Kiswahili · Kidato 6

Maana ya tafsiri

Dakika 14 za kusoma ·

Yaliyomo

Maana Ya Tafsiri

Tafsiri ni kitendo cha kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi). Kisha mawazo yanayolingana huwekwa badala yake katika lugha nyingine (lugha lengwa).

Mfasiri

Mfasiri ni mtu anayefanya tafsiri kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Sifa za mfasiri

  1. Ajue lugha zote mbili.
  1. Awe amesoma maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga. Halafu aweze kuyafikiria katika lugha lengwa.
  • Awe na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi.
  • Awe na uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.
  • Awe mjuzi wa TEHAMA.
  • Afahamu vizuri watu, jamii na utamaduni wa watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa.
  • Afahamiane na watu wengi, yaani ajichanganye na watu wa fani au sekta mbalimbali.
  • Awe na tabia ya kushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.

Mambo Ya Kuzingatia Katika Tafsiri

  1. Soma matini nzima

Hii itasaidia kubaini ni aina gani ya marejeo muhimu yatakayosaidia kutafsiri.

Mifano ya marejeo hayo ni kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.

  1. Baini lengo la matini chanzi

Kubaini lengo la matini kutakufanya utoe tafsiri safi inayoendana na habari unayoifasiri.

  1. Baini wasomaji lengwa (hadhira)

Mfasiri anatakiwa kujiuliza maswali haya ili aibaini hadhira ya tafsiri yake

  • Msomaji wa tafsiri yake ni nani?
  • Ana kiwango gani cha elimu? Ni msomi wa kawaida au msomi aliyebobea?
  • Wana umri gani na ni jinsia gani?
  • Hadhira yake imo katika tabaka gani katika jamii?

Kuibaini hadhira ya matini lengwa kutamsaidia mfasiri kuamua kuirahisisha tafsiri yake au kuifanya iwe ngumu. Uamuzi huo hutegemea uwezo wa hadhira ya tafsiri lengwa.

  1. Kubaini mtindo wa matini chanzi

Mfasiri anatakiwa kujua matini chanzi imetumia mtindo gani katika kuwasilisha maudhui yake.

  • Je, imetumia mtindo wa kirasimu?
  • Au imetumia mtindo wa kitaaluma?
  • Je, imetumia mtindo wa kiuandishi wa habari au mtindo wa kimawasiliano yasiyo rasmi?
  • Je, imetumia lugha rasmi au ya mtaani?

Mtindo wa matini chanzi unatakiwa kulingana na ule wa matini lengwa.

Tazama mfano ufuatao

Kingereza: Please, Sir do no mind it! If I arrive earlier, I'll wait for you

Kiswahili: Mkubwa! Kausha tu! Na kama nitatia maguu mapema, nitakusikilizia Palepale

Katika mfano huo, mitindo iliyotumika ni miwili tofauti.

Katika lugha chanzi, mtindo wa lugha uliotumika ni mtindo rasmi.

Katika tafsiri (lugha lengwa), mtindo uliotumika ni wa lugha ya mtaani. Jambo hilo si zuri katika tafsiri.

Mtindo wa lugha lengwa sharti ulingane na mtindo wa lugha chanzi.

  1. Kusoma matini kwa mara ya mwisho

Mfasiri anashauriwa aisome matini chanzi kwa mara ya mwisho. Anapoisoma, apigie mstari au aandike katika kidaftari kidogo mambo haya:

  • msamiati
  • istilahi
  • misemo muhimu ya matini chanzi, kama vile methali, nahau, maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k.

Kufanya hivyo kutamrahisishia mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri. Pia kutamsaidia asiyasahau wakati wa kutafsiri.

Mambo Ya Kuzingatia Wakati Wa Mchakato Wa Kutafsiri

  1. Maandalizi ya kutafsiri

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake na mtindo wa matini.

Pia anatakiwa kuweka alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri.

Anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi. Mifano ni methali, nahau, maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k.

Hii itamrahisishia kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri. Pia itamsaidia asiyasahau wakati wa kutafsiri, au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.

  1. Uchambuzi wa matini chanzi

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi. Ni yale aliyoyaandika au kuyapigia mstari katika hatua ya maandalizi.

Kisha ayatafutie visawe vyake katika lugha lengwa.

Hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.

  1. Uhawilishaji

Uhawilishaji ni uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa. Ni pia uhamishaji wa mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri.

Maana yake ni kwamba katika hatua hii, visawe vya kisemantiki (kimaana) vya matini chanzi huhamishwa kwenda matini lengwa. Visawe hivyo vilibainishwa katika hatua ya uchambuzi.

Kisha hupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake.

  1. Kusawidi / Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri

Katika hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia.

Kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi. Hivyo analazimika kuchunguza zaidi matini chanzi. Analazimika pia kupekua zaidi na zaidi marejeo aliyoyaandaa kwa ajili ya kuyatumia katika tafsiri.

