekezwe namna ya kujikomboa kiuchumi.

Wanapaswa kuona kuwa ngono si chanzo cha mapato. Wanapaswa kujibidisha ili wawe na vipato vya kukidhi mahitaji yao ya muhimu.

Ukosefu wa uadilifu katika kazi

Padre James katika kitabu ameonekana kutokuwa muadilifu kulingana na maadili ya kanisa akiwa Padre.

Anajisahau na kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na mtoto Furaha. Anajua kabisa kuwa ni kinyume na maadili na kazi yake ya upadre. Uk. 10: “Furaha alikuja kama alivyoagizwa….ee.. Ekaristi takatifu ilipatikana lazima uelewe jinsi ilivyo vigumu kwa mtu wa hadhi yangu na wadhifa wangu”

Ilitegemewa kuwa Padre James angekuwa mstari wa mbele kuiongoza jamii katika maadili mema. Lakini yeye ndiye anakuwa chanzo cha uharibifu wa maadili.

Suala hili lipo katika jamii. Wapo watu walioteuliwa kuwa kioo na taa ya jamii ili kumulika maovu. Lakini wao hutumia cheo hicho kama mwamvuli wa kujifunika na kufanya maovu kwa urahisi zaidi.

Mwandishi anaona hili ni tatizo, na anakemea vikali watu wa aina hii.

Umuhimu wa kusema ukweli na kuwa wazi

Hii ni suluhu mojawapo ambayo mwandishi anaamini kuwa ikitumika vyema ni kinga tosha dhidi ya Ukimwi.

Baadhi ya watu hujua wazi kuwa tayari ni waathirika, lakini hawapendi kuwa wazi na kusema ukweli. Hunyamaza na kuendelea kuambukiza wengine.

Mwandishi amemtumia mhusika Furaha na Mama Furaha kuwa mfano wa kuigwa. Hawakuona haya kusema ukweli kuhusu ugonjwa uliomuua Furaha. Wanalisema hili mbele ya wanakijiji wote, wakiwa na lengo la kuikomboa jamii yao.

Barua ya Furaha ni mfano tosha, uk. 44-45: “kondom, uaminifu, elimu, welewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha,…ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote…wanusuruni watu wetu….wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Mnusuru Afrika…yetu nzuri.”

Pia hakumficha mchumba wake Salim, bali alimwambia ukweli. Uk. 29 Furaha anasema: “Nina Ukimwi Salim”

Suala la upendo

Upendo wa kweli ni ule unaojali kitu au mtu katika shida na raha. Ni kujitolea kwa moyo wote bila kujali lolote. Ni kujitoa kwelikweli.

Mwandishi analizungumzia jambo hili kama suala muhimu sana katika jamii.

Tunapaswa kuonesha upendo kwa wagonjwa wa Ukimwi kwa kuwafariji na kuwapa matumaini.

Wahanga wa ugonjwa huu pia wanapaswa kusaidiwa, kama vile watoto yatima wanaoachwa na wazazi wao wakiwa wadogo. Wanapaswa kupewa msaada na matunzo mazuri. Hawapaswi kunyanyapaliwa, bali kupendwa.

Katika kitabu, mhusika Mama Furaha ameonesha upendo wa kipekee kwa mwanawe, pamoja na hali aliyokuwa nayo Furaha. Hili si jambo rahisi kwa watu wengi.

Mfano uk. 30-31, Mama Furaha anaongea na mwanawe akiwa hoi kitandani, kwa upendo na kujali. Anasema: “hakuna mtu aliye kamili. Lakini uliwaangalia wadogo zako. Na kila mahali ulipokuwapo, kulikuwa na nuru ya jua! Ulikuwa binti mzuri…binti yangu mzuri…. Inaelekea kama umezaliwa jana tu. Na hata wakati huo ulizidi kunifanya nisubiri, wakati nikiwa na mimba yako. Nakumbuka jinsi ulivyokua. Ukikimbia shambani mwetu, ukijaribu sana kumfurahisha baba yako…unajua anakujali kwa namna yake…..amelala sasa lala mwanangu”.

Imani potofu juu ya Ukimwi

Wanakijiji wengi katika kijiji cha Furaha hawakuwa na elimu juu ya ugonjwa huu hatari.

