Ukuaji na ueneaji wa kiswahili enzi ya…
Dakika 10 za kusoma ·
Yaliyomo
Ukuaji Na Ueneaji Wa Kiswahili Enzi Ya Waingereza Na Baada Ya Uhuru
A: Ukuaji Wa Kiswahili Enzi Za Waingereza
Kukua kwa lugha ni hali ya kuongezeka kwa msamiati katika lugha.
Msamiati huo hutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni yanayoikumba jamii.
Waingereza walianza kuitawala Tanzania (wakati huo Tanganyika) baada ya vita ya kwanza ya dunia (1914 – 1918). Walianza kutawala baada ya Wajerumani kung'olewa.
Wakati wa utawala wa Waingereza, lugha ya Kiswahili ilipokea maneno mengi mapya. Maneno hayo hayakuwa yakitumika hapo awali. Pengine yalikuwa hayafahamiki kabisa.
Mambo Yaliyosaidia Ukuaji Wa Msamiati Wa Kiswahili Enzi Ya Utawala Wa Waingereza
Shughuli za kiuchumi
Mfano ni kilimo cha mazao ya biashara na biashara kwa ujumla. Waingereza waliendesha kilimo cha karanga, tumbaku na pamba.
Maneno mapya yaliyozalishwa ni kama vile
- Yadi – kipimo kilichokuwa kikitumika kupima eneo la kulima kibarua.
- Bani – jengo maalumu la kukaushia zao la tumbaku.
- Belo – mitumba ya tumbaku.
- Manamba – vibarua.
- Mtama – zao lililokuwa linalimwa.
Shughuli za kiutamaduni
Mfano ni uenezaji wa muziki wa kigeni. Baadhi ya maneno yaliyoongezeka katika Kiswahili ni dansi na twisti.
Shughuli za kidini
Waingereza walieneza dini ya Ukristo. Baadhi ya maneno ya Kiswahili yaliyotokana na shughuli za kidini ni roho mtakatifu, ubatizo, kipaimara, sala na mengineyo.
Waingereza walipoitawala Tanganyika, walikuta Uislamu umekwishaingia. Uislamu pia ulichangia maneno mbalimbali kama vile msikiti, shekhe, kibla, imamu, rakaa, msahafu, alhaji na mengineyo.
Shughuli za kisiasa
Waingereza waliunda vyombo vya dola. Jukumu la vyombo hivyo lilikuwa kusimamia utekelezwaji wa sheria na sera za watawala wao.
Maneno yaliyozalishwa kutokana na shughuli za kisiasa ni mahakama, ofisa, jimbo, boma, baraza na chifu.
Utaalamu
Sayansi na teknolojia ziliendelea. Kwa sababu hiyo, maneno mengine yalichukuliwa kutoka lugha ya Kiingereza na kuingizwa katika Kiswahili.
Mfano ni mofimu, stigma, alofoni, fonimu, mashine, televisheni, chaki, rula na mengineyo.
Shughuli za ujenzi wa nchi
Waingereza waliendeleza ujenzi wa reli ulioachwa na Wajerumani kabla ya vita ya kwanza ya dunia.
Maneno yaliyotoholewa ni kama vile reli, stesheni, tiketi, tiitii, treni na mengineyo.
Usanifishaji wa Kiswahili
Usanifishaji wa Kiswahili ulisaidia ukuaji wa lugha ya Kiswahili. Ulileta ulinganifu wa lugha katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Hivyo Kiswahili kiliweza kutumika bila kuleta tofauti za msamiati.
Kuundwa kwa kamati ya kusanifisha lugha
Chama cha kusanifisha lugha (The International Language Swahili Committee) kiliundwa tarehe 1-1-1930.
Madhumuni yake makuu yalikuwa
- Kusimamia shughuli zote za usanifishaji.
- Kupendekeza utaratibu wa matamshi, msamiati, muundo na maumbo ya Kiswahili, na kuyapa kibali rasmi.
Vitabu vilivyochapishwa ni "The Standard Swahili" na English – Swahili Dictionary.
Kuchapishwa kwa vitabu vya Kiswahili
Shirika la kushughulikia upitiaji na uchapaji miswada, "The East African Literature Bureau", lilianzishwa mwaka 1948. Kisha uchapaji wa vitabu ulianza.