Jambo la kuzingatia: mfasiri anapohamisha mawazo au ujumbe, azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili asiathiri tafsiri yake.

  1. Kudurusu / Kuipitia rasimu ya kwanza

Baada ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri. Aiweke kando kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake.

Kisha aanze kuidurusu (kuipitia) rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi. Aangalie kama kuna makosa yaliyojitokeza katika rasimu yake au la. Ayafanyie marekebisho pale inapobidi.

  1. Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu au watu wengine

Wasomaji hao wanaweza kuhakiki, kushauri, n.k.

Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri wenye mantiki.

  1. Usawidi / Kuandika rasimu ya mwisho

Baada ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kutumia maoni, mapendekezo na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake.

Hatimaye huandaa na kutoa rasimu ya mwisho. Rasimu hiyo huwa tayari kwa kusomwa na wasomaji.

Njia / Mbinu Za Tafsiri

Zipo njia mbalimbali zinazotumika katika kutafsiri. Baadhi ya njia hizo ni

  1. Tafsiri ya neno kwa neno
  2. Tafsiri sisisi
  3. Tafsiri ya kimaana / uwazi
  4. Tafsiri ya kimawasiliano
  1. Tafsiri ya neno kwa neno

Hii ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke. Hufasiriwa kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha.

Katika aina hii ya tafsiri, mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika.

Kwa kawaida, matini inayotafsiriwa huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi.

Tazama mfano ufuatao wa tafsiri ya neno kwa neno

Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi

Kingereza: He/past/study/until/morning

  1. Tafsiri sisisi

Tafsiri Ya Kisemantiki Na Ya Kimawasiliano

Maelezo ya mwanzo (mwisho wa aina ya tafsiri iliyotangulia)

Hii ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke. Mfasiri huzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha.

Hata hivyo, ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi, hasa kipengele cha kisintaksia cha lugha lengwa.

Tuangalie mfano ufuatao

Kingereza: He was taken at the Central Police Station

Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.

(iii) TAFSIRI YA KISEMANTIKI/MAANA AU UWAZI (Semantic Translation)

Hii ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi.

Katika aina hii, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo. Hufuata sarufi ya lugha chanzi, hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia.

Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.

Mfano

Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali

Kingereza: He went up to hospital

Faida ya tafsiri ya kisemantiki

Aina hii ya tafsiri ina faida kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa. Huingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi.

Mathalani, lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza. Baadhi ya miundo hiyo ni:

  • Kiswahili: Usiku mwema, kutoka Kingereza: Good night
  • Kiswahili: Mabibi na mabwana, kutoka Kingereza: Ladies and gentlemen

(iv) TAFSIRI YA KIMAWASILIANO/HURU

Hii ni aina ya tafsiri inayomlenga msomaji (hadhira) wa matini lengwa.

Msomaji huyu hatarajii kukutana na ugumu wowote katika matini atakayoisoma. Hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha yake, kwa kadiri itakavyoonekana.

Hivyo, mfasiri wa aina hii yuko huru kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno, methali, nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa.

Tafsiri ya kimawasiliano hufuata sarufi ya lugha lengwa. Pia ni lazima ifuate utamaduni, mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa.

Mifano

Kingereza: Jane married John

Kiswahili: John alimwoa Jane

Kingereza: No need to cry over spilt milk

Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki

Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo inayopatikana katika lugha lengwa. Methali hiyo huwa inahusiana au kukaribiana na ile ya lugha chanzi.

Zoezi

Jaribu kutafsiri misemo/methali zifuatazo za Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza

  • Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
  • Asiyekubali kushindwa si mshindani
  • Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa

Swali la kujiuliza

  • Ukalimani ni nini?

Maana Ya Ukalimani

Ukalimani umefasiliwa kuwa ni uhusishaji wa kuhamisha maana kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa) katika mazungumzo.

Hivyo basi, tunaweza kusema pia kuwa ukalimani ni hali ya mtu kuhamisha mawazo ya kinachozungumzwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine katika mazungumzo.

Hii ina maana kuwa ukalimani ni lazima uhusishe pande mbili.

Upande wa kwanza, sharti awepo mtu anayezungumza lugha fulani.

Upande wa pili, kunakuwa na mtu anayesikiliza kinachozungumzwa. Mtu huyo huyarudia hayo yanayozungumzwa kwa kutumia lugha nyingine, tofauti na ile iliyotumiwa na mzungumzaji wa kwanza.