Furaha alipougua, kila mmoja alisema lake. Wengine walidai kuwa amerogwa. Pengine pia ujinga ulichangia wao kutoelewa kuhusu Ukimwi.

Mfano uk. 25-26 ni majibizano ya wanakijiji juu ya habari za kuumwa kwa Furaha

  • Mwanakijiji wa 1: Bi Furaha anaumwa sana…
  • Mwanakijiji wa 2: Tulijua anaumwa
  • Mwanakijiji wa 1: Ndiyo lakini katibu katika ofisi ya daktari kanambia ana huu ugonjwa wa AIDS
  • Mwanakijiji wa 4: Hicho si kitu kizuri
  • Mwanakijiji wa 1: Wanauita slim kwa sababu ugonjwa wenyewe hukufanya ukondeane
  • Mwanakijiji wa 3: Lakini amewezaje kuupata ugonjwa kama huo!
  • Mwanakijiji wa 1: Rahisi! kuna mtu kamroga…. Pengine rafiki msichana mwenye wivu.
  • Mwanakijiji wa 2: Nasikia unaupata kwa kugusana tu!
  • Mwanakijiji wa 4: Au hata kuwa nao katika chumba kimoja!

Mazungumzo hayo yanatuweka wazi kuhusu hali iliyoko kijijini juu ya elimu kuhusu Ukimwi. Wapo baadhi ya watu wanaoamini bado kuwa Ukimwi ni kurogwa tu.

Serikali na mamlaka husika zinapaswa kutoa elimu ya kutosha katika jamii ili kuwakomboa watu walioko vijijini.

Migogoro

Mgogoro kati ya Furaha na wazazi wake

Sababu ya mgogoro huu ilitokana na Furaha kuanza kupotoka kimaadili. Alitoroka nyumbani usiku na kwenda kwa wanaume baa kunywa pombe.

Baba yake na mama yake walimuadhibu ili kukemea suala hili.

Mgogoro kati ya Padre James na Mama Furaha

Sababu ya mgogoro huu ni orodha. Padre James alimzuia Mama Furaha asisome barua yenye orodha. Alihofia kwamba pengine jina lake lingetajwa miongoni mwa watu waliokuwa na mahusiano ya mapenzi na Furaha.

Suluhisho la mgogoro huu: Mama Furaha alimweka wazi Padre juu ya umuhimu wa kuisoma barua hiyo. Alimwambia kuwa hana la kuficha, bali aliisoma kwa lazima. (Uk. 3 na 43)

Mgogoro kati ya Salim na Mama Furaha

Salim hakutaka orodha isomwe. Hivyo alichana barua yenye orodha mazishini.

Mama Furaha hakusita. Aliisoma barua hiyo kwa kukusanya vipande na kuviunga. (Uk. 43 na 44)

Mgogoro kati ya Furaha na dada mdogo

Mgogoro huu ulitokea pale Furaha alipotaka kutoroka usiku, na mdogo wake akabaini. Mdogo wake alitishia kusema kwa wazazi.

Suluhisho: Furaha alimkemea na hata kutishia kumchinja. (Uk. 6) Mdogo wake aliogopa na hakusema lolote tena.

Mgogoro kati ya Salim na Furaha

Mgogoro huu ulitokana na Salim kumlazimisha Furaha amsomee orodha yeye kwanza. Furaha aligoma na kumsihi asubiri.

Ndipo Salim alipokasirika, nao wakaanza kutupiana maneno.

Mama Furaha alisuluhisha mgogoro huu kwa kumuamuru Salim atoke nje. (Uk. 30)

Mgogoro wa nafsi

Mgogoro huu uliwakuta Padre James, Salim, Kitunda na Bw Ecko. Walihofia orodha ambayo Furaha aliiandika ili isomwe katika mazishi yake.

Walihofia kutajwa katika orodha hiyo. Wangeaibika mbele ya kijiji, kwa sababu walijua fika kuwa mambo waliyoyafanya yalikuwa kinyume na maadili.

Walijitahidi kuzuia orodha hiyo isisomwe kwa hali na mali, lakini hawakufanikiwa.

Mama Furaha alifanikiwa kusoma orodha hiyo na kutoa ujumbe kwa jamii nzima.

Wale watu wanne walipata amani baada ya kujua kuwa orodha iliyosomwa haikuwa na majina yao.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa jamii ikielimishwa juu ya ugonjwa wa Ukimwi, ni rahisi kuepuka na kujikinga na maambukizi mapya.