Baadhi ya vitabu vilivyochapishwa ni
- B.W. Swahili Grammar (including intonation) [1940] na Ashton E.O.
- Sarufi ya Ufasaha I, Vihusishi II, Miao (1959) na Kapoka E.B.
Vitabu hivi vimechangia sana katika ukuaji wa msamiati wa Kiswahili wakati wa utawala wa Waingereza. Vitabu vingine ambavyo havijatajwa pia vimechangia.
Ueneaji Wa Kiswahili
Ueneaji wa lugha ni namna lugha inavyotumika katika sehemu nyingine zaidi, mbali na pale ilipoanzia.
Kihistoria, lugha ya Kiswahili ilianzia katika upwa wa Afrika Mashariki. Kisha kilienea taratibu hadi sehemu za bara.
Mambo yafuatayo yalisaidia kuenea kwa Kiswahili nchini wakati wa enzi ya utawala wa Waingereza:
- Suala la elimu: Wakati wa Mwingereza, Kiswahili kilitumika kufundishia shule za msingi, darasa la 1-4. Pia kilikuwa somo mojawapo hadi darasa la 12 katika shule za Waafrika.
- Suala la kilimo na manamba: Kilimo cha Waingereza kilitegemea sana manamba (vibarua) waliotoka katika makabila tofauti. Lugha ya mawasiliano iliyotumika na vibarua hao ilikuwa Kiswahili. Hivyo basi, hata waliporudi nyumbani kwao, walieneza Kiswahili sehemu mbalimbali za nchi.
- Mchango wa vyombo vya habari: Mfano ni magazeti, redio na majarida mbalimbali. Kwa upande wa redio, mwaka 1950 Redio Tanganyika ilianza kurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Magazeti yaliyosaidia ueneaji wa Kiswahili ni Mambo Leo (1923), Mwangaza (1923), Sauti ya Pwani (1940), Habari za Leo (1954) na Kiongozi (1950).
- Suala la jeshi (KAR): KAR lilikuwa jeshi la mkoloni lililoundwa na watu kutoka makabila tofauti. Hivyo basi, Kiswahili kiliteuliwa kitumike kama lugha ya mawasiliano katika jeshi hilo.
- Harakati za kudai uhuru: Harakati za kudai uhuru zilianza mwaka 1954, baada ya kuzaliwa kwa TANU. Wanaharakati walitumia Kiswahili kuhamasisha watu katika harakati hizo.
- Suala la utawala: Waingereza walisisitiza kwamba kila chifu afahamu Kiswahili ili atumike katika shughuli za utawala. Vilevile, ili mtu apate ajira katika ngazi za utawala, ilikuwa lazima afahamu Kiswahili.
Tathmini Ya Maendeleo Ya Kiswahili Wakati Wa Waingereza
Kiswahili kilipata maendeleo ya kuridhisha katika muhula wa Waingereza. Hata hivyo, kilikabiliwa na changamoto mbalimbali, ambazo ni:
- Kutofundishwa Kiswahili katika shule zote. Kiswahili kilifundishwa kwenye shule za watoto wa Kiafrika pekee.
- Kiswahili hakikutumika kama lugha ya kufundishia.
- Kukosekana kwa vyombo vya kizalendo vya kuendeleza lugha ya Kiswahili.
- Kushamiri kwa kasumba ya kuthamini Kiingereza.
Ukuaji Na Ueneaji Wa Kiswahili Baada Ya Uhuru
Maendeleo ya Kiswahili yalipata msukumo zaidi baada ya uhuru. Hii ilitokana hasa na hatua ya serikali kukipitisha Kiswahili kuwa lugha ya taifa.
Kimsingi, zipo sababu nyingi zilizosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili baada ya uhuru. Sababu hizo ni hizi zifuatazo:
- Sababu za kisiasa:
Miongoni mwa mambo ya kisiasa yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili baada ya uhuru ni kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa na kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Maneno kama kupe, unyonyaji, kujitegemea, ujamaa, azimio, bwanyenye, kabaila, bepari na mengineyo yaliibuka katika kipindi hiki.
Vilevile, vita ya Tanzania na Uganda mwaka 1978-1979 vilichangia ukuaji wa lugha ya Kiswahili. Maneno kama nduli, fashisti, kujaa, diktekta, walokole na mengineyo yaliibuka.