Sifa Za Mkalimani Bora

  1. Awe mtu anayezielewa vizuri lugha chanzi na lugha lengwa.
  1. Awe mtu ambaye ameishi pande zote za lugha anazozikalimani, ili aelewe mila na desturi za watumiaji wa lugha hizo.
  1. Awe stadi wa ukalimani. Hapa anatakiwa awe na uhodari wa kukalimani na kuzungumza vizuri, na maneno yake yasikike. Awe na uwezo wa kukalimani neno kwa neno au sentensi kwa sentensi. Atumie ishara zinazoambatana na ishara za mzungumzaji wa lugha chanzi. Atumie pia mtindo anaodhani unaweza kuwavutia wasikilizaji wake.
  1. Awe muadirifu, yaani asiyeweza kupotosha au kubadili ukweli wa kinachozungumzwa. Hii ni muhimu kwa sababu wakalimani hutumika hadi mahakamani. Kama si muadirifu, anaweza kuufanya upande mmoja ukose haki inayostahiki.
  1. Asiwe mbaguzi. Hapa ina maana mkalimani asiamue kupotosha ukweli wa kinachozungumzwa kwa sababu tu kinakwenda kinyume na itikadi yake ya kisiasa, kidini, kiutamaduni, n.k. Pia asiangalie jinsia, umri wala hali ya mtu anayemfanyia ukalimani.

Mambo Ya Kuzingatia Katika Ukalimani

Kwa ujumla, yapo mambo kadha wa kadha ambayo mkalimani anatakiwa kuyazingatia anapotaka kufanya ukalimani.

Mambo hayo tunaweza kuyagawa katika makundi mawili

  1. Kabla ya kuanza ukalimani
  2. Katika ukalimani wenyewe

Kabla ya kuanza ukalimani

Katika hatua hii, mkalimani anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo.

(a) Awe na uelewa mzuri wa lugha zote anazotaka kukalimani. Hapa tuna maana kuwa awe na uwezo wa kuzungumza na kuelewa lugha chanzi na lugha lengwa. Hii itamsaidia kutopotosha kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi.

(b) Awe anaijua historia na utamaduni wa jamii zote mbili, yaani ile ya lugha chanzi na ile ya lugha lengwa.

(c) Kama ni ukalimani rasmi, ni vizuri mkalimani amjue mzungumzaji wa lugha chanzi. Ni vema pia afanye naye mazungumzo kidogo ili amzoee na atambue vionjo vyake. Hivyo itakuwa rahisi kwake, na wakati wa ukalimani hataonekana kama mgeni.

(d) Ni muhimu pia awe na uelewa mzuri wa mada inayozungumzwa. Hii itamrahisishia ukalimani wake.

Katika ukalimani wenyewe

Mkalimani anapokuwa amesimama mbele ya hadhira (wasikilizaji) pamoja na mzungumzaji wa lugha chanzi kwa ajili ya kuanza ukalimani, anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo.

(a) Awe makini katika kusikiliza kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi. Hii ni ili kuepuka kuachwa mahali na kuepuka kumuomba mzungumzaji kurudia mara kwa mara.

(b) Aitambue hadhira ya lugha lengwa. Ni watu wa namna gani? Wana kiwango gani cha elimu? Ni wasomi wa kawaida au waliobobea? Ni watu wa jinsia na umri gani? Hii itamsaidia kujua aina ya msamiati na miundo ya tungo atakayoitumia, iwe rahisi au migumu kulingana na hadhira yake.

(c) Atumie mitindo anayodhani itaeleweka vema na hadhira (wasikilizaji) wa lugha lengwa. Kwa mfano, kama hadhira ni vijana, ajaribu kutumia mitindo inayopendwa na vijana. Kama wasikilizaji ni watu rasmi, naye hana budi kuwa rasmi.

(d) Aweke mkazo sehemu ambazo mzungumzaji wa lugha chanzi anaweka mkazo. Hii ni ili kuepuka utofauti kati yake na mzungumzaji wa lugha chanzi, na kuepuka kuathiri lengo la mzungumzaji huyo.

(e) Atumie ishara zinazotumiwa na mzungumzaji wa lugha chanzi. Hii itawafanya wasikilizaji waamini kuwa kinachozungumzwa na mkalimani ndicho kilekile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi.

(f) Asiwe muda mwingi akimtazama mzungumzaji wa lugha chanzi na kusahau kuitazama hadhira yake. Anatakiwa kuitazama hadhira ili kugundua kama wako pamoja naye, au kuna sehemu ambazo hawajamwelewa, ili aweze kuwafafanulia zaidi.

(g) Amwombe mzungumzaji wa lugha chanzi kurudia sehemu anayodhani hakuisikia au hakuielewa vizuri. Ni kosa kwa mkalimani kukalimani sehemu au jambo ambalo hakulisikia vizuri au hakulielewa.

Dhima Za Tafsiri Na Ukalimani

  1. Hutuwezesha kujifunza lugha tofauti.
  1. Hutumika kama njia ya mawasiliano.
  1. Tafsiri na ukalimani hutumika kueneza utamaduni.
  1. Tafsiri na ukalimani zina dhima ya kuwasilisha ujumbe wa manufaa kwa watu ambao hawafahamu lugha chanzi (lugha asilia).

