Kiswahili · Kidato 4

Uandishi…

Dakika 7 za kusoma ·

Yaliyomo

Uandishi

Taratibu za uandishi ni mfumo wa alama na mpangilio wa maneno unaomuongoza mwandishi kuandika vizuri.

Alama Za Uandishi

  1. Nukta (kituo kikuu) (.)

Nukta ndiyo alama ya kituo iliyo kuu kuliko alama nyingine zote za vituo.

Alama hii hutumika katika uandishi kwa madhumuni yafuatayo

  • Kuonyesha mwisho wa sentensi. Mfano: Asanteni kwa kuja.
  • Kufupisha maneno. Mfano: S.L.P, n.k, s.m.z
  • Kuonyesha vipimo na sehemu zake. Mfano: Lita 60.5, Hekari 6.4, km 7.34
  • Kutenganisha siku, mwezi na mwaka katika uandishi wa tarehe. Mfano: tarehe 12.01.1992
  • Kuandika anwani za tovuti. Mfano: www.kitalulaabubakar.co.tz
  1. Nukta pacha (:)

Alama hii hutumika kwa madhumuni yafuatayo

  • Kuonyesha vitu vilivyo katika hali ya mfululizo wa orodha katika sentensi. Mfano: Aliagizwa vitu vifuatavyo: ndoo, sia, jembe, nk.
  • Kuandika anwani za tovuti. Mfano: tovuti: www.org.co.tz
  1. Nukta pacha na kistari (:-)

Alama hii hutumika kuashiria sentensi fupifupi zilizo katika hali ya mfululizo wa orodha.

Mfano: Madhumuni ya kuanzisha kikundi hiki ni haya:-

  • Kupiga vita Ukimwi
  • Kupambana na umasikini
  1. Nukta na mkato (;)
  • Hutumika kuunga tungo mbili zenye hadhi sawa lakini zisizo na kiunganishi. Mfano: Wengine wanakula; wengine wanalima.
  • Hutumika kuonyesha pumziko la muda mrefu zaidi katika kusoma kuliko unapotumia mkato. Mfano: Alikwenda mpaka nyumbani kwake; hakumkuta.
  1. Mkato (,) au koma

Alama hii hutumika kwa madhumuni tofauti

  • Kuandika anwani. Mfano: S.L.P. 9, Korogwe
  • Kutenganisha miezi na mwaka kwenye tarehe. Mfano: 7, 8, 2006.
  • Kutumika baada ya kiunganishi katika sentensi. Mfano: Tulifika kwake, hatukumkuta.
  1. Alama ya kuuliza (?)

Alama hii hutumika badala ya nukta au alama ya kushangaa ili kufunga sentensi za maswali.

Mfano: Wanafunzi wako wapi? Mbona siwaoni?

  1. Alama ya mshangao / kushangaa (!)

Alama hii pia hutumiwa badala ya nukta na alama ya kuuliza ili kufunga tungo ya mshangao.

Inapotumika, sentensi inayofuata huanza na herufi kubwa.

Mfano: He! Ni wewe!

  1. Alama za mtajo (" ") au (' ')
  • Hutumika kukariri maneno yaliyosemwa au kuandikwa na mtu mwingine. Mfano: Ali alisema "Sichezi tena mpira".
  • Hutumika kubainisha maneno yasiyokubalika katika mfumo wa lugha inayoandikwa. Mfano: Mara tu alipomuona 'dingi' akakitoa.
  1. Mstari mshazari ( / )
  • Hutumika kuandika namba za kumbukumbu katika barua.
  • Hutumika kutenganisha siku, mwezi na mwaka katika tarehe.
  • Hutumika kuandika anwani za tofauti.
  • Hutumika kutenganisha namba za simu.
  1. Mabano ( )
  • Hutumika kufunga maneno yanayotoa maelezo zaidi kuhusu maneno yaliyotangulia. Mfano: Wao (wanafunzi) hawatakuja.
  • Hutumika kuonyesha maana fupi ya maelezo fulani marefu. Mfano: Alikula maembe, ndizi, machungwa (matunda).
  • Hutumika kuonyesha namba au herufi. Mfano: (i) (ii) (iii), au (a) (b) (c)

B: Uandishi Wa Insha Za Kiada

Insha ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumziwa au kuandikwa.