Pia, kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977 kulizalisha misemo kama "chama kushika hatamu".
Mwaka 1992, katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi, maneno kama walalahoi, wakereketwa, ngangari na mengineyo yaliibuka.
- Sababu za kielimu: Baada ya uhuru, Kiswahili kiliteuliwa kutumika kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi. Pia kilifundishwa kama somo katika shule za sekondari na vyuo.
- Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA): Baraza hili liliundwa mwaka 1967. Kazi yake kuu ilikuwa kuratibu shughuli zote za ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kote nchini.
- Vyombo vya habari, hasa magazeti, redio na televisheni.
Asasi Na Vyombo Mbalimbali Vya Kukuza Na Kueneza Kiswahili Nchini
Taasisi Ya Uchunguzi Wa Kiswahili (Tuki)
Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ilihamishiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1964. Ilipandishwa hadhi na kuitwa TUKI. Sasa hivi inaitwa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI).
Kazi za TUKI (TATAKI)
- Kuendesha uchunguzi wa lugha kwa madhumuni ya kukuza na kustawisha Kiswahili.
- Kuwatia moyo watu wanaojishughulisha na uandishi wa vitabu katika lugha ya Kiswahili.
- Kushughulika na ukuzaji wa maneno ya Kiswahili na utengenezaji wa kamusi za Kiswahili.
- Kuhifadhi ufasaha wa lugha ya Kiswahili.
- Kuitisha semina fupifupi kwa ajili ya kutayarisha vitabu vya kutumiwa katika shule za msingi.
TUKI (TATAKI) imegawanyika katika sehemu zifuatazo
- Sehemu ya fasihi: Inajishughulisha na utafiti wa fasihi andishi na fasihi simulizi.
- Sehemu ya uchapaji: Hujihusisha na utoaji wa vitabu na majarida ya Kiswahili na Mulika.
- Sehemu ya isimu: Hushughulikia utafiti katika sarufi na matumizi ya Kiswahili, pamoja na lahaja za Kiswahili.
- Sehemu ya kamusi: Hujishughulisha na uundaji wa kamusi. Mfano ni Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
- Sehemu ya istilahi na tafsiri: Hujihusisha na uundaji wa istilahi na kutafsiri vitabu mbalimbali kutoka lugha za kigeni au za Kibantu.
Mafanikio ya TUKI
- Imefanikiwa kutoa majarida mbalimbali ya Mulika na jarida la Kiswahili.
- Imesaidia kutoa kamusi mbalimbali, kama vile Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981), Kamusi ya Isimu na Lugha (1996) na Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza (2001).
- Imechapisha vitabu mbalimbali vya fasihi na sarufi ya Kiswahili. Mfano ni Maisha ya Salum Abdullah (1975), Pete (1978), Samikisa (2001) na vinginevyo.
- Imefanikiwa kuendesha semina mbalimbali za kimataifa. Kutokana na semina hizo, wametoa vitabu mbalimbali. Mfano ni Lugha ya Kiswahili (1983) na Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili (1980) na vinginevyo.
- Imefanya uchunguzi wa tanzu mbalimbali za fasihi, yaani fasihi simulizi na andishi.
- Imetafsiri vitabu mbalimbali kwa Kiswahili kutoka lugha ya Kiingereza. Mfano ni Historia Kuu ya Afrika, juzuu 1-8.
Matatizo ya TUKI
- Uhaba wa fedha za kuendeshea shughuli zao za utafiti wa Kiswahili.
- Uhaba wa wataalamu. Wataalamu wengi hukimbilia nje ya nchi kwenye maslahi mazuri.
- Uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi.
Baraza La Kiswahili La Taifa (Bakita)
Baraza hili liliundwa kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1967. Ndilo lililoshika hatamu ya ukuzaji wa lugha ya Kiswahili hapa nchini.
Kazi za BAKITA
- Kukuza maendeleo na matumizi ya Kiswahili fasaha katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Kutafsiri na kufanya ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali, pamoja na asasi nyingine.
- Kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuthibitisha usahihi wa Kiswahili kwa vitabu vyote vya Kiswahili vinavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.
- Kuratibu kazi za ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa jinsi lugha ya Kiswahili ilivyo.