Hii ni kupitia mambo anayoyapendekeza mwandishi, kama vile

  • uwazi
  • uadilifu
  • ukweli
  • upendo
  • matumizi ya kondomu
  • elimu
  • welewa
  • msamaha
  • uaminifu

Mtazamo

Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu. Anayaona mambo kwa udhati na uhalisia wake.

Anapinga mtazamo wa kidhanifu juu ya ugonjwa wa Ukimwi, kama vile kuamini kuwa ugonjwa huu unapatikana kwa kurogwa.

Anaweka wazi sababu za upatikanaji wa ugonjwa huu.

Msimamo

Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi. Analenga kuikomboa jamii kutoka katika hatari ya ugonjwa wa Ukimwi.

Anapendekeza mambo ya kufanya ili kuepuka ugonjwa huu, kama vile uaminifu, uadilifu, upendo, ukweli, uwazi n.k.

Fani

Mtindo

Mtindo wa dayalojia au majibizano

Mtindo aliotumia mwandishi ni wa dayalojia au majibizano. Ameunda visa na masimulizi yake kupitia majibizano ya wahusika.

Mtindo wa monolojia

Kwa kiasi kidogo, mwandishi ametumia pia mtindo wa monolojia. Mfano, uk. 27 Padre James anasema:

"Bwana natazamiwa kuiendesha sala hiyo! Ni kitu ambacho hakikubaliki! Shetani yu kazini kijijini hapa! Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyoipanda! Oh! Njia ya mtumishi wa bwana ni ngumu. Imejaa majaribu! Mtu lazima awe na nguvu na kuileta kazi ya bwana kwa watu hawa wa kawaida. Nimepewa kazi iliyo rahisi lakini ni ngumu sana! Ni kazi ya upweke!!! Mwili ni mdhoofu! Oh Bwana utulinde."

Hapa Padre James alijiongelea mwenyewe, akifikiri, akiwaza na kujutia kazi anayofanya.

Katika ukurasa huohuo, tunaona pia maneno ambayo Salim anajiongelea mwenyewe. Mifano mingine ni uk. 10, 23, 37 na 40.

Mtindo wa barua

Mwandishi ametumia pia mtindo wa barua katika kazi yake. Lengo ni kuweka mkazo katika mambo muhimu ya kuzingatia ili kuepuka UKIMWI.

Barua yenyewe ilisema hivi (uk. 44)

"Kwa Kijiji changu kipendwa,

Nawashukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika, kukua kama mtu; hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna orodha ya vitu ambavyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama, tafadhali wasomee watu wote orodha hii.

  • Uepukaji
  • Kondomu
  • Uaminifu
  • Elimu
  • Welewa
  • Uwazi
  • Uadilifu
  • Uwajibikaji
  • Ukweli
  • Upendo
  • Msamaha

Ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote. Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na majiji mengine katika nchi yetu hii nzuri. Wanusuruni watu wetu ili waweze kuyafaidia maisha kikamilifu. Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Mwinusuru Afrika... Afrika yetu nzuri.

Kwa kijiji changu kiishi maisha marefu na kiwe na furaha! Msihukumu mapema mno. Kwa mama, baba, dada zangu, nawapenda. Jaribuni kuwa wenye furaha wakati mnaweza kufanya hivyo.

Wenu awapendaye,

Furaha."

Matumizi Ya Nafsi

Mwandishi ametumia nafsi mbalimbali. Hii ni mifano

Nafsi ya kwanza umoja na wingi

  • Uk. 28 Salim: "nilidhani sitakuona tena, sijakuona muda mrefu"
  • Uk. 42: "oh huwezi kuamini jinsi tulivyojaribu"

Nafsi ya pili

  • Salim: "usifurahi kupita kiasi"
  • Salim: "hufai kuhukumu unalala kama....."
  • Mama Furaha: "usiwe hivyo wewe u mtoto mzuri."

Nafsi ya tatu

  • Mama Furaha: "kabla Furaha hajafa alitaka niahidi kumfanyia kitu fulani hapa kwenye mazishi. Ingawaje alikuwa na maumivu na mateso, aliandika barua hii hapa na kunipa."

Matumizi Ya Lugha

Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na inayoleweka kwa wasomaji wake.

