Kuongeza msamiati wa kiswahili
Dakika 4 za kusoma ·
Yaliyomo
Dhana Ya Uundaji Wa Maneno
Maendeleo ya jamii hukua na kuongezeka kila mara.
Lugha nayo hukua na kuongezeka kila wakati kulingana na maendeleo hayo, ili kukidhi haja ya mawasiliano.
Kigezo kimojawapo cha kukua na kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa msamiati wake.
Ili msamiati uongezeke katika lugha, sharti maneno mapya yaundwe.
Njia Za Uundaji Wa Maneno
- Kutohoa maneno:
Kutohoa ni njia ya uundaji wa maneno ambapo lugha ya Kiswahili hukopa maneno ya lugha nyingine za kigeni kama yalivyo.
Mifano
Kiingereza kwenda Kiswahili
- Tractor – Trekta
- Number – Namba
- Picture – Picha
Kiarabu kwenda Kiswahili
- Wakil – Wakili
- Rijali – Rijali
- Shukran – Shukurani
Kireno kwenda Kiswahili
- Bibo – Bibo
- Mesa – Meza
- Lenco – Leso
Kiajemi kwenda Kiswahili
- Pilao – Pilau
- Jamadaar – Jamadari
- Darbyn – Darubini
Kihindi kwenda Kiswahili
- Achari – Achari
- Bhajiya – Bajia
Kituruki kwenda Kiswahili
- Sol – Soli
- Kohkoni – Korokoroni
Kifaransa kwenda Kiswahili
- Champ – Shamba
- Duvin – Divai
Kijerumani kwenda Kiswahili
- Schule – Shule
- Heller – Hela
Lugha za makabila ya Kitanzania
- Kabila – Kiswahili
- Ikulu – Kigogo, Kisukuma, Kinyamwezi
- Bunge – Kigogo, Kisambaa, Kiha, Kiganda
- Kitivo – Kipare, Kisambaa
- Unga – Kizigua
- Ndafu – Kichaga
- Kigoda – Kizaramo
- Njia ya miambatano (kuunganisha maneno):
Ni uundaji wa maneno kwa kuunga maneno mawili au zaidi na kuunda neno moja.
Mifano
Nomino + Nomino
- Mwana + Nchi = Mwananchi
- Askari + Kanzu = Askari kanzu
- Njugu + Mawe = Njugu mawe
Kitenzi + Nomino
- Zima + Moto = Zimamoto
- Changa + Moto = Changamoto
- Kata + Mbuga = Katambuga
Nomino + Kivumishi
- Mtu + Mwema = Mtumwema
- Mcheza + kwao = Mcheza kwao
- Mwana + Kwetu = Mwanakwetu
- Njia ya kutumia mpangilio tofauti wa fonimu au vitamkwa:
Kila lugha ina mpangilio maalumu wa vitamkwa.
Mfano, neno lima linaweza kubadilishwa na kuunda maneno yafuatayo
- Mali
- Mila
- Imla
- Lami, na kadhalika
- Njia ya kuambisha maneno:
Uambishaji wa maneno ni kuunda maneno kwa njia ya ubandikaji wa viambishi kabla na baada ya mzizi.
Mfano: mzizi -lim- unaweza kubandikwa viambishi, tukapata maneno kama vile walilima, mkulima, kilimo, ukulima, na kadhalika.
- Njia ya kufananisha sauti, sura au tabia:
Kufananisha sauti au mlio wa vitu. Mifano
- Pikipiki – Limeundwa kutokana na mwigo wa sauti ya chombo hicho.
- Mtutu – Limeundwa kutokana na mlio wa bunduki.
- Kengele – Limeundwa kutokana na mlio wa chombo hicho.
- Nyau – Limetokana na mlio wa sauti ya paka.
Kufananisha sura. Mfano
- Kifaru (silaha ya kivita) – Limetokana na kufanana sura na kifaru, mnyama wa porini.
Kufananisha tabia. Mfano
- Beberu – Limetokana na mnyama (mbuzi) kuwa na tabia ya uonevu.
Kufananisha umbile. Mfano
- Mkono wa tembo (aina ya ndizi) – Limeundwa kutokana na kufananishwa kwa umbo la aina hiyo ya ndizi na mkonga wa tembo.
- Kuangalia athari za kitu:
Hii ni njia ya kuunda maneno kwa kutumia mbinu ya kuangalia athari za kitu kinachohitaji kuundiwa neno au jina.
Mfano
- Vichachu – Vitu vyenye uchachu.
- Njia ya kufupisha maneno:
Hii ni njia ya kuunda maneno kwa kufupisha maneno marefu.
- Ufupisho wa kuchukua herufi za mwanzo tu za maneno (akronimu). Mifano:
- Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)
- Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
- Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA)
- Ufupisho wa uhulutishaji (blending). Mifano:
- Mtu asiye na kwao (Msikwao)
- Mnyama mfu (Nyamafu)
- Joto baridi (Jotoridi)
- Njia ya urudufishaji:
Hii ni njia ya kuunda maneno kwa kurudiarudia neno lilelile.
Mifano
- Taka – Takataka
- Mbali – Mbalimbali
- Kizungu – Kizunguzungu
- Kati – Katikati
- Njia ya kutumia tafsiri sisisi:
Njia hii hutafsiri neno kwa neno kutoka katika lugha nyingine.
Mifano
- Watermelon – Tikiti maji
- Head of state – Mkuu wa nchi
- Tree – Mti
Uundaji Wa Maneno Katika Miktadha Mbalimbali
Ili kukidhi haja ya mawasiliano, hakuna budi kuunda maneno mapya. Maneno hayo huundwa ili yaendane na haja ya matumizi ya lugha.
Tuangalie mifano ifuatayo
- Maneno kama fedha, pesa, shilingi, senti, benki na ushuru yameingia kwenye Kiswahili baada ya kutokea kwa maendeleo ya kiuchumi. Maendeleo hayo ni ya kutumia fedha badala ya kubadilishana bidhaa.
- Maneno kama gari, kompyuta, gesi, petrol, bomu, bunduki, nyuklia, sinema, redio na umeme yametokana na maendeleo katika sayansi na teknolojia.
- Maneno kama raisi, mtemi, mfalme, ukoloni, jamhuri, demokrasia na walala hoi yametokana na mabadiliko ya mfumo wa siasa na utawala katika nyakati tofauti.
- Maneno kama zahanati, hospitali, aspirini, bendeji, plasta na vidonge yametokana na maendeleo katika mfumo wa tiba.
- Maneno kama gauni, suruali, shati, viatu, uma, vitunguu, dansi na bendi yametokana na maendeleo ya kiutamaduni.
Umuhimu Wa Kuongeza Msamiati
- Hufanya lugha ijitosheleze kimsamiati.
- Hurahisisha mawasiliano katika nyanja mbalimbali.
- Hutia mvuto katika lugha.
Maswali
- Uambishaji ni nini?
- Andika maneno matatu yaliyotokana na njia ya urudufishaji.
- Buni virefu vya maneno haya:
- BASATA
- UKIMWI
- TUKI
- Jamii inapata faida gani pindi maneno mapya yanapoundwa?
- Orodhesha maneno yasiyopungua matano ya Kiswahili yaliyotokana na lugha nyingine za kigeni.
- Andika njia zilizotumika kuunda maneno yafuatayo:
- Barabara
- BAKITA
- Kifaru
- Mashine