Changamoto Na Mapungufu Katika Tafsiri Na Ukalimani

  1. Tofauti za kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa:

Tofauti za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiingereza wakati mwingine husababisha matatizo au upungufu katika tafsiri na ukalimani.

Kwa mfano, maumbo ya vitenzi vya Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonyesha umoja au wingi wa wahusika. Pia hazionyeshi majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa.

Maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ni tofauti. Huonyesha umoja na wingi wa wahusika, na hata kuwa na majina ya vitu husika.

Tazama mfano ufuatao kama ulivyotolewa na Mwansoko (2006)

Kiingereza: No parking

Kiswahili: Usiegeshe gari hapa

(Je, kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?)

Vilevile, tofauti za maana kati ya lugha ya Kiingereza na Kiswahili zinaweza kuathiri tafsiri au ukalimani. Mathalani:

Kiswahili: Wasiojiweza

Kiingereza: Disabled

(Si wote wasiojiweza ni walemavu, na si walemavu wote hawajiwezi.)

  1. Tofauti za mitindo kati ya lugha chanzi na lugha lengwa:

Tofauti za mitindo ya uzungumzaji pia zinaweza kuathiri tafsiri na ukalimani. Hii ni kwa sababu unaweza kukuta mtindo fulani unatumika katika muktadha fulani, lakini ukashindwa kupata tafsiri katika lugha nyingine katika muktadha ule ule. Mathalani:

Kiingereza: (i) Thou shall not steal (mtindo wa kidini)

Kiswahili: Usiibe

Kiingereza: Do not steal (mtindo wa kawaida)

Kiswahili: Usiibe

Kiingereza: (ii) Lend me your ears (mtindo wa kishairi)

Kiswahili: Naomba mnisikilize

Kiingereza: May I have your attention (kawaida)

Kiswahili: Naomba mnisikilize

Tafsiri zote tulizoziangalia katika mfano (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ileile iliyomo katika matini chanzi. Hata hivyo, tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha uliotumika katika matini chanzi.

  1. Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa:

Tofauti za kiutamaduni ni tofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa. Tofauti hizi zinaweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu.

Kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza kuna milo minne, wakati Waswahili wana milo mitatu. Hii hufanya iwe vigumu kupata dhana za milo hiyo ya Waingereza katika dhana ya Kiswahili.

Mfano

Waingereza wana: Breakfast

Waswahili wana: Kifungua kinywa

Waingereza wana: Lunch

Waswahili wana: Chakula cha mchana

Waingereza wana: High tea

Waswahili wana: ?

Waingereza wana: Dinner

Waswahili wana: Chakula cha jioni

Waingereza wana: Supper

Waswahili wana: ?

Mifano Ya Tofauti Za Kiutamaduni

Ukiangalia mifano hiyo, utaona kuwa ni vigumu kupata dhana za high tea na supper katika lugha ya Kiswahili. Sababu ni kwamba hakuna utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo kwa siku.

Pia ni vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama ugali na makande katika lugha ya Kiingereza. Sababu ni kwamba hakuna vyakula vya aina hiyo.

Tofauti Za Kiitikadi Kati Ya Lugha Chanzi Na Lugha Lengwa

Tofauti za kiitikadi pia zinaweza kuathiri tafsiri na ukalimani. Sababu ni kwamba wafasiri wengi, hasa waandishi wa habari, huegemea zaidi katika itikadi.

Mifano

  • Kiingereza: Businessman. Kiswahili: mlanguzi. Tafsiri hii inatokana na mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ujamaa.
  • Kiingereza: Businessman. Kiswahili: mfanyabiashara. Tafsiri hii inatokana na mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ubepari.
  • Kiingereza: Freedom fighter. Kiswahili: wapigania uhuru. Hii ni tafsiri ya vyombo vya habari vya Tanzania wakati wa kupigania uhuru.
  • Kiingereza: Freedom fighter. Kiswahili: magaidi. Hii ni tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika Kusini wakati huo.

Hitimisho

Tunaweza kusema kuwa ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango ambacho mila na desturi za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana au zinafanana.

Idara Ya Tafsiri Na Ukalimani Ya Bakita

Tafsiri na ukalimani ni taaluma muhimu. Kwa sababu hiyo, serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) imeanzisha idara maalumu ya Tafsiri na Ukalimani.

Idara hiyo ina majukumu yafuatayo

  • Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mbalimbali kwa mashirika, idara, wizara, balozi na watu binafsi.
  • Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa, na katika shughuli za mashirika, makampuni na watu binafsi.
  • Kupitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na asasi mbalimbali au wafasiri wa nje.
  • Kutoa ushauri kuhusu masuala ya tafsiri na ukalimani.