Bakita: Idara Zake, Mafanikio Na Matatizo
BAKITA imegawanyika katika idara zifuatazo
- Idara ya tafsiri: Inashughulikia tafsiri mbalimbali.
- Idara ya uchapishaji: Hujishughulisha na uchapishaji, uchapaji na uhariri.
- Idara ya lugha na fasihi: Hujishughulisha na ufasaha wa lugha na kuratibu maendeleo ya Kiswahili.
- Idara ya istilahi: Hujishughulisha na usanifishaji wa istilahi.
- Idara ya uhusiano: Hujishughulisha na uhamasishaji wa vipindi vya redio na televisheni.
Mafanikio Ya Bakita
- Imeandaa istilahi za taaluma mbalimbali kama vile fizikia, biashara, kemia, bailojia, uchumi, bunge, posta na kadhalika.
- Imetoa majarida mbalimbali kama vile Lugha Yetu, Lugha ya Kiswahili, Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine na mengineyo.
- Huendesha vipindi mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili katika Redio Tanzania Dar es Salaam. Mfano: "Lugha Yetu" na "Ulimwengu wa Kiswahili".
Matatizo Ya Bakita
- Uhaba wa fedha.
- Uhaba wa wataalamu.
Vyombo Vingine Vya Kukuza Kiswahili
Takiluki:
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar (TAKILUKI) ilianzishwa mwaka 1979. Chombo hiki kilitokana na ile Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ilipohamishiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1963.
Kazi za TAKILUKI
- Kuendesha semina na warsha za Kiswahili.
- Kufanya tafiti za Kiswahili katika nyanja zake zote, ambazo ni fasihi na sarufi.
- Kuendesha mafunzo ya masomo ya Kiswahili na lugha za kigeni kwa wanafunzi wenyeji na wanafunzi kutoka nje.
Chaka:
Chama cha Kiswahili cha Afrika (CHAKA) kiliundwa katika semina ya kimataifa ya usanifishaji wa istilahi za Kiswahili. Semina hiyo ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978.
Kazi za CHAKA
- Kukuza na kueneza Kiswahili kote Afrika.
- Kuleta umoja katika mataifa ya Afrika kwa kutumia lugha za asili.
- Kutengeneza vifaa vya kufundishia Kiswahili, kama vile kamusi, vitabu vingine vya kitaaluma, kanda za sauti, santuri na kadhalika.
- Kuanzisha vyama vya Kiswahili kwa kila nchi mwanachama na kukusanya data mbalimbali.
- Kutafuta misaada ya hiari inayoweza kusaidia shughuli za ukuaji wa Kiswahili.
- Kutafuta misaada ya mafunzo kwa walimu, wakalimani, wafasiri na watafiti, ili waweze kufikia malengo yao ya kukuza Kiswahili.
Bamita:
Baraza la Mitihani la Taifa (BAMITA) lina lengo kuu la kutahini katika viwango mbalimbali vya elimu nchini. Hutahini kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo.
Limefanikiwa kutahini hadi kiwango cha sita na stashahada.
Chama cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chama hiki kilianzishwa mwaka 1970 na wanafunzi waliokuwa wakisoma chuoni hapo.
Lengo kuu lilikuwa kukuza ari ya kupenda somo la Kiswahili na kuthamini Kiswahili kwa ujumla.
Taasisi ya Elimu Tanzania
Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1966.
Kazi yake ni kutayarisha mihtasari ya masomo ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya msingi.
Pia hutayarisha na kuongoza semina mbalimbali kwa ajili ya walimu, ili kuwawezesha kufundisha vyema lugha ya Kiswahili.
Taasisi hii imefanikiwa kuandaa vitabu vya Kiswahili vya kufundishia, kama vile Kiswahili Kidato cha 1-4.
Maswali
- Nini maana ya kukua kwa lugha?
- Taja mambo ambayo yalisaidia ukuaji wa msamiati wa Kiswahili enzi za Wajerumani.
- Maneno ya Kiswahili kama vile ghali, pesa na shilingi yametokana na muktadha gani?
- Eleza changamoto zilizoikumba lugha ya Kiswahili wakati wa Waingereza.
- Ni kwa namna gani siasa ilisaidia kukuza lugha ya Kiswahili enzi za Waingereza?