Matumizi Ya Tamathali Za Semi

Sitiari

  • Uk.2 "Waridi changa" na "Ua kavu". Mama anamfananisha Furaha na waridi au ua.
  • Uk.4 "Nyie Mbu mlolaaniwa". Baba Furaha anawaita wadogo zake Furaha hivyo.
  • Uk.6 "Ua". Neno hili linamaanisha Furaha.
  • Uk.25 "Slim". Neno hili linamaanisha UKIMWI. Wanakijiji wanaufananisha ugonjwa huu na jina hili kutokana na sifa yake ya kukondesha mwili.

Tashibiha

  • Uk.18 "yeye ni kama Punda wa kijiji". Mwanakijiji wa 1 anamfananisha Furaha na Punda kutokana na tabia yake ya kuwa na wanaume wengi. Ni malaya.
  • Uk.13 "kisura ni kama jiji la New York…"
  • Uk.43 "…vipande vinaanguka kama theluji".

Mubaalagha

  • Uk.13 "kisura ni kama Jiji la New York ya Afrika Mashariki. Kule kuna majengo makubwa kiasi kwamba unaweza kuona mlima Kilimanjaro kwa juu".
  • Pia anasema: "Ndiyo mpenzi na Maduka… wana moja linaloitwa Shoppers Plaza…! Pengine ndilo eneo kubwa lenye maduka makubwa kuliko yote katika Afrika".
  • Uk.20:

Furaha: nani aliyesema mambo hayo?

Mama Furaha: Nusu ya kijiji kizima badala ya watu wengi.

Mama Furaha anazidisha chumvi kuonesha ukubwa wa hilo jambo.

Tafsida

  • Uk.7 ni maongezi kati ya wahusika:

Mary: hiyo ni bia yake ya mwanzo.

Furaha: ni chungu.

Mary: ladha yake utaizoea tu.

Bw. Juma: kama ulivyoizoea wewe mayai yangu madogo!

Bw. Ecko: Unaona! Inashangaza jinsi ambavyo mtu unaizoea haraka ladha hiyo!

Bw. Juma (kwa Mary): kama ulivyofanya wewe, mishikaki yangu midogo….

Mazungumzo haya yamepunguza ukali wa maneno. Maneno kama "mishikaki" na "mayai" ni sehemu za siri.

Mbinu Nyingine Za Kisanaa

Mdokezo

  • Uk.8 "ndiyo padre….. ni …..".
  • Uk.9 "Furaha…..fur….tuta…..".
  • Uk.20 "ame…..tuseme…..".
  • Uk.36 "misamaha padre mi…".
  • Uk.44 "uepukaji….".

Nidaa

  • Uk.15 "Ooo!"
  • Uk.34 "Oh!"
  • Uk.41 "Eee"

Takriri

  • Uk.28 "Hapana hapana hapana nitauona!" na "mpumbavu mpumbavu mimi".
  • Uk.9 "hili ni jambo zito sana… sanasana…..sana hasa…".
  • Uk.44 na 45 maneno haya yamerudiwa kuonesha msisitizo:

Mwanakijiji wa 2: kondom

Mwanakijiji wa 3: elimu

Mwanakijiji wa 4: elimu

Mwanakijiji wa 1: uwazi

Kitunda: uadilifu

Padre James: ukweli

Mary: upendo

Salim: msamaha.

Tashtiti

  • Uk.20:

Mama Furaha: wewe na marafiki zako wa kiume.

Furaha: marafiki gani wa kiume?

Furaha anauliza swali ambalo majibu yake anayo. Anataka tu kuupindisha ukweli.

  • Uk.38:

Baba: msalaba wako, padri. Uko shingoni mwako!

Padre James: kweli?

Baba: padre!

Padre James: hakika?

Padre James alijua wazi kuwa msalaba ulikuwa shingoni. Alikutwa katika pilika za kutafuta barua, akasingizia amedondosha msalaba kwa kutaka kuficha ukweli. Alijifanya kuuliza kama vile hajui.

Onomatopea au tanakali sauti

  • Uk.33-34 "Myaau!"
  • Uk.35 "Oooowww!"

Matumizi Ya Semi

Misemo

  • Uk.27 "Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyopanda".