Insha za kiada ni insha zisizo za kisanaa. Uandishi wa insha za kiada huzingatia taratibu zote za uandishi.

Muundo Wa Insha Za Kiada

Kichwa cha insha

  • Huandikwa kwa herufi kubwa, katikati juu ya insha.
  • Huandikwa kwa ufasaha na muhtasari, kisizidi maneno matano.
  • Huzingatia wazo kuu la insha.
  • Wakati mwingine hupigiwa mstari.

Utangulizi / mwanzo

  • Huzingatia fasili ya jambo linalozungumziwa, uhusiano wake na vitu vingine, na muhtasari wa insha inayotungwa.
  • Kwa kawaida utangulizi wa insha hauzidi aya moja.

Kiini cha insha

  • Hii ndiyo sehemu kuu ya insha.
  • Sehemu hii huzingatia mawazo makuu ambayo hupangwa katika aya zenye mtiririko mzuri wa mawazo.
  • Kiini huonyesha kwa undani jambo linalozungumziwa.

Mwisho wa insha

  • Huwa na msisitizo kwa yaliyojadiliwa.
  • Huwa na maoni na mapendekezo ya mwandishi kuhusu jambo lililotungiwa insha.
  • Mara nyingine huonyesha muhtasari wa yaliyojadiliwa au kuandikwa pamoja na hitimisho.

Mambo mengine ya kuzingatia katika insha

  • Kuzingatia kichwa cha habari na maelezo kama yapo.
  • Kuandika kwa kutumia taratibu za uandishi na lugha fasaha.
  • Kutotumia lugha ya mkato, kama vile kuandika sh. badala ya shilingi.
  • Kuandika utangulizi unaovuta makini ya wasomaji au wasikilizaji.
  • Kuandika kiini cha insha kwa mpangilio unaojitosheleza. Kila wazo kuu lipewe aya yake. Mawazo ya aya zote yahusiane.
  • Kuandika mwisho wa insha unaovutia ili wasomaji wapende kuendelea kusoma.

C: Uandishi Wa Hotuba

Hotuba ni maelezo yanayotolewa na mtu mbele ya watu.

Hotuba hutolewa kwa madhumuni maalum. Kwa mfano, inaweza kutolewa kwa madhumuni ya kuhimiza kazi au kutoa taarifa fulani kwa watu.

Muundo Wa Hotuba

Utangulizi

  • Sehemu hii ni maelezo ya kuwavuta wasikilizaji au wasomaji wa hotuba.
  • Maelezo hayo hutanguliwa na salamu. Mfano: Wananchi oyee!
  • Utangulizi pia huwa na utambulisho kulingana na vyeo. Mfano: Mheshimiwa mgeni rasmi, Ndugu wananchi.
  • Vilevile, utangulizi huwa na shukrani pamoja na muhtasari wa hotuba itakayotolewa.

Kiini cha hotuba

  • Hii ndiyo sehemu inayoonyesha jambo linalowasilishwa kwa wasikilizaji.

Hitimisho

  • Ni sehemu ya mwisho ya hotuba.
  • Mwisho wa hotuba huwa ni muhtasari wa yale yaliyoelezwa, kwa ajili ya kusisitiza, kutoa shukrani au kuagana.
  • Aghalabu hotuba huhitimishwa na maneno kama haya:
  • Natoa shukrani zangu kwa wote mlionisikiliza.
  • Baada ya kusema hayo machache…

D: Uandishi Wa Risala

Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya viongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu.

Muundo Wa Risala

Utangulizi

  • Katika sehemu hii hukaa maneno ya utangulizi.
  • Maneno hayo huwa ni ya salamu, kama vile "Wanakijiji oyee!"

Mwanzo

  • Katika sehemu hii hukaa maelezo yanayofafanua waandishi wa risala na lengo la risala.
  • Mfano: Risala ya wafugaji wa ng'ombe kwa wazazi wa mifugo.

Kiini

  • Hapa ndipo lengo la risala huwekwa bayana.

Hitimisho

  • Katika hitimisho huonyeshwa msisitizo, shukrani na jina la mtu aliyeandika risala, kwamba imeandikwa na fulani.

E: Uandishi Wa Kumbukumbu Za Mikutano

Muhtasari wa mambo muhimu yaliyojadiliwa na kukubaliwa katika mkutano huitwa kumbukumbu za mikutano.

Uandishi wa kumbukumbu za mikutano husaidia kurahisisha utekelezaji wa mambo yaliyoamuliwa.

Pia, kumbukumbu hizo hutumika kwa ajili ya marejeo kwa vizazi vya baadaye.

Namna Ya Kuandika Kumbukumbu Za Mikutano

Kichwa cha kumbukumbu

  • Kitaonyesha kuwa mkutano unahusu nini, mahali ulipofanyika na tarehe ilipofanyika.

Mahudhurio

  • Mwandishi anapaswa kuandika orodha ya majina ya watu waliohudhuria mkutano na wasiohudhuria.

Ajenda

  • Mwandishi anapaswa kuandika ajenda, yaani mambo yatakayozungumziwa katika mkutano.
  • Mambo yaliyojadiliwa katika kila ajenda yaandikwe kwa muhtasari.
  • Kwa kila ajenda, mwandishi anatakiwa kuonyesha kama ajenda hiyo imekubaliwa au imekataliwa.

Kufungua mkutano

  • Mwenyekiti akishafungua mkutano, mwandishi au katibu aandike saa ya kufungua kikao na muhtasari wa yale yaliyozungumzwa.

Kufunga mkutano

  • Baada ya majadiliano ya ajenda, mwenyekiti afunge mkutano.
  • Mwandishi wa kumbukumbu azingatie muda au wakati kikao kilipofungwa.

Kumbukumbu Za Mkutano

Kazi ya mwandishi baada ya mkutano

Baada ya mkutano, mwandishi apitie tena kumbukumbu hizo. Aziandike vizuri na azihifadhi kwa ajili ya marejeo ya mkutano ujao.

Kumbukumbu hizo zitiwe saini na mwenyekiti na mwandishi (katibu).

Wakati wa mkutano mwingine, kumbukumbu hizo zisambazwe na zisomwe na wajumbe wa mkutano.

Baadaye wajumbe na mwenyekiti wazithibitishe. Mwenyekiti atie saini ya kuonyesha kuthibitisha huko.

Mfano Wa Kumbukumbu Za Mkutano Unaofanywa Kwa Mara Ya Kwanza

Mahudhurio

  • Waliohudhuria ni wanafunzi 34 wa kidato cha 4A (orodhesha majina yao).
  • Wasiohudhuria ni wanafunzi 10 wa kidato cha 4A (orodhesha majina yao na sababu).

Ajenda

  • Kufungua mkutano
  • Uchaguzi wa kamati ya maadili ya mahafali
  • Mengineyo
  • Kufunga mkutano

Kufungua mkutano

Kiranja wa darasa alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo. Alifungua mkutano mnamo saa 4:00 asubuhi. Aliwaeleza wajumbe madhumuni ya mkutano huo.

Uchaguzi wa kamati

Wanafunzi wafuatao walichaguliwa ili wafanye mipango ya kuandaa na kusimamia sherehe ya mahafali yao:

  • S. Maganza
  • D. Makoba
  • F. Kipacha
  • B. Chimatu

Wajumbe hao walikubali uchaguzi huo. Waliahidi kupeana majukumu.

Mengineyo

Wajumbe walisisitiza kwamba kamati ifanye mipango kwa kuzingatia kwamba muda uliobaki ni mfupi.

Iliamuliwa kwamba kufanyike mkutano wa kuwapatia wajumbe taarifa kuhusu mgawanyo wa majukumu.

Kufunga mkutano

Mwenyekiti alifunga mkutano kwa kuwaomba wajumbe wengine wawe na ushirikiano na wenzao katika kufanikisha mahafali hayo.

Mkutano ulifungwa saa 6:00 mchana.

Sehemu ya saini

Mwenyekiti ……………………………………………

Tarehe ……………………………………………………

Katibu …………………………………………

Tarehe …………………………………………

Maswali

  1. Eleza matumizi ya alama hizi za uandishi:
  2. Mkato
  3. Alama ya kuuliza
  4. Mstari mshazari
  1. Insha za kiada ni zipi?
  1. Eleza tofauti iliyopo baina ya hotuba na risala.
  1. Taja mambo ya kuzingatia katika uandishi wa kumbukumbu za mikutano.
Jaribu quiz ya KiswahiliMaswali 8