Wahusika

Furaha

  • Ni binti mdogo wa miaka kati ya 13-19.
  • Ni malaya.
  • Anaathirika kwa ugonjwa wa UKIMWI.
  • Alikuwa na bidii na mwenye kujituma.
  • Ana tama.
  • Ni mlevi.
  • Ni mkweli na muwazi.
  • Ni jasiri.

Baba

  • Ni baba yake Furaha.
  • Ni mkali.
  • Ana upendo.

Mama Furaha

  • Ni mama yake Furaha.
  • Ni mkweli na muwazi.
  • Ana upendo.
  • Ni jasiri.
  • Ni mchapakazi.
  • Ni mpole.
  • Ana msimamo.
  • Anafaa kuigwa na jamii.

Mary

  • Ni binti mdogo.
  • Ni malaya.
  • Si rafiki mwema.
  • Anachangia kuharibu maisha ya Furaha.
  • Ni mlevi.
  • Anapenda anasa.
  • Ana tama.
  • Hafai kuigwa na jamii.

Bw. Ecko

  • Ni mwanaume mtu mzima.
  • Ni malaya.
  • Si muaminifu katika ndoa yake.
  • Ni mrubuni kwa mabinti wadogo.
  • Ni mlevi.
  • Ni mfanyabiashara.
  • Ni muathirika wa UKIMWI.

Juma

  • Ni mwanaume mtu mzima.
  • Ni malaya.
  • Ni laghai kwa mabinti wadogo.
  • Ni mlevi.
  • Anapenda anasa.
  • Ana tama.
  • Ni rafiki wa Bw. Ecko.

Padri James

  • Ni mtumishi wa Mungu katika kanisa katoliki.
  • Si muadilifu.
  • Anaogopa ukweli na uwazi.
  • Ni dhaifu kwa wanawake.
  • Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI.

Kitunda

  • Ni kijana wa mtaani.
  • Anapenda anasa.
  • Ana tama.
  • Ni mlaghai kwa wasichana.
  • Ni muhuni.
  • Ni mlevi na mvuta bangi.
  • Ana lugha ya kihuni.

Salim

  • Ni kijana wa kiume.
  • Ni msomi.
  • Ni mchumba wa Furaha.
  • Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI.
  • Si mkweli na muwazi.
  • Si muadilifu.

Wanakijiji 1, 2 Na 3

  • Ni wanakijiji katika kijiji cha Furaha.
  • Hawana elimu juu ya UKIMWI.
  • Ni wambea.
  • Wana imani potofu.

Dada Mdogo

  • Ni mdogo wake Furaha.
  • Ana tabia njema.
  • Ni mkweli lakini muoga.
  • Hapendezwi na tabia ya dada yake.

Mandhari

Mandhari aliyotumia mwandishi ni ya vijiji vya Afrika Mashariki kwa ujumla wake.

Mwandishi ametumia mandhari hii makusudi. Imeendana na yale anayoyazungumza katika kitabu.

Suala la ujinga na upotofu wa dhana kuhusu UKIMWI lipo zaidi vijijini. Wanakijiji hawaelewi juu ya UKIMWI.

Mambo anayoyaibua mwandishi yanaendana na jamii ya watu wa vijiji. Kwa hiyo mandhari ni sadifu.

Ujumbe

  • Elimu ya UKIMWI ni muhimu kutolewa katika jamii ya leo.
  • Wagonjwa na wahanga wa UKIMWI wanapaswa kupendwa na kujaliwa.
  • Ukweli na uwazi ni suluhu mojawapo ya kuepusha maambukizi mapya.
  • Watu wazima wanaoharibu maisha ya watoto wadogo wanapaswa kupigwa vita.
  • Upendo ni jambo la msingi kwa wahanga wa UKIMWI.
  • Wazazi wanapaswa kuwa makini katika malezi bora kwa vijana.
  • Watu wanapaswa pia kukombolewa kiuchumi kama njia dhidi ya kupinga UKIMWI.
  • Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.
  • Ulevi ni kichocheo cha maovu.

Maswali

  1. Nini tofauti kati ya maneno yafuatayo?
  1. Kuhakiki na uhakiki.
  1. Mhakiki na tahakiki.
  1. Eleza dhima za mhakiki katika uhakiki wa kazi za fasihi.
  1. Hadhira ina uhusiano gani na mhakiki?
  1. Ubora wa wahusika wa tamthiliya hutazamwa katika mambo yapi?
  1. Eleza hatua za uhakiki wa riwaya.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 8